23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Waamua kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa kuwapima wanawake saratani

AVELINE KITOMARY

HUWA ni jambo la kawaida katika jamii watu kusherekea sikukuu zao za kuzaliwa kwa njia tofauti, ili mradi mhusika afurahi.

Utofauti wa aina ya sherehe huzingatia mazingira na umri wa wanaosherehekea na aina ya sherehe.

Katika makala hii ya afya na jamii, leo tunakuletea simulizi ya wasichana watatu ambao walizaliwa tarehe moja na mwezi mmoja  na kuwa marafiki wa miaka zaidi ya nane sasa.
Safari yao ya urafiki ilianza walipokutana   kwa nyakati totafuti, baada ya kujua kuwa wamezaliwa siku moja na mwezi mmoja wakaamua kuungana. Hiyo ilikuwa mwaka 2013 jijini Dar es Salaam .

Tangu walipokutana katika urafiki wao  wasichana hao Irene Ketegwe, Iman Hatibu na Rosemary Marwa, walikuwa na desturi ya kusherekea siku yao ya kuzaliwa pamoja.

Lakini kwa mwaka huu, mambo yamebadilika wamejikuta wakisherehekea siku ya kuzaliwa wakiwa wawili badala ya watatu.

Hiyop imetokana na mmoja wao kutangulia mbele ya haki June, mwaka huu, kutokana na maradhi ya saratani ya kizazi (calvic canser).

“Hisia na maumivu ndizo ziliamua namna ya kusherehekea siku yetu ya kuzaliwa kwa mwaka huu, hatukuwa na jinsi lakini sasa tumeamua kufanya kitu katika jamii ili kupunguza maumivu yetu.

“Maumivu zaidi yalikuja baada ya kuona ni uzembe kumpoteza rafiki yetu tuliyezaliwa naye siku moja kwa sababu ya ugonjwa unaoweza kutibika, kwani tulitarajia kuwa watatu katika kusherehekea siku hii muhimu kwetu,” anasema Irene ambaye pia ni daktari katika Hospitali ya Agha Khan.

Wakizungumza na MTANZANIA, wasichana hao wawili Iman na Dk. Irene   wanasema kutokana na pigo walilopata la kumpoteza mpedwa wao, wameamua kufanya sherehe yao ya siku ya kuzaliwa kwa kupima wanawake saratani ya shingo ya kizazi.

Wasichana hao wanasema kufanya hivyo ni kukataa uzembe wa kumpoteza rafiki yao  Rosemary kwani ugonjwa huo unatibika endapo ukigundulika mapema.

“Kwa kazi yangu ya udaktari, mara kadhaa nimewafanyia watu uchunguzi wa awali wa  saratani ya shingo ya kizazi  ila mimi binafsi nilikuwa sijawahi kufanya uchunguzi.

“Sio kwamba nilikuwa sijaona umuhimu, lakini unajua kiubinadamu wanasema mganga hajigangi hivyo, inawezakana jambo hilo ambalo unakumbushia wenzio lakini wewe unasema kesho nitafanya na siku ndio zinazidi kwenda.

“Binafsi nina jukwaa la kufanya hivyo nikisema nataka kufanya nitaingia chumba  cha daktari mwenzangu kwahiyo, nilikuwa nasema iko siku nitafanya,” anaeleza Dk. Irene.

Anasema alipogundua rafiki yake Rosemary anaugua saratani ya kizazi alishtuka na hivyo akaamua kupima ili kujua hali yake kiafya.

“Nakumbuka mwaka jana kwenye mwezi wa kumi na moja hivi, Rosemary alinipigia simu akaniuliza pacha uko wapi? Nikamwambia niko mijini Dar, tukazungumza mengi akaniambia anaumwa kansa ya kizazi.

Dk. Irene anaeleza kuwa waliweza kumuuguza rafiki yao  lakini kwa bahati mbaya alifariki.

 “Ilikuwa ni mshtuko mkubwa kwangu kwa sababu alikuwa binti mdogo, kwa mwaka huu ilikuwa atimize miaka 30 kwenye siku ya kuzaliwa sisi  kwa sababu tulizaliwa naye siku moja  ni kitu ambacho  kilituumiza.

Anasema kutokana na kifo hicho, mwaka huu wameamua kuadhimisha siku yao ya kuzaliwa kwa kuwapima wanawake saratani ya shingo ya kizazi.

“Tumeamua kufanya hivi kwa sababu saratani ya shingo ya kizazi inazuilika na  kuna chanjo ambayo sasa serikali inatoa kupitia Wizara ya Afya  kwa mabinti wenye miaka 14 waliopo shuleni.

“Inapogundulika mapema inaweza  kutibiwa, tatizo letu tunachelewa kupima na hivyo kugundulika ikiwa katika hatua za mwisho,” anabainisha.

Anaongeza: “Kwa nchi zilizoendelea, idadi ya watu wanaougua saratani ya mlango wa kizazi inapungua lakini hapa kwetu inaongezeka na vifo ni vingi.

 “Tulifikiria tukaona kwamba shida kuu ni watu kutofahamu na wengine wanapata tu hofu na huenda hawana jukwaa la kusemea, hawajui wazungumze na nani na waanzie wapi.

“Kwahiyo, tumekubaliana tujaribu kudhamini angalau wanawake wachache ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku yetu ya kuzaliwa.”

Anasema katika upimaji huo wameweza kudhamini wanawake 100 huku waliojitokeza kupimwa wakiwa ni 60. 

Dk. Irene anasema kuwa asilimia 99.9 ya wanawake ambao wameanza kufanya mapenzi wako kwenye hatari ya kupata saratani ya shingo ya  kizazi.

UELEWA WA JAMII

Kwa upande wake Iman Hatibu, ambaye ni Msimamizi wa Masuala ya Jinsia kutoka Policy Forum, anasema wanawake wengi hawana  uelewa kuwa saratani ya mlango wa kizazi ipo na inatibika.

“Wakati mwingine wanakuwa ni waoga  wa kwenda kupima, wengine wanadai kuwa  ukienda kupima inauma au wanapata hofu  kwamba akikutwa na saratani hatapona tena, itakuwa ndio mwisho wa maisha yake.

“Tukaona ni bora tuwaambie wanawake, tuwaelimishe na kutoa taarifa kwamba huu ugonjwa unatibika ukiwahi, kwahiyo ni vizuri kujua kwamba  ninao au sina ili ujue  jinsi ya kujikinga kwa sababu ukishapima hapa unaambiwa tena uje kufanya tena uchunguzi, tuliona ni jambo zuri,” anaeleza.

Anasema wanawake waliopata vipimo wanasema zoezi hilo limewasaidia na wamenufaika kwa sehemu kubwa.

“Kwa sababu kuna mwingine alitaka kufanya lakini hakupata nafasi ya kufanya au mwingine hana uwezo wala wengine hawajui gharama za upimaji.

“Tunawaelimisha jamii kuwa wasichelewe kama rafiki yetu Rosemary kwamba saratani ya kizazi ikifika hatua ya mwisho unashindwa kutibu wakati ukiwahi  unatibika.

Anasema wanapanga zoezi hilo kuwa endelevu kutokana na uhitaji mkubwa kutoka kwa wanawake kutakiwa kufanya uchunguzi wa saratani hiyo.                                   

“Hatuwezi kusema kuwa zoezi hili litafanyika siku ya kuzaliwa, tunapanga kwani kwa kila tarehe ya kuzaliwa tunaona ni mbali tunataka na hapa katikati tufanye huduma kama hili.

“Tutaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu saratani ya mlango wa kizazi ya kwamba inatibika mimi nafanya kazi katika taasisi binafsi kwahiyo nafanya masuala ya jinsi nitaendelea kuongea na wanawake nitawaelimisha na nitaendelea kutoa rai kwa wanawake wenzangu.

“Hapa Agha Khan gharama tulizotumia ni Sh 50,000 kwa mwanamke mmoja,” anaeleza Iman.

WITO KWA JAMII

Iman na Dk. Irene wanaishauri jamii  kusherekea siku zao za kuzaliwa kwa kuacha alama katika jamii hasa kwa upande wa afya.

 “Tunashukuru kwa ushirikiano tulioupata kwa hospitali ya Agha Khan kwaajili vipimo, wameweza kutoa wafanyakazi na unaona hadi sasa muda wa kazi umeshaisha lakini bado wanatoa huduma.

SARATANI MLANGO WA KIZAZI NI NINI?

Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Ujue Ugonjwa wa Saratani’ kilichoandikwa na Daktari Bingwa wa Ugonjwa huo kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk.  Hellen Makwania, ni aina ya saratani inayoshambulia seli/chembechembe zilizoko ndani ya ngozi laini inayozunguka shingo ya kizazi.

Tafiti zinaonyesha kwa asilimia kubwa saratani hii ya shingo ya kizazi inasababishwa na kirusi kiitwacho Human Papilloma Virus (HPV) ambacho huenezwa kwa njia ya kujamiiana.

Kupitia kitabu hicho Dk. Makwania ameanisha kuwa saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza hapa nchini kwa asilimia 56.6 ikifuatiwa na saratani ya matiti ambayo ni asilimia 12.8.

TABIA HATARISHI

Anasema kuna tabia au hali hatarishi ambazo zinachangia mtu kupata saratani ya shingo ya kizazi.

Ikiwa ni pamoja na kuanza ngono katika umri mdogo (chini ya miaka 18).

DALILI

Anasema dalili zinaweza kujitokeza wakati ugonjwa upo katika hatua za mwisho ambazo ni pamoja na kutokwa damu isiyo ya hedhi ukeni, kutokwa na damu ukeni baada ya kujamiiana na kutokwa na damu ukeni kwa wanawake waliokwisha kukoma hedhi.

Anazitaja dalili zingine kuwa ni damu inayochanganyikana na majimaji ya uke, matone ya damu au damu kutoka kipindi kisicho cha hedhi, kutokwa na majimaji au uchafu ukeni wenye harufu mbaya na wakati mwingine ukiwa umechanganyika na damu.

“Vilevile mtu anaweza kupata maumivu wakati wa kujamiiana, maumivu chini ya tumbo, nyonga na kiunoni, kukojoa mkojo wenye damu, kupitisha mkojo na haja kubwa kwenye uke na upungufu wa damu.

NAMNA YA KUGUNDUA

Anasema saratani ya Mlango wa kizazi inaweza kugundulika endapo mhusika atapima.

“Vipimo vya uchunguzi vinavyofanyika ni pamoja na Pap Smear, kipimo hiki ni rahisi na hakina madhara yoyote. Inashauriwa kufanya kipimo hiki mara moja kwa mwaka,” anasema.

Anasema huduma za matibabu hutolewa kwa kufanya upasuaji katika hatua za mwanzo za ugonjwa, mionzi, dawa za saratani ama mionzi pamoja na dawa za saratani.

NAMNA YA KUJIKINGA

Anasema mtu anaweza kujikinga na saratani ya shingo ya kizazi kwa kupata chanjo ya ‘Human Papilloma Visur’.

“Njia nyingine ni kuepuka ngono katika umri mdogo, kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu, kuepuka kuvuta sigara, kufanyiwa uchunguzi wa saratani hiyo angalau mara moja kwa mwaka, tiba kamilifu ya magonjwa ya ngono (STI) na kupunguza mafuta mengi kwenye chakula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles