30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Augua miaka 23 sasa, mke amkimbia

AVELINE  KITOMARY

KATIKA maisha ya kila siku, binadamu hukutana na huzuni na furaha kwa kila hatua anayoipitia ikiwa ni sehemu ya maisha.

Licha ya huzuni na furaha, lakini wapo pia ambao maisha yao hayana matumaini tena kutokana na mambo yanayowasibu.

Ukosefu wa kipato, magonjwa, mifarakano na matengano ni vitu ambavyo  kwa kiasi kikubwa huifanya jamii kunyong’onyea.

Wapo watu ambao wameshakata tamaa na kusubiri mwisho wa maisha yao hapa duniani kutokana na matatizo ya muda mrefu.

Waswahili wanasema; ‘ya mwenzako sikia  usiombe yakukute.’ Usemi huu unaweza kuwa na maana kubwa  kwa Mohammed Ally Ngondu,  mwenye umri wa miaka 68, mkazi wa Mbagala jijini Dar es Saalaam, ambaye anasumbuliwa na maradhi kwa miaka 23 sasa.

Anasema alizaliwa akiwa mzima kabisa  huko mkoani Lindi, mwaka 1952  na kulelewa na wazazi wake wawili.

“Katika familia yetu tulizaliwa tukiwa wawili mimi na mdogo wangu wa kike na tuliishi Lindi lakini baba yetu hakuwa mwenyeji wa hapo, kwao ni Tunduma.

“Licha ya kujua kuwa baba yetu kwao ni Tunduma, hatujawahi kubahatika kwenda kwa ndugu zake hata hivyo nikiwa na miaka sita aliondoka kurudi kwao na tangu hapo hatujaonana.

“Mwaka 1976 nilisikia kuwa kafariki, baada ya kupata hiyo taarifa hatukuwahi kujua tena nini kinaendelea na wala sijawahi kuwajua ndugu zake, tuliendelea kulelewa na mama yetu Lindi.

“Nilipelekwa shule, nikasoma nilipofika  darasa la nne kwa bahati mbaya sikufaulu hivyo na elimu kwangu ikawa basi tena, ukizingatia kipindi kile maishi yalikuwa magumu,” anasema.

Anasema kuwa baada ya kulelewa  na mama yao kwa muda mrefu mwaka 1974 aliamua kuhamia katika Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta maisha.

“Nilivyokuja mwaka huo nilikuwa naishi Tandika na kwenye mwaka 1984 nikahamia Chamazi ambako ndio ninaishi hadi sasa.

“Mwaka 1995 tukapata msiba wa dada yangu ambaye tulizaliwa wawili, ulikuwa msiba mkubwa kwangu kwa sababu nilifikiria kuwa sina ndugu mwingine ndio basi tena tukamzika Lindi tukaendelea na maisha.

“Mwaka 2001 nilikuja kupata pigo lingine la kufiwa na mama kwahiyo nikawa nimebaki mwenyewe na kwa wakati huo nilikuwa bado hata sijaoa.

“Kipindi cha nyuma nilikuwa na mawasilino na wajomba zangu huko ambao wameshafariki, katika ukoo wetu hatukuwa wengi, asilimia kubwa hawapo tena duniani; ni kama ukoo umekwisha,” anasimulia kwa masikitiko.

AJALI ILIVYOHARIBU NDOTO YAKE  

Mwaka 1998 ulikuwa ni mbaya zaidi kwa Mohamed, hii ni baada ya kupata ajali iliyogharimu maisha yake yote.

Anasimulia: “Mwaka huo nilitumwa kwenda kununua ubao, ule ambao Waislamu wanautumia wakati wa mazishi, nikiwa natembea barabarani maeneo ya Mbagala, nyuma yangu  kulikuwa na gari la abiria maarufu daladala, mlango wake ukakatika ukaja kunigonga nikaanguka chini.

“Baada ya hapo, walinipeleka hospitali ya  Temeke wakanitibia, baada ya miezi mitatu  nikapata nafuu kwani nilichubuka sehemu za miguu na mgongo.

“Hata hivyo, baada ya kupata nafuu mguu ukaanza tena kunisumbua ukawa unajoto kali, ugonjwa ukarudi kidogo kidogo lakini nikuwa nafanya shughuli zangu za ufundi seremala kama kawaida, na kwa wakati huo nilikuwa tayari nimeshaoa.

Anaeleza kuwa ilipofika mwaka 2006 ugonjwa ulizidi zaidi na hata alipokwenda Hospitali ya Muhimbili hakupata nafuu yoyote.

“Nilikuwa nikifanya kazi, nikishika nyundo mikono inakosa nguvu, ikafika mahali hata kula mwenyewe nikawa siwezi tena.

“Muhimbili walinichoma sindano kwenye pingili mgongoni lakini hali ilizidi kuwa mbaya zaidi, sikuweza kusimama  kwa sababu ya mgongo kuuma na kiuno hivyo hadi leo hii sinyanyuki hapa na wala sijui ninaugonjwa gani,” anasema Mohamed.

Anasema wapo watu wanaohusisha tukio la ugonjwa wake na imani za kishirikina hata hivyo, hajapata mtu wa kumsaidia katika njia hiyo.

“Kuna watu wanasema kwamba nimerushiwa jini na wengine wanasema haiwezekani umerogwa, lakini mimi sijawahi kwenda kutafuta tiba asili na sio kwamba sitaki ni kwa sababu sina uwezo wa kifedha la sivyo ningeenda ili nipate kupona,” anabainisha Mohamed.

MKEWE AMKIMBIA

Anasema ugonjwa ulivyomzidi na hata kufikia hatua ya kushindwa kuingiza kipato, mkewe wa ndoa alimkimbia.

“Kwa sasa sina familia, mke wangu alinikimbia baada ya kuona siponi kila siku hali inazidi kuwa mbaya. Katika ndoa yetu hatukubahatika kupata mtoto hivyo hata mawasiliano hatuna kabisa, sijui yuko wapi.

“Tangu wakati huo nikawa sina mtu wa kuniangalia nahudumiwa na majirani tu, watu wanaopita hapa akinionea huruma anakuja kunisaidia wengine wananiogesha, wananipa chakula lakini sina ndugu wa kuzaliwa nao wote wamefariki.

Anasema kuwa angekuwa na ndugu anaamini asingekuwa anaishi maisha ya mateso kama anayoishi sasa.

“Ndugu zangu ndio hawa wanaopita barabarani, wananisaidia wengine wananiletea sabuni, maji na mahitaji mengine muhimu. Kila mtu akipita hapa akiniona ananisaidia maisha yanaendelea.

MGOMO WA MADAKTARI ULIVYOMWATHIRI

Anasema mwaka 2007 alipangiwa na daktari kupata vipimo na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, lakini kwa wakati ule mgomo wa madaktari ulimfanya akakosa nafasi ya matibabu. 

“Ilibidi matibabu yaahirishwe na ikawa vigumu tena kwenda hospitali, mgomo huo uliniathiri kwani  ilibidi nipate matibabu lakini nikakwama kutokana na suala hilo licha ya kwamba nilipata watu wa kunisaidia matibabu lakini haikuwezekana.

“Matibabu yangu ni ghali, kutoka hapa nilipo ukikodi bajaji hadi Muhimbili ni Sh 30,000 na sina huo uwezo wa kifedha.

Mohamed anasema anakabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa zaidi ikiwa ni njaa, kwani anaweza kukaa hata siku mbili bila kupata chakula.

“Siwezi kunyanyuka hapa nilipo, nikisikia mtu anapita barabarani (chumba chake kipo karibu na barabara) namwita namwambia naomba chakula.

“Hivyo kuna wakati ninaweza kushinda na njaa hata siku mbili, nasubir tu huruma ya majirani zangu na wapiti njia.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni mahali pa kuishi, kwa sababu sehemu anayoishi ni kwenye nyumba ya rafiki yake ambaye pia alishafariki.

“Nilikuwa na urafiki naye tangu mwaka 1993 na maradhi yaliponipata alinisaidia na kunitunza hapa kwake hadi alipofariki kwa maradhi ya saratani.

“Tangu alipofariki nimeendelea kuishi hapa na watoto wake ambao wamenipa eneo dogo ili niweze kujenga chumba changu lakini uwezo huo sina kutokana na hali yangu,” anaeleza.

AOMBA MSAADA  

Kutokana na hali yake mbaya ya kiafya na kiuchumi, Mohamed anaomba Watanzania wamsaidie ili aweze kupata matibabu na huduma muhimu ikiwamo chakula na kujengewa sehemu ya kuishi.

“Nawaomba Watanzania wanisaidie nijengewe pa kuishi ili niweze kuondoka katika nyumba hii kwa sababu nilishapewa eneo dogo la kujenga.

“Naomba wanisaidie, hapa nilipo hali yangu sio nzuri, watu wa dini zote na yeyote mwenye moyo mzuri wa kunihudumia naomba msaada wake niweze kupata chumba changu na chakula.

“Kingine natamani  kupata vipimo vya mwili mzima, vile vikubwa ili ijulikane ninaumwa nini kwasababu hapa tunafanya kuhisi tu kuwa sababu ni ajali, hapa nilipo sina mtu wa kunipeleka hospitali  lakini natamani kupata tiba.

“Nilishakwenda  hospitali kipindi cha nyuma, wakaniambia hadi niwe na kiasi cha Sh 350,000  kipindi  hicho kupata hela hiyo ilikuwa mtihani hasa na mimi nilikuwa na msamaha wakaniambia wataniatolea 200,000 na  iliyobaki 150,000 nitoe mimi lakini bado nilishindwa,” anasema Mohamed.

Anaomba kwa mtu yoyote mwenye kutaka kumsaidia amtafute kwa namba 0652798041 ampe mchango wowote aliojaaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,391FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles