30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Vyama vyaja na mikakati zaidi Uchaguzi Mkuu

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

AJENDA kubwa ya nchi kwa mwaka huu ni kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ambao ni wa sita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.   

Tayari vyama mbalimbali vya siasa vimeanza kujiandaa kuelekea katika uchaguzi huo ambao ni maalumu kwa ajili ya kumpata rais, wabunge na madiwani.

 Joto la uchaguzi huo limezidi kupanda kwa vyama mbalimbali ambavyo vimekuwa na mikakati ikiwemo ya maandalizi ya ilani za uchaguzi na namna ya kuwafikia wapigakura wengi hasa wa ngazi ya chini.

CCM NA MAANDALIZI YA ILANI

Mwenyekiti wa CCM, Dk. John Magufuli, ameagiza kuandaliwa kwa Ilani ya Uchaguzi ya 2020/25 itakayoainisha mambo muhimu yanayogusa wapigakura.

Akizungumza hivi karibuni wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) jijini Mwanza, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa NEC kuhakikisha inatengeneza ilani ya chama hicho kwa mwaka 2020/25 sambamba na sera au mpango wa utekelezaji wa serikali katika miaka 10 ijayo (2020/30) yenye mwelekeo wa kiuchumi unaotegemea sekta ya viwanda na kulifanya Taifa lijitengemee kiuchumi.

“Lazima ilani hii tutakayokuwa tumeitengeneza ama uelekeo wa Chama cha Mapinduzi , ujielekeze kwenye namna tunavyoweza kutumia rasilimali tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kujiletea maendeleo na mabadiliko makubwa kiuchumi sisi kama taifa,”alisema Rais Magufuli.

Miongoni mwa mambo ambayo Rais Magufuli aliwataka wajumbe wa NEC kuyapa kipaumbele ni pamoja na afya, elimu, maji, kilimo na mifugo, madini, utalii na miundombinu.

Kuhusu Afya Rais aliwataka wajumbe kuhakikisha wanazingatia sera ya kuwa na kituo cha kutoklea huduma ya afya kila kata, kijiji na mtaa.

Pia Rais alisisiza sekta ya elimu kupewa kipaumbele kwa kujikita kuinua ubora wa elimu ya msingi, sekondari na kuhakikisha zinakuwa na mazingira yanayofaa.

Kuhusu sekta ya maji alisema lengo liwe kuongeza vyanzo vya maji na kasi ya usambazaji ili kujitosheleza mahitaji kwa asilimia 100 mjini na vijijini.

Kilimo na mifugo alisema ni vyema sekta hiyo ikapewa msukumo mpya wa kipekee, kwa kuwa ndio kichochea cha sekta ya viwanda.

Kwa upande wa madini Rais Magufuli alisema ilani iwe na lengo la kuhakikisha madini yote yanasindikwa na kuongezwa thamani kabla ya kuuzwa na kuwajengea uwezo wazawa wa kuwekeza kwenye sekta hiyo.

Kuhusu miundombinu, alisema lengo ni kuendelea kujenga mtandao wa barabara kwa uunganisha wilaya zote na kuhakikisha barabara mapaka mitaa zinajengwa.

Pamoja na maagizo hayo Mwenyekiti huyo wa CCM aliwataka viongozi wa kupitia chama hicho kutojisahau na kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa hata CCM inaweza kuanguka kama ilivyotokewa kwa vyama vingine vikongwe duniani.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, anasema chama hicho kitashinda kwa kishindo kama ilivyotokea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, CCM kilishinda mitaa yote 4,263 huku wagombea 316,474 wakipita bila kupingwa.

Alisema kazi kubwa ambayo inawakabili viongozi na wanachama CCM ni kuhakikisha wanakuwa kitu kimoja katika kutekeleza majukumu yao kwa kuingiza wanachama wapya, jambo ambalo litasaidia kuendelea kushika nafasi katika Uchaguzi mkuu ujao na kuendelea kukaa madarakani.

Anasema ili wana CCM waweze kuwa wamoja ni lazima waheshimiane na kuacha kudharauliana na jambo hili ni lazima lianze kwa viongozi ambao wamepewa madaraka ya kusimamia wenzao.

Dk. Bashiru anasema endapo kutakuwa na ofisi za umma kutakuwa na watu ambao wanachelewesha kazi au wanatumia vibaya madaraka waliopewa pamoja na kudai rushwa ili waweze kutoa huduma kwa wananchi hao watakuwa wanahujumu umoja wao.

KURA NNE ZA CHADEMA

Wakati hali ikiwa hivyo kwa CCM, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanaamini kuwa kwa sasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekuwa imara zaidi kwani pamoja na kuondokewa na makada wake waliokuwa wakishikilia nafasi za udiwani, hakijaparaganyika badala yake viongozi wamshikamana.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, anasema kazi kubwa atakayoifanya ni kuongoza Chadema kuchukua dola katika uchaguzi huo.

Mnyika ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni, mapema wiki hii alikaririwa na gazeti hili akimuomba Rais Dk. John Magufuli kuandaa utaratibu utakaowezesha Watanzania kupiga kura za aina nne, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Alisema utaratibu huo, utamwezesha mwananchi kupiga kura ya kumchagua rais, mbunge, diwani na kura ya maoni juu Katiba mpya ambayo itaweka uhalisia Watanzania wanahitaji Katiba mpya au la.

Anasema kama utaratibu huo, utashindikana ni vema Serikali kwa kushirikiana na Bunge kufanya marekebisho ya mpito kwenye Katiba iliyopo sasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2020 ili kuwa na tume huru ya uchaguzi.

Anasema muda uliobaki kabla ya uchaguzi huo, haiwezekani kukamilika kwa mchakato mzima wa katiba mpya, inawezekana kufanyika marekebisho ya muda ili kukidhi matakwa ya wananchi yakiwamo kupinga matokeo ya rais mahakamani na kuwa na tume huru.

“Nilipochaguliwa katibu mkuu kuna vipaumbele karibu vitano nilijiwekea kikiwamo cha kudai tume huru ya uchaguzi, mpya kwa bahati nzuri watanzania wanayo rasimu ya Katiba mpya ya Jaji Joseph Warioba ambayo kwa namna moja au nyingine iliharibiwa na watu wachache.

“Mara kadhaa Rais Dk. Magufuli amenukuliwa akisema Katiba mpya siyo kipaumbele chake, wakati kwenye ilani ya chama chake ni miongoni mwa mambo ambayo waliahidi kuyatekeleza, alipokuja kuzindua Bunge mjini Dodoma alihiadi, tunashangaa anabadilika,tunapaswa kuchukua tahadhari kwa kumtaka  aruhusu mchakato uendelee.

“Kwa kuwa muda uliobaki kwenda kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu ni mchache, tunamshauri rais aandae utaratibu utakaowezesha mwananchi kupiga kura ya kumchagua diwani, mbunge, rais na kupira kura ya maoni juu ya katiba mpya, hapo tutaona uhalisia kama Watanzania wanahitaji jambo hilo au la.

“Sote tunajua Katiba mpya ni ya miaka kuanzia 50 na kuendelea,kama  mchakato huio utakuwa mgumu, basi kabla ya uchaguzi lazima tufanye marekebisho ya mpito kwenye katiba yetu ili tupate tume huru ya uchaguzi  na matokeo ya rais kupingwa mahakamani vingine nguvu ya umma itatumika ili kupata ushindi,”alisema.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anasema wamejipanga kuhakikisha hawafanyiwi figisu.

Akizungumza hivi karibuni katika mkutano mkuu wa Baraza la Wanawake  wa Chadema (Bawacha) uliofanyika jijini Dar es salaam, Mbowe anasema pamoja na kuzuiliwa kufanya mikutano ya hadhara walikuwa wakiendelea kufanya siasa kimya kimya za mtu kwa mtu, nyumba kwa nyuma na kitongoji kwa kitongoji na kusajili wanachama zaidi ya milioni sita  

“Leo hii sitamani mikutano ya hadhara, natamani kufanya siasa za namba, namba hazidanganyi tuliamua kufanya kimyakimya pasipo kushirikisha au kutangaza kwenye vyombo vya habari na tulifanikiwa”anasema Mbowe.

CUF YAHIMIZA MARIDHIANO

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, anamuomba Rais Magufuli kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ili kuweka mazingira mazuri ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2020 na kuwa wa huru na haki.

Akitoa salamu za mwaka mpya wa 2020 anasema amani ya kweli ya nchi itaathirika ikiwa yaliyofanyika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na chaguzi za marudio yataendelea kwenye uchaguzi wa 2020.

“Ushiriki wa wananchi katika kuamua mambo yanayogusa maisha yao ni suala muhimu la maendeleo endelevu, na ujenzi wa demokrasia ni sehemu muhimu ya maendeleo. Kuwanyima wananchi kuchagua viongozi wanaowataka ni kudumaza maendeleo ya kisiasa na kijamii,” anasema Profesa Lipumba.

UCHAGUZI WA SITA

Uchaguzi wa mwaka 2020 ni wa sita tangu chaguzi za vyama vingi kuanza tena nchini ukitanguliwa na chaguzi kama hizo za mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.

Katika chaguzi zote za awali, CCM ilitangazwa kuongoza kwenye nafasi zote ilizowania katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Benjamin Mkapa alishinda urais wa Muungano mwaka 1995 kwa asilimia 61.8, akashinda tena kwa asilimia 71.7 mwaka 2000, ambapo Jakaya Kikwete alishinda kwa asilimia 80.28 mwaka 2005 na tena kwa asilimia 62.8 mwaka 2010.

Kwa upande wa Zanzibar, Salmin Amour Juma, alitangazwa mshindi kwa asilimia 50.2 mwaka 1995, huku Amani Abeid Karume akitangazwa kwa asilimia 67.04 mwaka 2000 na asilimia 53.1 mwaka 2005 na mwaka 2010, Dk. Ali Mohamed Shein akatangazwa mshindi kwa asilimia 50.1.

Hata hivyo uchaguzi uliopita (2015) ulikuwa na ushindani mkali tangu kurejeshwa kwa historia ya vyama vingi nchini.

Katika matokeo ya mwaka 2015 kwa nafasi ya Rais CCM kupitia Dk. Magufuli walishinda kwa asilimia 58.46 akiwa na kura 8,882,935 huku mgombea wa Chadema, Edward Lowassa alipata kura 6,072, 848 sawa na asilimia 39.97

Lowassa alisimama kugombea kiti cha uraisi kupitia Chadema wakiwa katika muunganiko wa vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, uliounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanatahadharisha Watanzania kuwa waangalifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwani jambo la msingi ni kumchagua mgombea anayefaa ambaye atakuwa ni msaada kwenye maendeleo yao na si anayeangalia masilahi yake binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles