Gabriel Mushi, Dodoma
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amewasilisha bajeti ya Sh bilioni 143.3 kwa mwaka wa fedha 2018/2019, yenye vipaumbele 13.
Akiwasilisha bajeti hiyo leo Mei 10, bungeni jijini Dodoma, Mwijage amesema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 43.3 ni za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 100 ni za matumizi ya maendeleo.
Mwijage amesema vipaumbele vya wizara hiyo kwa kushirikiana na taasisi zake ni kutunisha mtaji wa Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF); kuendeleza miradi ya kielelezo ya Mchuchuma na Liganga kwa kulipia fidia, mradi wa magadi Soda Engaruka na Kiwanda cha Matairi Arusha.
Pia kuendelezaji wa eneo la Viwanda TAMCO Kibaha, mradi wa kuunganisha matrekta ya URSUS, uendelezaji wa Mitaa/maeneo ya viwanda vya SIDO; Kuendeleza Kanda Kuu za Uchumi (Ruvuma, Tanga, Kigoma na Manyoni).
“Pia kuendeleza mradi wa Bagamoyo SEZ & BMSEZ; Kurasini Logistic Centre and Kigamboni Industrial Park; Kuendeleza utafiti kwa ajili ya TIRDO, CAMARTEC na TEMDO; Dodoma Leather and Dodoma SEZ; na ujenzi wa maeneo maalumu ya viwanda,” amesema.
Amesema pamoja na vipaumbele hivyo, wizara itaweka msukumo wa pekee katika kuhamasisha ujenzi wa sekta binafsi ya Kitanzania iliyo imara ili iweze kushiriki na kuchangia ipasavyo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.