Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
VIONGOZI wa dini nchini wamehimizwa kuendelea kusimamia mmomonyoko wa maadili kwani bado ni tatizo hivyo kulipa nguvu kulinda vizazi kwani ni mustakabali wa kujenga Taifa.
Wito huo umetolewa leo Juni 8, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maji, Juma Aweso wakati akizindua uchimbaji wa visima 200 vya Mfuko wa Maendeleo ya Mufti(MDF) uliohudhuriwa na viongozi pamoja na masheikhe mbalimbali.
Amesema mipango alinayo mufti lazima washirikiane katika kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani.
“Kiongozi ni muhimu tusione muhimu wake kwa sasa siku akiondoka tuone umuhimu wake tumpe ushirikiano mufti japo kuna watu watakukatisha tamaa kazi imeanza hatutakuwa kikwazo katika mradi huu,”amesema Waziri Aweso.
Amesema rasilimali watu inaongeze hivyo wanahitaji kuongeza huduma na maji ni muhimu katik sekta mbalimbali nakwamba ni jukumu la kila mmoja kulinda na kutunza vyanzo vya maji kama mboni ya jicho.
Aidha, amesema jambo hilo linahitaji pesa na amewaomba wadau washirikiane kutekeleza mradi huo na kufanya vipindi mbalimbali kwenye luninga jinsi watanzania watanufaika na mradi huo.
Naye Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi Bin Ally amesema lengo la kuanzisha Mfuko huo ni kwa ajili ya kuhudumia jamii katika sekta ya afya, elimu, madini, uchumi na zinginezo.
Amesema mradi huo unalenga kuchimba visima vya maji shuleni, vyuoni, madrsa na vijijini ili waweze kutatua changamoto za maji.
“Wanatarajia kuchimba visima 200 katika Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Singida, Arusha, Kagera na mingine, visima vya awamu ya kwanza tunatarajia kukamilisha ndani ya mwaka mmoja ambapo gharama ya kisima kimoja ni Sh milioni 15,” amesema Mufti Zuberi.
Amesema wana mipango mingi katika sekta tofauti na watawatumia wataalamu mbalimbali kubuni miradi ndani ya Baraza.
Ameongeza kuwa maji ni muhimu sana kila unachoona vipo hai ni maji na yasipokuwepo ibada hakuna vitu vingi haviwezi kuendelea bila maji.
Aidha, Mufti Zuberi amesema mradi huo wa kuchimba visima wanashirikia na Kampuni ya Victoria ya Uchimba Visima na wana timu inayoratibu mambo ya mradi huo.