29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

VIONGOZI AFRIKA WAFUTENI MACHOZI WANANCHI WENU

Na THOMAS MONGI



“NI mambo yasiyofanana katika Bara la Afrika, ni Bara lililojaAliwa kuwa na watu wa kutosha na madini ya kila aina lakini ni bara lililo maskini zaidi duniani, ni Bara lenye ardhi kubwa yenye rutba inayotosha kulilisha Bara hilo lakini haliwezi kujilisha, ni Bara lililobarikiwa mito na maziwa makubwa lakini bado linasumbuliwa na ukame na kuna baadhi ya maeneo watu wake wanakufa kwa kiu na la kushangaza  ni kuwa Bara maskini kuliko  yote duniani lakini baadhi ya viongozi wake ni mabilionea “

Haya yalikuwa maneno ya Waziri wa Zamani wa Elimu nchini Malawi, Sam Mpasu, alipokuwa akitoa maoni yake katika Jarida la Development Policy Analysis , toleo la April 26, 2010.

Mpasu, ni mzaliwa wa Afrika na ni Mwafrika, ambaye ni mfano wa viongozi ambao waliuona ukweli na kuusema kwa jinsi alivyoliangalia Bara lake linavyoteketea kwa kuwa na viongozi wengi wasiojali maslahi ya watu wanaowaongoza. 

Viongozi hawa wanadhani nchi wanazoziongoza ni zao na wao ndio wenye haki zaidi ya kufaidika na rasilimali za Bara hili kuliko wananchi wao, taabu, mahangaiko, njaa, kiu majeraha na vifo vya wananchi wao wengi  viongozi wasiowajibika wa nchi nyingi za Afrika haziwagusi wala kuwastua. hawajui wala hawaoni kwanini kuna shida, taabu, kiu na njaa kwa raia zao na wao kuwa ni chanzo cha  baadhi ya vifo vya raia zao hao. 

Viongozi hawa tumewaona kama si kusikia wakijigamba kuwa wao wanapendwa na wananchi wao, wanajali matatizo ya watu wao, wanahangaika kila pembe ya dunia kusaka maendeleo ya raia na nchi zao kwa jumla.

Robert Mugabe wa Zimbabwe, Joseph Kabila wa Congo( DRC), Piere Nkurunzinza wa Burundi na Silver Kiir wa Sudan Kusini ni baadhi ya viongozi wasababishao madhara mazito kwa raia  maskini wa nchi zao lakini bado wanajigamba kupendwa na kuwa wao ni wafia nchi zao, kwa mfano; Robert Mugabe, tangu aingie madarakani miaka 27 sasa  nchi yake kwa sasa inakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi lakini anajigamba kuwa yeye anajali wananchi wake. Mwaka 2000, aliamua kuchukua mashamba ya wakulima wazungu na kisha kuyagawa kwa raia na hasa wanajeshi wa zamani wa nchi hiyo. Uamuzi huo ulisababisha wawekezaji wengi kuikimbia Zimbabwe na uchumi kushuka sana. Inasemekana kwa sasa Zimbabwe kati ya watu kumi (10) ni mmoja tu ana ajira. Hali hii ya Zimbabwe inadhihirisha jinsi gani kiongozi akiwa hajali au si mwenye kuwaangalia wananchi wake jinsi anavyoweza kuleta dhiki na taabu kwenye taifa lake.

Serikali sasa ipo kwenye mgongano na wananchi wake ambao wanayaona maisha kuwa magumu kila kukicha, inawanyamazisha kwa nguvu wananchi pale wanapodai haki zao.

Mugabe hajali wala hafikirii kutoa fursa ya demokrasia kwa kuacha kuongoza pamoja na kuonesha dhahiri kuwa  ameshindwa kuiongoza Zimbabwe. Amekuwa akivitisha vyombo vya habari, anazuia taasisi za kiraia kufanya kazi zake, anadhibiti Tume ya Uchaguzi, Bunge na mahakama nchini mwake.

Machozi ya  wananchi wa Zimbabwe, yatafutwa na nani? Mashaka na hofu ya kuishi katika nchi yao waliyoipigania kwa damu yatakwisha lini?   Sijui ni kwanini kiongozi huyu na wengine wenye utaratibu kandamizi wa kutawala hawaoni wala kusikia vilio vya wananchi wao, kwa mfano; Mchezaji nyota wa Kimataifa wa zamani wa Liberia, George Weah, akihojiwa na gazeti la New York Times alisema “ Ni vyema Umoja wa Mataifa ungeichukua Liberia na kuwa chini ya uangalizi wake na si kwa muda bali ni kwa maisha yote, ili kufanya Waliberia waweze kuamini katika demokrasia na waweze kuheshimu haki za binadamu.” George Weah, aliyasema maneno haya baada ya wapwa zake wa kike wawili kubakwa na kuuawa ncnini Liberia, kisha nyumba waliyokuwa wakiishi ambayo ni ya George Weah ilichomwa moto .

Haya ni maneno yaliyotoka kwa mwananchi  aliyekata tamaa na uongozi wa nchi yake, amechoshwa na vita na vurugu chanzo kikubwa kikiwa utawala usiofaa, kipindi hiki Liberia ilikuwa katika vurugu na mauaji ya kutisha chini ya aliyekuwa Rais Charles Taylor.

Waliberia waliishi maisha bora na mazuri sana ilikaribia kuitwa nchi iliyoendelea. Mwishoni mwa miaka ya themanini na mwanzoni mwa miaka ya tisini, nchi hii iliingia kwenye  vurugu na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha mauaji ya kutisha na kujikuta ikiangukia kwenye umaskini mkubwa hadi sasa.

Yaonekana viongozi hawa wamejisahau, vyeo vimewalevya, hawakumbuki tena kuwa hakuna marefu yasiyo na ncha, hawajiulizi Mobutu kilimtokea nini baada ya kuwatawala kikatili wananchi wa Zaire(Congo-DRC) na sasa yuko wapi? Nini kilimgharimu Charrles Taylor wa Liberia, aliyefanya wananchi wake kuchukia kuishi katika nchi yao waliyoipenda sana na wakumbuke kuwa Hussein Habre wa Chad, aliikimbia nchi yake baada ya wananchi kusema basi na kusimama kidete na kumkimbiza baada ya kuchoshwa na utawala wake uliojaa uonevu, mauaji na rushwa.

Viongozi hawa ni mifano ya viongozi waliokuwa wababe na makatili  mbele ya wanaowatawala, kwa kuwanyima   haki za msingi  kama huduma za afya, maji, elimu, haki ya kuchagua viongozi wawatakao na kutowatengenezea mazingira mazuri ya kujiajiri au kuajiriwa na hivyo kuwaingiza katika maisha yasiyofaa ambayo yamesababisha kuwa duni katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Rais Joseph Kabila wa Congo (DRC), aliteuliwa kuwa Rais 2001, akiwa na miaka 30 baada ya kifo cha Baba yake Laurent Kabila aliyuawa. Hadi sasa ameitawala kwa mihula miwili kipindi kinachokubalika kikatiba nchini Congo.  
 
Kabila amekataa kufanya uchaguzi nchini Congo, uliotakiwa kufanyika hapo Disemba 2016, lakini sasa amekubali kufanya uchaguzi huo hapo mwaka 2018 baada ya viongozi wa dini kuingilia kati huku yeye akiambiwa awe Rais kwa kipindi hiki cha mpito cha miaka miwili kabla ya uchaguzi nchini humo. Kwa tamaa ya madaraka  Kabila ameshindwa kuheshimu Katiba hivyo akataka kuibadilisha ili aendelee tena kwa muhula wa tatu. Kwa tamaa yake  hiyo  tayari  damu za Wacongo zilishamwagika kwa kiasi kikubwa kupinga hatua hii ya Kabila. 

Hali au uamuzi usiofaa ulio kinyume na demokrasia tulishuhudia kwa Piere Nkurunzinza, alimwaga damu za ndugu na jamaa zake na kubadilisha Katiba ya Burundi, kisha kuingia madarakani kwa nguvu za jeshi. 

Hizi ni tabia chafu za kikatili ambazo hazijali maslahi ya wengi ambazo wengi wa viongozi wa Afrika wanazo.

Aina hii ya viongozi imeifanya Afrika idumae katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii  sababu muda mwingi na fedha  nyingi za nchi huelekezwa kwenye ununuzi wa silaha ambazo fedha zake hutokana na kodi za wananchi maskini kisha silaha hizo hizo hutumika kuwaulia wananchi hao hao, jambo hili linasikitisha na kukatisha tamaa sana kwa wananchi ndani ya nchi kama hizi barani humo.

Vitendo vya viongozi hawa kutojali maslahi ya nchi na wananchi na badala yake kujilinda wao na makundi yanayowazunguka husababisha jamii kuparaganyika na kuchanganyikiwa kiasi ambacho huzaa makundi ya waasi ambayo nayo huzidisha hali kuwa mbaya na nchi kuwa katika majanga ya njaa kwa kuwa wananchi hushindwa kushiriki katika shughuli za kilimo au shughuli zingine zozote za uzalishaji mali na mwishowe hali kuangukia katika umaskini wa kutupwa.

Mfano Sudan ya Kusini, ambapo watu zaidi ya 300,000, inakisiwa wameuawa baada ya Rais Salva Kiir Mayardit na aliyekuwa Makamu wake wa Rais Riek Machar, kutofautiana na kila mmoja kuwa na kundi lake la kijeshi ambapo kwa sasa wapo kwenye mapigano makali.

Amani imepotea nchini Sudan ya Kusini, amani hiyo imepotezwa na watu wawili tu ambao ndiyo wasababishao vifo na njaa kwa wananchi wasio na hatia yoyote. Ulafi na tamaa pekee za Kiil na Machal ndizo zinazoliangamiza Taifa changa la Sudan Kusini, hii haikubaliki hata kidogo. Utaumia zaidi pale utakapowaona kinamama na watoto wanavyoteseka na kuhangaika ili kuokoa maisha yao ambayo hayana thamani mbele ya wanajeshi katili ambao ni raia wenzao wanaotumwa na viongozi wao hawa ili kutekeleza nia ya viongozi hao ili waingie au kulinda mamlaka waliyonayo.

Itaendelea wiki ijayo……

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles