TEHRAN, IRAN
UAMUZI wa Serikali ya Rais wa Marekani, Donald Trump wa kuziwekea vikwazo nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran umepandisha bei ya mafuta duniani.
Uamuzi huo unaohusu usambazaji wa mafuta ghafi umesababisha bei ya mafuta ipande kwa kiasi kikubwa tangu Oktoba mwaka jana.
Wataalamu wa sekta hiyo wamesema vikwazo hivyo vinaweza kusababisha kupungua kwa hadi mapipa milioni 1.2 ya mafuta katika soko la kimataifa.
Lakini idadi hiyo inaweza ikawa ndogo zaidi kulingana na jinsi nchi zitakavyoupokea uamuzi huo wa Marekani na kiasi cha mafuta ambacho Iran itaendelea kusafirisha.
Rais Trump alisema anataka kuvuruga mapato ya Iran yanayotokana na mauzo ya mafuta.
Anaamini fedha hizo zinatumiwa na Iran kufadhili shughuli ambazo ni haribifu katika Mashariki ya Kati na kwengineko.