Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa makampuni ya madini ya Pangea, North Mara, Bulyanhulu na Exploration Du Nord Ltee, Deogratias Mwanyika na mwenzake Alex Lugendo, Â jana walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Walisomewa  mashtaka 39 yakiwamo ya kula njama, kughushi, utakatishaji fedha,   dola za Marekani bilioni 374.2.
Vigogo hao pia wanadaiwa kukwepa kodi na kusababisha Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kupata hasara ya dola za Marekani bilioni 112.2.
Katika hati ya mashtaka,  ya kughushi yapo manane, kukwepa kodi manane na kutakatisha fedha   17.
Katika kesi hiyo, upande wa serikali uliwakilishwa na mawakili, Faraja Nchimbi, Jackline Nyantori na Shadrack Kimaro, wakati upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili Hudson Ndusyepo, Gasper Nyika, Frola Jacob na Alex Mushumbusi.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi, Calvin Mhina,Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi alidai  kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30, 2017,  washtakiwa hao kwa pamoja walitenda makosa hayo katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam, Kahama, Tarime, Biharamulo, Johannesburg Afrika ya Kusini, Toronto, Canada na Uingereza.
Wanadaiwa wakiwa na ufahamu walitoa msaada wa kula njama, kupanga mkakati na kutekeleza vitendo vya uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.
Washtakiwa hao kwa pamoja, wanadaiwa kughushi mkataba wa mkopo ulioonyesha kuwa Kampuni ya Madini ya Pangea imepata kibali cha kukopa dola za Marekani milioni 90  kutoka kwa Kampuni ya Kimataifa ya Barrick na Kampuni ya Madini ya Explorations Nord Ltee.
Vilevile wanadaiwa kutakatisha fedha kati ya Mei 16 na Desemba 31, 2008, baada ya kutoa taarifa za uongo kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Â waweze kukwepa kodi ya dola za Marekani milioni 9.3 huku Kampuni za Pangea na Explorations, zikijipatia kiasi hicho cha fedha kinyume na sheria.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kukwepa kulipa Kodi ya Mapato TRA, dola za Marekani 840,000, kushawishi Kampuni za Pangea na Explorations  ziweze kujipatia kiasi hicho cha fedha huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la ukwepaji wa kulipa kodi na kughushi katika kosa tangulizi.
Wanadaiwa kutakatisha fedha na kukwepa kulipa kodi ya TRA, Â dola za Marekani milioni 1.5 zilizotokana na gawio kutoka mgodi wa Tulawaka/PML/MDN.
Vilevile wanadaiwa kughushi nyaraka na kujipatia mkopo wa dola za Marekani milioni 6.7 kutoka Kampuni ya Barrick.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuishawishi Kampuni ya Pangea na Explorations kujipatia   dola Marekani 674,497 na kukwepa kulipa kodi ya kiasi hicho cha fedha kwa TRA.
Mwanyika na wenzake, wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo zilizoonyesha Kampuni ya Bulyanhulu imejipatia mkopo usio na faida wa dola za Marekani milioni 4.1 kutoka  Kampuni ya Barrick waweze kukwepa kodi ya TRA na kuzishawishi kampuni za Pangea na Expolorations  kufanya muamala wa kuhamisha fedha hizo zilizotokana na zao la uhalifu.
Pia wanadaiwa kutoa rushwa ya dola za Marekani milioni 7.1 kwa aliyekuwa Mkuu wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Shinyanga, Hussein Kashindye   kumshawishi asiweze kufanya uchunguzi kwenye Kampuni ya Bulyanhulu.
Wanadaiwa kughushi  kuonyesha Kampuni ya Pangea imesaini makubaliano ya mkataba ya kukubali mkopo  fedha hizo ziweze kutumiwa na Kampuni ya Madini ya Buzwagi.
Vilevile wanadaiwa kughushi nyaraka ilioonyesha Kampuni ya Pangea ilijipatia mkopo usio wa faida wa dola za Marekani milioni 59.8 kutoka Kampuni ya Barrick.
Katika shtaka la 28, 29, 30. kwa pamoja wanadaiwa kughushi nyaraka zilizoonyesha wamejipatia mkopo wa dola za Marekani bilioni 339.8.
Washtakiwa hao wanadaiwa kukwepa kodi dola za Marekani bilioni 101.9.
Pia wanadaiwa kughushi nyaraka iliionyesha Kampuni ya Bulyanhulu imejipatia mkopo usio na faida wa dola za Marekani bilioni 752.6 ili wasiweze kulipa kodi.
Wanadaiwa kukwepa kodi ya TRA ya dola za Marekani 225.7 wakati huo wanadaiwa kughushi nyaraka iliionyesha mgodi wa North Mara umepata mkopo wa dola za Marekani bilioni 374.2.
Shtaka la mwisho linalowakabili washtakiwa hao ni kukwepa kodi ya dola za marekani bilioni 112.
washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa VILE kesi inayowakabili ya utakatishaji FEDHA na uhujumu uchumi.
Nchimbi alieleza mahakama hiyo  upelelezi  haujakamilika na kuiomba   kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Ndusyepo aliiomba mahakama hiyo   kutoa amri kwa Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP)  waweze kubadili hati ya mashtaka kwa mshtakiwa wa kwanza, iliyoandikwa Deogratias Mwanyika badala ya Deodatus Mwanyika kwa madai kuwa familia yake itakapoenda kumtembelea mahabusu watashindwa kujua ni nani.
Hoja hiyo ilipingwa na Wakili Nchimbi kwa madai kuwa  suala la kubadili jina kwenye hati ya mashtaka halina msingi kwa madai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na isitoshe mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao hawapaswi kusema au kufanya lolote mpaka watakaposomewa maelezo ya awali.
Hakimu Mhina alisema   suala la kubadli jina katika hati ya mashtaka halina msingi na kwamba wanaweza kueleza jambo hilo wakati wa kusomewa maelezo ya awali na likabadilishwa.
Hakimu Mhina aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 31, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.