Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
SERIKALI imetangaza vigezo vipya vya utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambavyo vitazingatia vipaumbele vitano vya kitaifa vitakavyoendana na mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano ijayo.
Vigezo hivyo vilitangazwa juzi na Naibu Wazari wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa Dar es Salaam juzi.
Taarifa hiyo ya Mhandishi Manyanya ilieleza kuwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) itatoa kipaumbele kwa wakopaji watakaosoma mafunzo ambayo yatazalisha watalaamu wanaokidhi mahitaji ya kitaifa katika fani zilizochaguliwa.
“Vipaumbele vilivyowekwa ni pamoja na fani za sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta na gesi asilia, sayansi asilia na mabadiliko ya tabianchi na sayansi za ardhi, usanifu majengo na miundombinu,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya Mhandisi Manyanya.
Taarifa hiyo ilisomeka zaidi kuwa mbali na kuzingatia vipaumbele katika utoaji mikopo, pia HESLB itaangalia uhitaji wa waombaji hususani wenye mahitaji maalumu ambao ni walemavu, yatima pamoja na kuangalia ufaulu wa waombaji katika maeneo ya vipaumbele na umahiri
Mhandisi Manyanya alieleza katika taarifa yake kuwa mpaka sasa HESLB imeshakamilisha uchambuzi wa majina ya waombaji ambao wana sifa zilizoainishwa na majina ya wanufaika wapya yametangazwa juzi katika maeneo husika.
Kwamba utaratibu wa kutoa vigezo kwa wanufaika wa mikopo hufanyika kila mwaka, lengo likiwa kuendana na malengo na matarajio yaliyopo katika mipango na mikakati ya kitaifa kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa 2025.
“Vigezo hivyo vimetokana na uwepo wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17 -2020/21), Sera ya Elimu na Mafunzo (2014) na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuzingatia mipango mikakati na sera, pia mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka 2016/2017 katika mwaka wa masomo 2016/17.
“Kuanzia mwaka huu wa masomo, wanufaika wote wa mikopo (wapya na wanaoendelea na masomo) watakopeshwa kulingana na uwezo wao katika vipengele vyote vya mikopo,” ilisomeka taarifa za Mhandisi Manyanya.