29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Mbatia ahoji vyeti vya Magufuli

mbatia

AGATHA CHARLE Na FERDNANDA MBAMILA

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia vyeti vya kitaaluma vya Rais John Magufuli vifanyiwe uhakiki kama vinavyohakikiwa vya watumishi wengine wa umma.

Amesema mbali na vyeti vya Rais Magufuli, vyeti vingine vinavyopaswa kuhakikiwa ni vya Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Wabunge na waandishi wa habari.

Mbatia aliyasema hayo jana wakati wa Kikao Maalumu cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho kilichofanyika katika Hoteli ya Lamada, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, kabla ya Mbatia kuibuka na hoja hiyo, iliibuliwa kwanza kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forums ambao pamoja na mambo mengine mtoa hoja alihoji iwapo Dk. Magufuli alitimiza vigezo vyote vinavyotakiwa kabla ya kutunukiwa shahada ya uzamivu.

“Kuhakiki vyeti tuanzie kwa viongozi, tuanze na Rais, udaktari wake aliupataje? 2006-2009, hili litasaidia taifa. Tuteremke kwa Majaliwa (Waziri Mkuu) hadi chini. Tuanze kuhakiki vyeti vya Spika, wabunge ambao ndio wanatoa mawaziri. Sio mkuki kwa nguruwe.., tuangalie vyeti vyote hadi vya waandishi wa habari,” alisema Mbatia.

Alisema yeye ataanza kwa kuweka wazi vyeti vyake ikiwemo namna alivyopata Uhandisi wake.

Mbatia alisema elimu nchini haina maandalizi ya kutosha na kwamba mambo mengi hayana mpangilio mzuri ikiwa ni pamoja na kutoa kauli kuwa watoto wote wasome masomo ya Sayansi.

“Hili litaisaidia nchi kwa ujumla, tulitoka kwenye GPA, kaja huyu (Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako) katurudisha kwenye Divisheni utasema Tanzania watoto wake ni wa sampuli za maabara. Ndarichako anasema watoto wote wasome Sayansi maandalizi yako wapi? “Kinachotakiwa ni kuhakikisha maandalizi na tuione elimu ya Tanzania kwa miaka 50 ijayo,” alisema Mbatia.

Alisema ndani ya miaka 17 bila Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kumekuwa na vitu vya ajabu huku utu ukikosekana kutokana na watu kukosa elimu rasmi ya kujitambua.

“Leo hii kuna ulimbukeni kwamba ile elimu yako ndio unatanguliza majigambo, madaktari wengine wanakagua watu lakini tukiwakagua wao ni shida, elimu yako iwe kujitambua. Suala la mbwembwe za kusoma ziwepo lakini ziifanye dunia mahali pazuri pa kuishi. Nyerere aliliona hili mwaka 1961, leo ndio tunazungumzia elimu huyu alikuwa na maono makubwa.

“Mwenendo wa sasa wa serikali ni kama inatoka vitani kwa namna ya kujijenga upya, namna bora ya kukuza nchi ni kujielimisha na kutumia elimu kwa faida ya wengine, hatuna viongozi walioandaliwa, wakweli na wenye uwezo,” alisema Mbatia.

Mbatia alitoa sifa za kiongozi anayefaa kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo na astahili, mcha Mungu, mkweli wa maneno na matendo na achukie ufisadi na mapato ya dhuluma.

“Tunahitaji tuwe na chuo cha kuandaa viongozi sio mtu aseme alipenyapenya,” alisema Mbatia.

Akizungumzia hali ya siasa nchini, alisema NCCR – Mageuzi hakitakubali kufanya siasa kwa kuamriwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali kitaendelea kufanya mikutano ya hadhara kwa kuwa kipo kikatiba.

“Hakuna aliye juu, Nyerere alitawala akaiacha nchi, akaja mwingine, akaja Mkapa (Rais mstaafu wa awamu ya Tatu)..na Magufuli ataondoka nchi itabaki akitaka la kwake kwamba ni sheria hilo halipo,” alisema Mbatia.

Akizungumzia maafa ya tetemeko lililotokea mkoani Kagera, Mbatia alisema kulikuwa hakuna mamlaka ya uokoaji.

Alisema tathimini ya awali ambayo yeye na wenzake waliifanya walipokwenda mkoani humo walibaini kuwa gharama za awali ili kurudisha hali ya kawaida kwa wakazi zilipaswa kupatikana Shilingi Bilioni 100.

“Gharama ya Bilioni 100 tuliifanya kwa mjini pekee pasipo kuweka uharibifu wa Misenyi na Bukoba vijijini, ukitoa pole na vitu vingine tulibaini ni Shilingi Bilioni 300 na si Shilingi Bilioni 90 kama ilivyodaiwa na serikali,” alisema Mbatia.

Alisema iwapo serikali ina fedha zozote za maendeleo inapaswa kuzipeleka Kagera ili kuwasaidia wananchi ambao alidai wanaolala nje baada ya nyumba zao kuharibiwa na tetemeko.

Mbatia alisema hata kama ni fedha zilizotengwa kwa ajili ya jambo la maendeleo ziwasilishwe bungeni ili libadili matumizi kwa dharura na serikali ianzishe mamlaka ya kupambana na maafa nchini.

Pia Mbatia aliilaumu serikali kwa ilichelewa kutoa msaada wakati wa maafa hayo na kwamba vikosi mbalimbali vya majeshi hapa nchini vilipaswa kuwasili ndani ya saa nane baada ya tukio jambo alilodai halikufanyika.

Kikao hicho maalumu wa NCCR-Mageuzi kililenga kuchagua viongozi wakuu watatu kujaza nafasi ya Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Mweka Hazina wa Taifa pamoja na wajumbe wanane wa Halmashauri Kuu nafasi ambazo zilikuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles