NAIROBI, KENYA
MAELFU ya wagonjwa katika hospitali za umma wanahangaika bila matibabu baada ya mgomo wa nchi nzima wa madaktari na wahudumu wengine wa afya, huku karibu wagonjwa 100 wakiripotiwa kutoroka Hospitali Kuu ya Wagonjwa wa Akili ya Mathari jijini Nairobi.
Katika mgomo huu ulioanza wiki hii, madaktari wanaishinikiza Serikali kutekeleza makubaliano ya mwaka 2015 yaliyofikiwa na Muungano wa Wahudumu wa Afya ukiwa na lengo la kuboresha mazingira ya kazi.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, polisi walisema wamefanikiwa kuwarejesha baadhi ya wagonjwa wa akili hospitalini, ambao inaaminika walitoroka wakitumia fursa ya kutokuwapo kwa madaktari waliogoma.
Wagonjwa wengine katika hospitali za umma nchini hapa, wamelazimika kurudi nyumbani au kutafuta matibabu katika zahanati binafsi ambazo gharama zake ni kubwa.
Mwaka 2013, sekta ya afya nchini Kenya ilipeleka baadhi ya huduma zake chini ya mamlaka za kaunti, hatua iliyosababisha hospitali za umma kuwa chini ya usimamizi wa magavana.
Hata hivyo, Wizara ya Afya bado inasimamia hospitali kuu za kitaifa, ikiwamo ya Kenyatta iliyoko Nairobi na Moi iliyoko Magharibi mwa Kenya.
Tangu sekta ya afya kuwekwa chini ya usimamizi wa kaunti, huduma za afya zimeonekana kudorora, huku wauguzi na madaktari wakifanya migomo ya kila mara kulalamikia mazingira duni ya kazi.