23.6 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

Uzalishaji kiwanda cha sukari TPC ulivyomkuna Mchechu

Na Safina Sarwatt, Mtanzania Digital

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ameeleza kuridhishwa kwake na ufanisi wa kiwanda cha sukari cha TPC Limited, akibainisha faida kubwa iliyopatikana katika kipindi cha mwaka 2022/23.

Kiwanda hiki kimeweza kuzalisha faida ya Sh bilioni 72.7 baada ya kodi kutokana na mauzo ya Sh bilioni 235, huku gawio kwa wanahisa likifikia Sh bilioni 69.9. Hayo yalielezwa katika kikao cha wanahisa kilichofanyika hivi karibuni mkoani Kilimanjaro.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu (katikati) akiwa na uongozi wa kiwanda hicho alipokitembelea hivi karibuni.

Mchechu alieleza kuwa tangu mwaka 2000, kiwanda hiki kimekuwa kikiongeza uzalishaji mwaka hadi mwaka. Kwa sasa, uzalishaji wa sukari umeongezeka kutoka tani 36,000 mwaka 2000 hadi kufikia tani 116,700 kwa mwaka huu. Ongezeko hilo la uzalishaji wa sukari limetokana na mavuno ya miwa yaliyofikia tani 1,150,000 kwa mwaka huu.

“Katika uzalishaji wa sukari kwa mwaka huu, TPC Limited imezalisha zaidi ya tani 116,700 katika kipindi cha Juni 2022 hadi Machi 2023, kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kuzalishwa tangu TPC kuanza uzalishaji wake mwaka 1936,” alisema Mchechu.

Aliongeza kuwa serikali, wakati wa ubinafsishaji, iliweka malengo ya kuzalisha tani 750,000 za miwa kwa mwaka, lakini kwa sasa wanazalisha tani 1,150,000, kiwango kilichozidi malengo ya serikali. “Eneo lile lile lakini uzalishaji unazidi kuwa mkubwa kutokana na tija katika uzalishaji, ambapo mwaka huu TPC imeweza kutoa tija ya wastani wa tani 148 kwa hekta, kiwango cha juu barani Afrika na mojawapo ya viwango bora duniani,” alisisitiza Mchechu.

Pia alieleza kuwa TPC imeongoza kwa miaka mitatu mfululizo kwa kutoa gawio zuri na kubwa serikalini kuliko mashirika mengine yote ambayo serikali ina hisa kidogo. Katika hatua nyingine, Mchechu alitangaza ujenzi wa kiwanda kipya cha uchakataji wa molasses ili kuzalisha bidhaa nyingine kama spirit kwa ajili ya matumizi ya viwandani na watumiaji wengine. Ujenzi huo unatarajiwa kuanza mapema 2024 na kukamilika Julai 2025, ukiwa na uwekezaji wa zaidi ya Sh bilioni 100.

Uwekezaji huu utaongeza ajira na mapato ya ndani ya kiwanda, na kuwezesha kulipa kodi nyingi zaidi. Kiwanda hicho kitazalisha spriti itakayouzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Kwa sasa, TPC imeajiri wafanyakazi 4,000, kiwango kikubwa na chenye mishahara iliyoboreshwa pamoja na bonasi, huku wakiwaghariamia matibabu wafanyakazi na familia zao.

Mchechu alisema, “Uwekezaji huu ni wa mfano na ni aina ya uwekezaji ambao serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inahitaji. Tunaona fahari sana kuona ukuaji huu wa uwekezaji wa ndani ya kiwanda hiki cha TPC na manufaa yake kwa jamii inayozunguka.”

Pia alibainisha kuwa kutakuwa na ongezeko la uzalishaji wa nishati ya umeme ambapo kiwanda hicho kinatarajia kufunga mashine nyingine ya kuzalisha umeme na kutoa ziada ya megawati nne hadi saba ambazo zitaingizwa katika gridi ya Taifa.

Jafarry Ally, Mkuu wa Utawala wa TPC, alisema kiwanda hicho kimeweza kulipa kodi, ushuru, na gawio kwa serikali zaidi ya Sh bilioni 99, kiwango kikubwa ikilinganishwa na Sh bilioni 2 zilizokuwa zikitolewa wakati wa ubinafsishaji mwaka 2000. Hii inatokana na uzalishaji, mauzo mazuri, na ulipaji sahihi wa kodi kwa mujibu wa sheria na miongozo.

“Mwaka 2010 ndipo kiwanda kilianza kulipa gawio serikalini, na hadi mwaka 2022/2023 tumekuwa tukilipa gawio na kiwango kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka, kuifanya TPC kuongoza kwa miaka mitatu mfululizo kwa kutoa gawio zuri na kubwa serikalini kuliko mashirika mengine yote ambayo serikali ina hisa kidogo,” alisema Ally.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles