29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Utandawazi watajwa chanzo mmomonyoko wa maadili

Na Clara Matimo, Mwanza

Serikali imesema kitendo cha Watanzania   kupuuza mila na desturi naa kukumbatia tamaduni za kigeni ni moja ya sababu  inayochangia ongezeko la mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, kupitia hotuba  yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dk. Angeline Mabula, kwenye ufunguzi wa tamasha la utamaduni mila  na desturi zetu linalofanyika kwenye Uwanja wa Msalaba Mwekundu Kata ya Kisesa Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza.

Amesema  hali hiyo inachangiwa na kukuwa kwa matumizi ya teknolojia ambapo kundi kubwa hasa la vijana wamekuwa wakijihusisha nayo  kitendo kinachoongeza kasi ya kuenea kwa utamaduni wa kigeni na kufifisha utamaduni wa Taifa kwa kile wanachokiita utandawazi.

“Tusikubali mtu yeyote atuambie kuwa mila na desturi zetu hazifai, mila na desturi zetu ndiyo hasa chimbuko la maadili, utu, nidhamu, uwajibikaji na uzalendo wa taifa letu.

“Siku zote waswahili wanasema mkataa kwao ni mtumwa tusikubali Watanzania kuwa watumwa, amani tuliyonayo kama tusipokuwa na viongozi wetu wa kiutamaduni ambao wanatukumbusha mila na tamaduni zetu ni wazi taifa linaweza likapotoka.

“Rai yangu  kwa Watanzania leo tunapoenzi tamaduni , mila na desturi zetu niwaombe sana hasa machifu muendelee kushirikiana na serikali ili vijana wasikengeuke, bado mnaheshimika na mnakubalika katika jamii kwa kuendelea kuzilinda na kuzienzi mila zetu mfano lugha ya kiswahili ni utamaduni ambao unatukumbusha muasisi wa taifa hili, hayati Mwalimu Julius Nyerere,”amesema.

Hotuba hiyo imefafanua kwamba, ili kukabiliana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili, Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, imechukua hatua kadhaa ikiwamo  kuandaa kitabu cha  muongozo wa maadili ya utamaduni wa Mtanzania na  kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuandaa mitaala kwa ajili ya kufundisha somo la historia na utamaduni  wetu mashuleni.

“Kitabu hicho ni muhimu  sana kwa sababu kinatoa fursa kwa watakao kisoma   kitasaidia sana kuhamasisha jamii kutambua na kuthamini utamaduni wetu pia misingi ya maadili, kitaibua mjadala kuhusu taifa, msingi na maadili ya taifa hivyo nawaomba  kitapochapishwa na kuzinduliwa watanzania wote tujipatie nakala ili tusome maadili yetu,” amesema Dk. Mabula kwa niaba ya Bashungwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel,  amesema tamasha hilo ni zuri  kwa kuwa ni  utambulisho wa mila na desturi hivyo watahakikisha wanazilinda na kuzihifadhi  ili ziweze kuwa urithi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, amesema tamasha hilo ambalo linaikumbusha jamii mila za kichifu ni historia ya aina yake kwa sababu litasaidia kuifundisha jamii hasa vijana ambao ndiyo taifa la kesho jinsi ya kujenga maadili ya nchi yao.

Mwenyekiti wa Umoja wa Watemi  wa Usukuma, Itale Charles, amesema tamasha hilo limeandaliwa na  Umoja wa Machifu Tanzania lengo ni  kudumisha, kuendeleza, kufundisha  na kurithisha utamaduni wa nchi  kwa vizazi vya sasa ili viudumishe.

Tamasha hilo la siku mbili  linalofanyika katika uwanja wa historia ya kichifu(ngomeni) ambapo machifu hukutana na kufanya shughuli zao zaidi ya miaka 67 limekutanisha jumla ya machifu 94 kati ya 150 waliotarajiwa kuhudhuria  kutoka Tanzania Bara na Visiwani,  litahitimishwa kesho Septemba 8  na Rais Samia Suluhu Hassan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles