30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

UTAFUTAJI GESI HELIUM, SASA  KAMPUNI YAOMBA LESENI UZALISHAJI WAKE

 

Na JUSTIN DAMIAN


WAKATI gesi ya Helium ikigundulika kwa mara ya kwanza mwaka 2016 mkoani Rukwa, watafiti walikadiria kuwa ilikuwepo kiasi mita za ujazo bilioni 1.5 (54bcf).

Hata hivyo, utafiti mpya uliofanywa na Kampuni ya Helium One inayojishughulisha na utafutaji wa gesi hiyo kupitia wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza, unaonyesha kuwepo kwa mita za ujazo bilioni 2.8, (98.6bcf) karibu mara mbili ya kiasi kilichodhaniwa mwanzo.

Helium, ni moja kati ya gesi zenye thamani kubwa duniani, ikitumika kama mafuta ya roketi zinazokwenda anga za mbali pamoja na matumizi kwa vifaa tiba kama mashine za MRI zinazotumika kuchunguza maradhi yaliyo ndani ya mwili wa binadamu.

Wakati gesi hii ikiwa na thamani sana kwa matumizi mbalimbali, dunia inakabiliwa na upungufu wa gesi hii jadidifu (non-renewable) na uvumbuzi wa Tanzania umekuja wakati mwafaka kuziba pengo la wazi.

Kwa miongo kadhaa sasa chanzo kikuu cha gesi ya Helium kimekuwa ni hifadhi za chini ya ardhi zilizopo mji wa Texas nchini Marekani. Hata hivyo, uzalishaji unatarajia kukoma mwaka 2021 kwa kuwa hifadhi ya gesi hiyo itakuwa imekwisha.

Mzalishaji mwingine mkubwa ni nchi ya Qatar, lakini nchi hiyo imesimamisha uzalishaji kutokana na mgogoro wake na nchi ya Saudi Arabia jambo lililopelekea kufungwa kwa mpaka kati ya nchi hizo mbili. Hata hivyo, kiasi kilichopo Qatar ni kidogo sana ukilinganisha na kilichopo Tanzania.

Kupitia ugunduzi huu wa kihistoria, Tanzania inaingia katika ramani ya dunia kama moja ya mzalishaji mkubwa wa gesi hii adimu na yenye kuhitajika sana duniani.

Wiki iliyopita, Kampuni ya Helium One kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Jeolojia pamoja na Chuo Kikuu maarufu cha Oxford cha nchini Uingereza, waliandaa kongamano la siku moja kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali kuhusiana na gesi ya Helium.

Kongamano hilo lilihusisha wanasayansi magwiji wa masuala ya gesi kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, wataalamu kutoka idara ya geolojia UDSM, wafanya maamuzi, wadau wa maendeleo, watunga sera, watafiti na sekta binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Profesa Hudson Nkotagu, kutoa Idara ya Geolojia ya Chuo Kikuu Dar es Salaam, alisema ugunduzi wa gesi ya Helium unaifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa gesi hiyo duniani.

“Kama Tanzania tukijipanga vizuri na kuanza kuzalisha gesi hii kabla ya mwaka 2020 au kufikia mwaka 2020 yaani miaka miwili kuanzia hivi sasa, dunia nzima itakuwa inapata gesi  hii kutoka Tanzania. Itakuwa ni fursa muhimu kwa nchi yetu  kuendeleza azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda kwa kuwa Tanzania itakuwa ikizalisha Helium kwa ajili ya dunia nzima,” anasema

Profesa huyo anaongeza kuwa, uzalishaji wa gesi ya Helium utakwenda sambamba na uzalishaji gesi ya Nitrojeni ambayo inapatikana kwa wingi sana.

“Gesi ya Nitrojeni inapatikana kwa wingi sana kwenye sehemu ambapo Helium inapatikana.  Asilimia tisini ya gesi inayopatikana sehemu yenye Helium ni Nitrojeni. Gesi ya Nitrojeni inaweza kutumika kutengeneza mbolea na kwa vile Tanzania bado ni nchi ya kilimo tutaweza kupata viwanda vya kutengeznea mbolea,” anaongeza Prof Nkotagu

Mhadhiri huyo alisema Tanzania ina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa rasilimali alizoijalia ikiwamo gesi ya Helium huku akielezea kufurahishwa na Sheria mpya ya Madini na Gesi iliyofanyiwa marekebisho na ambayo itaisaidia nchi kuweza kupata zaidi kutokana na rasilimali zake.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya Helium One  Thomas Abraham-James alisema kampuni hiyo ina miradi mitatu ya utafutaji wa gesi ya Helium hapa Tanzania.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa mkoani Rukwa ambapo tayari ugunduzi wa 98.6bcf za helium umethibitika huku mahitaji ya gesi hiyo yakikadiriwa kufikia ni 6bcf kwa mwaka.

Miradi mingine alisema ni pamoja na maradi wa Ziwa Balangina lililopo mkoani Singida na mradi wa ziwa Eyasi lililopo mkoani Arusha. Kwa mujibu wa Mkurugenzi  huyo wa Helium One, miradi hii miwili ipo katika hatua za awali.

“Hadi kufikia hivi sasa tumeomba nakupewa Leseni za Utafutaji 23 huku maombi ya nyingine 3 yakiwa yanasubiri majibu kutoka kwa mamlaka husika. Leseni zote tulizonazo tunazimiliki kwa asilimia 100,” alisema.

Katika kongamono hilo, Helium One pia imetangaza ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wawili wa UDSM ambao watakwenda kusoma Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Oxford, ikiwa ni jitihada ya kuwajengea Watanzania uwezo wa kimataifa wa kisayansi juu ya masuala ya gesi pamoja na kuendeleza ushirikiano na UDSM.

Wanafunzi hao wawili waliopata udhamini, watafanya shahada zao za uzamili kuhusiana na gesi ya Helium na baada ya kumaliza wanatarajiwa kutumia ujuzi wao kufundisha kuhusu gesi ya Helium.

Kwa mujibu wa James, uelewa na ujuzi kuhusu gesi ya Helium duniani bado ni mdogo. Anasema, kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Oxford ujuzi na maarifa juu ya gesi ya Helium utakua na kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya kujifunza kuhusu gesi ya Helium duniani.

“Kampuni ya Helium One inaamini kuwa  kuna fursa ya kutengeneza vipaji vya wazawa vyenye hadhi ya kimataifa katika shughuli za utafutaji na maendeleo ya gesi ya Helium kwa hapa Tanzania. Tuatendelea kujenga ushirikiano wetu na UDSM kupitia kubadilishana ujuzi, mafunzo,” alisema.

Kwa uapnde wake, Clara Ole Kimani ambaye ni mmoja wa mwanafunzi waliopata udhamini huo alisema udhamini huo utamsaidia kuweza kujifunza zaidi kuhusu gesi hiyo adimu na pia kutumia ujuzi wake kuwafundisha wanafunzi wengine.

“Kwanza kabisa napenda kutoa shukrami kwa Kampuni ya Helium One kuweza kutoa udhamini huu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kunichagua mimi. Kama ambavyo imeelezwa ujuzi kuhusu gesi ya Helium bado ni mdogo na kwa hiyo ni fursa muhimu kwa sisi kwenda kujifunza na baadaye kuwafundisha wadogo zetu hapa chuoni,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles