KIGALI, RWANDA
WAKATI nchi ya Urusi ikiahidi kusaidia baadhi ya mataifa ya Afrika kujenga uwezo wake wa kutumia teknolojia ya nyukilia, msimamo huo umepingwa na viongozi wa upinzani nchini Rwanda .
Hayo yamejitokeza katika mkutano baina ya Urusi na wakuu wa mataifa 40 ya Afrika uliomalizika huko Sochi nchini Urusi.
Rwanda ni miongoni mwa mataifa yanayotarajiwa kunufaika kwa ushirikiano huu.
Hata hivyo, kumezuka sauti ya pingamizi kutoka ndani ya nchi hiyo.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Green nchini Rwanda, Frank Habineza amepinga mpango wa nchi yake kujenga kiwanda cha nyuklia kwa ushirikiano na Urusi akisema utakuwa na athari mbaya kwa wananchi.
Akizungumza na BBC, Habineza amesema wao hawakuunga mkono ushirikiano huo baina ya serikali ya Rwanda na Urusi kutokana na athari zake.
“Kulikuwa na mapatano ya Vienna kuhusu maswala ya nyuklia, na wakati huo huo Rwanda ilisaini mapatano mengine na Urusi kuanzisha kiwanda cha nyuklia hapa Rwanda. Mapatano ya Vienna yalikuwa kama kupalilia njia ya hayo ya Urusi kuanza kutekelezwa.”
“Bungeni sisi hatukupigia kura mswada huo kwa sababu tuliona kwamba bado ni mapema kwa nchi ya Rwanda kujiingiza katika kuidhinisha matumizi ya nishati ya nyuklia kwa sababu sehemu zote kulikojengwa nyuklia kumekuwa na athari mbaya kwa wananchi na kwa mataifa yenyewe” amefafanua.
Kiongozi huyo wa upinzani ametaja mfano wa nchi ya Ukraine ambako kiwanda cha nyuklia kililipuka na kuathiri nchi jirani ya Sweden.
Frank Habineza ni mbunge katika bunge la taifa, na chama chake cha Green kina uwakilishi wa viti viwili tu bungeni.
Muswada huo wa ujenzi wa nguvu za nyuklia ulipitishwa bungeni Rwanda isipokuwa pingamizi lilitolewa na wabunge wawili tu ambao hawakuunga mkono.
Mwaka jana Rwanda na shirika la nyuklia la Urusi la ROSATOM walitia saini makubaliano ya ujenzi wa nishati ya atomiki.
Rwanda inasema teknolojia ya nyuklia itaifaa kwa matumizi ya kutengeneza nishati, dawa na matumizi mengine ya amani.
Habineza ameeleza kwamba njia mbadala zipo.
“Bado Rwanda inaweza kupata nishati kutokana na mito iliyopo nchini au nishati ya miale ya jua, kumbuka pia kwamba Rwanda ina gesi ya kutosha”.
Kwa mujibu wa ripoti ya IAEA ya mwaka 2015, zaidi ya nchi 30 duniani, theluthi moja zikitoka Afrika zinajiandaa kuanzisha mipango ya nyuklia kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa usaidizi wa wataalamu kutoka Urusi.
Kampuni ya Urusi, Rosatom, imeshauriana na kuingia katika mikataba ya makubaliano na serikali kadhaa barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni katika kuidhinisha matumizi ya nishati ya nyuklia.
Mwaka jana kampuni hiyo ilitangaza kwamba imesaini makubaliano (MOU) na serikali ya Rwanda kupitia wizara yake ya miundo mbinu kushirikiana katika matumizi ya amani ya nishati ya atomiki.
Makubaliano hayo yaliidhinishwa kwa misingi ya ushirikiano wa pande mbili kujenga miundo mbinu ya nyuklia Rwanda na miradi mingine inayotokana na teknolojia ya nyuklia kama ilivyo kwa Uganda hivi sasa katika sekta zikiwemo za afya na hata ukulima.
Kenya, Afrika kusini na Nigeria ni miongoni mwa mataifa mengine ya Afrika yalio na ushirikiano na Urusi katika kuidhinisha miradi ya matumizi ya nishati ya nyuklia.