Morales ashinda muhula wa nne Bolivia

0
604
Rais wa Bolivia, Evo Morales akiwa amenyanyua mkono baada ya kujitangaza mshindi wa kiti cha urais katika mkutano na waandishi wa habari mjini La Paz

LA PAZ, BOLIVIA

RAIS wa Bolivia, Evo Morales ameshinda kwa awamu ya nne katika uchaguzi wa rais wa duru ya kwanza ulioandamwa na kiwingu cha madai ya wizi wa kura na ambao matokeo yake yanapingwa na upande wa upinzani.

Kulingana na matokeo rasmi yaliyotolewa baada ya asilimia 99 ya kura kuhesabiwa, Morales, mwanasiasa wa mrengo wa kushoto amepata asilimia 47.1 ya kura dhidi ya asilimia 36.5 ya mgombea wa siasa za wastani za mrengo wa kulia, Carlos Mesa.

Ushindi huo mwembamba umemwezesha Morales kuongoza kwa asilimia kumi kiwango kinachohitajika kuzuia kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi.

Morales tayari alijitabiria ushindi siku ya Jumatano na kurejea matamshi yake juzi saa chache kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo ya uchaguzi.

Wafuasi wa Morales walikusanyika kwenye kitongoji cha Cochabamba kushangilia ushindi wake wakipaza sauti na kusema “Udumu mchakato wa Mabadiliko, Udumu Evo Morales”

Bolivia imeshuhudia siku nne za maandamano ya umma dhidi ya madai kuwa serikali ilikuwa inafanya njama za kuiba kura.

Mgombea wa upinzani ambaye pia ni rais wa zamani wa nchi hiyo, Carlos Mesa,aliituhumu tume ya uchaguzi kufanya udanganyifu wakati iliposhindwa kuendelea kuchapisha matokeo ya uchaguzi yaliyoashiria uwezekano wa kufanyika kwa duru ya pili.

Tume ya uchaguzi ilitumia zaidi ya saa 24 kuhesabu sehemu ndogo ya kura  hatua iliyozusha maandamano ya umma yaliyodai kuna mipango ya kufanyika wizi wa kura ambapo ofisi za tume hiyo na zile za chama cha Morales zilishambuliwa.

Mesa amewataka wafuasi wake kuendelea na maandamano ya amani hadi pale duru ya pili ya uchaguzi itakapokubaliwa.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari mjini La Paz, Mesa alisema; “Kwanza, ni kushinikiza kuitishwa haraka kwa duru ya pili ya uchaguzi utakaosimamiwa kwa njia sahihi, huru na isiyoegemea upande wowote. Pili ni kuwatolea wito raia, mashirika ya kiraia na watu mashuhuri, kujiunga na mratibu wa ulinzi wa demokrasia na kuendelea kujikusanya kwa amani hadi pale matakwa ya watu walio wengi yatakapoheshimiwa”

Aidha wito wa kufanyika duru ya pili ulitolewa pia na jumuiya ya mataifa ya Bara Amerika ya OAS mnamo Jumatano wiki hii.

Umoja wa Ulaya umesema jana unakubaliana na tathmini ya OAS kuwa chaguo sahihi ni kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi ili kurejesha imani ya umma na kuhakikisha uamuzi wa kidemokrasia wa watu wa Bolivia unaheshimiwa.

Kadhalika kanisa katoliki nchini Bolivia na asasi 19 zisizo za kiserikali pia zimetaka kuwepo kwa duru ya pili.

Hata hivyo Rais Morales ameutaja msimamo huo wa upinzani kuwa jaribio la kufanya mapinduzi kwa msaada kutoka nje na kuagiza waangalizi wa uchaguzi kutoka jumuiya ya OAS wachunguzwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here