Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji, Dk. Suleiman Serera, ameeleza kuwa, Serikali inaitaji kuona Ushirika wa kisasa ambao unafuata mifumo ya kidigiti na kuzingatia taratibu na miongozo ya uendeshaji Ili kuwainua Wakulima.
Ameeleza kuwa, kukiwa na Ushirika wa kisasa wakulima watapata huduma kwa haraka mahala walipo ikiwa ni pamoja na kupokea malipo yao kwa wakati kutokana na uwepo wa taarifa za wakulima kwenye mifumo.
Ameeleza hayo Septemba 12, 2024 wakati wa ziara ya kikazi katika Mkoa wa Mtwara alipotembelea Kiwanda cha Kubangua Korosho cha TANECU kilichopo kijiji cha Mmovo, Wilayani Newala.
Vilevile amesema Serikali haitovumilia chama cha Ushirika kinachowanyonya wakulima kwani Ushirika umewekwa ili uwe daraja la kuwasaidia na kuwanyanyua wakulima ili kukuza uchumi wao.
“Hatujaweka Ushirika ili kuwanufaisha baadhi ya watu, endapo kiongozi yeyote umeingia kwenye Ushirika ili ujinufaishe mwenyewe achia ngazi mapema maana tukikubaini hautakuwa na mwisho mzuri kabisa,” Dk. Serera amesisitiza.
Aidha, ametoa rai kwa wanachama wa Vyama vya Ushirika kuacha kuchagua viongozi ambao hawawezi kuleta tija katika Ushirika na kuhakikisha viongozi wanaowachagua wanauwezo wa kuendesha Vyama vyao na kuviletea Maendeleo.
Kwa Upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dk. Benson Ndiege, ameeleza kuwa Vyama vinaenda kumaliza tatizo la ucheleweshaji wa malipo kwa mkulima atakayeuza mazao yake kupitia Vyama atapata malipo yake kwa wakati.