29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Usajili Yanga wazidi kutikisa

NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM

USAJILI mpya wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga umezidi kutikisa kutokana na jindi klabu hiyo inavyosajili kiufundi.

Baada ya kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji wa Mbeya City, Deus Kaseke ambaye anarithi mikoba ya Mrisho Ngassa aliyetimkia Afrika Kusini, klabu hiyo imeendelea na mipango mizito ya usajili wa wachezaji wengine wazawa na wale wa kimataifa ambao wanatarajiwa kutua nchini wiki hii kufanya majaribio.

Uongozi wa timu hiyo jana usiku ulitarajia kumpokea straika hatari wa FC Platinum ya Zimbabwe, Donald Ngoma, ambaye anatua nchini kukamilisha taratibu za kujiunga na timu hiyo.
Ngoma aliisumbua mno ngome ya ulinzi ya Yanga kwenye mchezo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu dhidi ya Platinum, ambayo ilishinda bao 1-0 lakini ikatolewa kwa jumla ya mabao 5-1.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, alisema wamejipanga kusajili wachezaji wenye hadhi ya kimataifa ili kuifanya timu hiyo kuandika rekodi bora kwenye michuano ya kimataifa mwakani.
Alisema usajili unaofanywa sasa umezingatia taratibu zote za kiufundi kwa maana ya wachezaji wote kuwa chaguo la Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans van Pluijm, hali itakayokifanya kikosi chao kuwa tishio msimu ujao wa Ligi Kuu.
Yanga inayotarajia kushiriki Ligi ya mabingwa Afrika mwakani, mbali na kumsajili Kaseke pia wamewabakiza nyota wake wa kulipwa kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na beki Mbuyu Twite huku pia ikimuongezea mkataba wa miaka miwili kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.
Alisema Yanga tayari wamenasa nyota wengine saba wa kulipwa ambao wanakamilisha idadi ya wachezaji 12 ambao watafanyiwa mchujo mara baada ya kutua nchini kwa Pluijm Juni 8, mwaka huu.
Muro alisema kama mapendekezo waliyowasilisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuomba kuongezwa kwa idadi ya wachezaji wa kulipwa ili kufikia nane yatakubaliwa, itafanya usajili wa historia kwa mara ya kwanza ambao haujawahi kufanyika.

Azam yaingia vita ya Chanongo

Wakati Yanga ikisuasua kwenye mbio za kunasa saini ya aliyekuwa winga wa Stand United, Haroun Chanongo, inaelezwa timu ya Azam inajipanga kuwapiga bao Wanajangwani hao.
Winga huyo aliliambia MTANZANIA jana mbali na Azam, klabu nyingine zilizowahi kufanya naye mazungumzo ni Stand United na Mwadui zote za Shinyanga.
“Sina haraka ya kusaini kwa kushirikiana na meneja wangu tutakubaliana na timu itakayotimiza mahitaji ninayohitaji, kama ni Azam, Yanga, Mwadui au Stand itajulikana,” alisema.
Akizungumzia dili la kujiunga na Yanga, Meneja wake, Jamal Kisongo, alisema bado hawajafikia makubaliano na Wanajangwani hao kutokana na baadhi ya mambo kutowekwa sawa, huku akidai timu itakayotimiza yale anayohitaji kwa manufaa ya mchezaji huyo ataikubalia iingie naye mkataba.
Kwa upande wa Yanga kuhusu winga huyo kutua Yanga, Muro alisema taratibu zitapokamilishwa litawekwa wazi, huku akidai wapo kwenye mchakato wa kumsajili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles