28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Ana kwa ana na Edward Lowassa

lowassaNa Khamis Mkotya, Dodoma

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana alikutana na wahariri wa vyombo mbali vya habari, ambapo alitumia fursa hiyo kujibu maswali na kutoa ufafanuzi juu ya mambo yanayosemwa dhidi yake.
Mazungumzo hayo ya kawaida yalifanyika nyumbani kwake, eneo la Area C, mjini hapa, siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza ratiba ya wagombea wa nafasi mbalimbali kuanza kuchukua fomu.
Katika mkutano huo, wahariri waliuliza maswali yaliyojikita katika nyanja mbalimbali, ikiwamo siasa, uchumi, elimu, michezo na mengine kuhusu afya yake. Yafuatayo ni maswali na majibu.
Swali: Mara nyingi nimekuwa nikisikia watu wanakuita Edward na wewe unawanyamazia tu, huoni ni kama vile hawakupi heshima?
Jibu: Edward ndiyo jina langu, that is my first name (hilo ndilo jina langu la kwanza), kwa hiyo mimi sioni tatizo kuitwa Edward.
Swali: Huko mtaani kuna maneno mengi sana yanasemwa juu yako, mengine ya kukuchafua na mengine ya ovyoovyo, kwanini umekaa kimya?
Jibu: Ni kweli yapo maneno mengi ya uongo na kupakaziana, wakati fulani niliwahi kuambiwa nimekusanya watu nimewaweka kwenye hema nimewaandalia chakula, uongo tu. Hata mazungumzo ya leo (jana), watu wamesema nimeita watu 3,000, wewe unavyoona hawa watu wanafika 3,000?
Hapa kwetu sasa kumekuwa na siasa mbaya, siasa za uhasama na kusingiziana, kwa hiyo kuepuka hayo niliamua kukaa kimya, wakati mwingine ukimya ni afya kwa mwanasiasa, leo nimeamua kuvunja ukimya.
Swali: Kwa kipindi cha miezi 12 wewe na wenzako mlikuwa ‘kifungoni’, juzi chama chako kilitangaza kuwa adhabu yenu imekwisha, yaani mmeachiwa huru, hebu tueleze nini sababu za kuingia katika kifungo hicho?
Jibu: Suala la kufungiwa na masuala mengine yanayohusiana na hayo nitalizungumzia kwa kina siku ya Jumamosi, Arusha nitakapokuwa natangaza nia, kwa hiyo sitajibu swali hilo.
Swali: Suala la afya yako limekuwa ni ajenda kubwa huko mtaani, leo tupo hapa hebu tueleze kama inavyosemwa ni tofauti?
Jibu: Hahaha (kicheko kidogo), hata nikikimbia km 100 watasema mgonjwa tu, siku moja nilikimbia na watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nilikimbia kilomita tano, kesho yake iliandikwa mahala nimelazwa Ujerumani.
Tunafanya siasa za kutakiana mabaya, jambo ambalo si zuri, afya ni suala la Mungu, niseme tu kwamba, mimi nipo fiti kwa lolote.
Mimi nashangaa suala hili linakuwaje ajenda? Nataka niseme wazi kuwa mimi pamoja na wenzangu wote wenye nia hii tukapime wote na mimi nitakuwa wa kwanza kupima ili tujue nani mgonjwa, tutakutana katika uwanja wa mapambano kwenye mchakato wa maendeleo.
Swali: Nataka kujua chanzo cha wewe kutoka serikalini ilikuwa nini, hivi ni kweli ulihusika katika sakata la Richmond au lilikuwa zengwe la kisiasa?
Jibu: Suala hili linaeleweka sana, mmeliandika sana, sioni sababu ya kulirudia. Tuelewe funzo moja katika hili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wakati ule, Hilary Clinton na Rais Barack Obama walipokuja hapa nchini walisifia ile mitambo wakasema ni mizuri.
“Kwa ubishi ule, imetugharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 120, nilipata taarifa kuwa mkataba ule tumeingia mkenge, kwa hiyo niliita wataalamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Hazina, wakati ule alikuwa Gray Mgonja, wakaangalia.
Wakasema mkataba uko sawasawa na mahakama ilithibitisha mkataba ule ulikuwa sawa sawa.
Huko nyuma mtakumbuka nikiwa waziri wa maji niliwahi kuvunja mkataba wa Kampuni ya City Water, iliyokuwa ikisambaza maji Dar es Salaam, walikwenda mahakamani tukawashinda na Serikali ilipata fedha nyingi.
Sikuweza kuvunja mkataba wa Richmond kwa sababu mamlaka ya kufanya hivyo hayakuwa ya kwangu yote, niishie hapo, sitaki kusema sana, yameandikwa mengi inatosha kujifunza, ajenda haikuwa Richmond, bali ajenda ilikuwa uwaziri mkuu ambao niliwaachia.
Swali: Umewahi kunukuliwa mara nyingi ukisisitiza kuhusu elimu kwanza, tofauti na kaulimbiu ya Serikali inayosema kilimo kwanza, huoni kama vile unapingana na mipango ya Serikali?
Jibu: Hili nitalizungumza Arusha, wakati fulani, Tonny Blair (Waziri Mkuu wa Uingereza) alipokuwa akigombea Uingereza, aliulizwa swali ni kitu gani anataka kufanya akipata madaraka, alijibu kwa kusema, elimu. Akaulizwa tena akajibu elimu, mara ya tatu akasema elimu.
Tukiwekeza katika elimu tutafika mbali kama taifa, nchi za wenzetu kama vile Indonesia, Malaysia na Singapore zimepiga hatua kwa sababu ya elimu. Ni ukweli elimu yetu imeparaganyika, kijana anahitimu chuo kikuu hajui kuandika hata sentensi ya moja ya Kiingereza, ipo shida.
Swali: Umekuwa ukilitazama tatizo la ukosefu wa ajira kama bomu linalosubiri kulipuka, pili, umekuwa ukiitwa majina mabaya, mara fisadi, mara mwizi, lakini sasa hali ni tofauti, naona kama vile nyota yako inang’aa, siri ya jambo hili ni nini?
Jibu: Hiyo ni neema ya Mungu, sina cha kusema zaidi ya hilo. Kuhusu tatizo la ajira ni kweli hili bomu lisipotafutiwa ufumbuzi, waziri mmoja aliwahi kunipinga na kusema kuwa ukosefu wa ajira si tatizo.
Narudia tena, tatizo la ukosefu wa ajira ni bomu, vijana wengi wanaohitimu vyuo hawana kazi, duniani kote kila mtu anayegombea urais anasema how many jobs he/she will create (atazalisha ajira ngapi).
Moja ya eneo ambalo tukilifanyia kazi vizuri litasaidia kuleta ajira ni gesi, siku moja niliwaita wataalamu nikasema tunaambiwa fedha za gesi tutaanza kuvuna 2020, hili likoje? Wakasema hapana, mnaweza kupata chini ya mwaka huu, itategemea vipaumbele vyenu.
Bodaboda ni eneo jingine ambalo linaweza kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, niseme kwamba ajira kwa vijana kwangu ndiyo kipaumbele, ukiniuliza mara ya pili na ya tatu hicho ndiyo kipaumbele changu.
Swali: Huko nyuma wewe na Rais Jakaya Kikwete mliitwa Boys II Men na wakati mwingine ulisema wewe na JK hamjakutana barabarani, hebu tueleze urafiki wenu ukoje?
Jibu: Urafiki wangu na Rais Kikwete umefanya nini, kwanini iwe ajenda? Yeye anafanya kazi zake na mimi naendelea na kazi zangu, acheni ajenda zisizokuwa na maana.
Swali: Ipo dhana kwamba wewe ni tajiri sana, umejilimbikizia mali na wengine wanasema hilo linaweza kuwa kikwazo katika safari yako ya matumani, nataka kujua chanzo cha utajiri wako.
Jibu: Hili limeandikwa sana kwamba nina mali nyingi, ukipita mtaani ukiona nyumba nzuri ya Lowassa, kifupi ni kwamba mimi nina nyumba chache tu, mifugo niliyonayo ni kati ya 800 na 1,000, lakini kwa eneo ninalotoka bila mifugo watu hawakuelewi.
Mimi nimekuwa Mbunge wa Monduli tangu mwaka 1995, masaini kiongozi anapewa ng’ombe ili watu watakapokuja kwako wawe na uhakika wa chakula, sioni kwanini watu wanatilia shaka mali zangu.
Kimsingi mimi natamani utajiri and I hate poverty (nachukia umasikini), natafuta uongozi wa nchi kusaidia Watanzania waondokane na umasikini, si kuukumbatia umasikini. Hii dhana kuwa kiongozi anapaswa kuwa masikini ndiyo aonekane mzalendo si sawa, umasikini si sifa ya uongozi.
Swali: Nini mtazamo wako kuhusu Serikali ijayo, unafikiri Serikali ya awamu ya tano inapaswa kujielekeza katika vipaumbele gani.
Pili, katika suala uchumi, unalitazamaje suala la dola kuzidi kupanda kila kukicha na shilingi inaporomoka. Tatu, unatoa hadhari gani kwa CCM katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Jibu: Maswali yako ni mazuri, lakini siwezi kuyajibu, vipaumbele na suala la dola nitayajibu Arusha. Hili la chama niseme kwamba, upinzani umeanza kupata nguvu mijini na vijijini.
Wito wangu ni kwamba CCM isibweteke, tusibweteke na mafanikio yaliyopo. Mifano ipo wazi, vyama vingi vilivyoshiriki ukombozi wa nchi zao vimeanguka na vikianguka havirudi tena madarakani, kikubwa tusibweteke.
Swali: Katika mchakato huu wa urais iwapo utashindwa kufanikiwa kuteuliwa kwa sababu yoyote ile, plan B yako ni ipi? (kuhama chama).
Jibu: Mimi ni mwanachama wa CCM, tangu mwaka 1975 nimekuwa mwanachama wa CCM, sijawahi kufanya kazi na chama tofauti zaidi ya Chama Cha Mapinduzi. My life (maisha yangu) ni CCM, huyu mbaya asiyenitaka CCM yeye ndiye ahame.
Swali: Ipo dhana kuwa, wewe ni mtu wa visasi na inasemwa kuwa ukiingia madarakani utalipiza visasi kwa wabaya wako, unazungumziaje suala hili?
Jibu: Hao wabaya wangu ni akina nani? Mimi nina imani ya dini, Yesu anasema samehe saba mara sabini. Siamini katika kufukua makaburi na wala sina kisasi na mtu yeyote.
Swali: Mtandao ulionao hauna tofauti na ule uliotumika kumwingiza Rais Kikwete madarakani, Serikali ya awamu ya tano itakuwa na tofauti gani na hii ya awamu ya nne?
Kwa mfano unasema marafiki zako ndio wanaokuchangia kufanikisha harambee, watu wanajiuliza ukifanikiwa urais hawa marafiki zako utawaweka wapi? Kama hawa akina Karamagi.
Swali jingine ni kwamba, kuna maneno yanasemwa kwamba Mwalimu Nyerere aliwahi kukukataa, unazungumziaje hili?
Jibu: Jamani Karamagi ana ubaya gani? Tusiwazushie watu tuhuma za bure bila sababu yoyote. Hili la Mwalimu, sijawahi kukataliwa na Mwalimu Nyerere, huo ni uzushi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles