22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara ya Kazi yanyimwa fedha za maendeleo

daftariNa Arodia Peter, Dodoma
WIZARA ya Kazi na Ajira haikutekelezea mradi wowote wa maendeleo kwa mwaka wa 2014/2015 kutokana na Hazina kutokuipatia fedha zilizotengwa kwa ajili hiyo.
Hayo yalibainika jana wakati wa kuwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa mwaka 2015/2016 mjini Dodoma jana.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Mwenyekiti wake, Dk. Maua Daftari, alisema mwaka jana wizara hiyo ilitengewa Sh bilioni 17.6, kati yake Sh bilioni 2.9 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, hadi kufikia mwaka mpya wa fedha 2015/2016, hakuna fedha yoyote iliyokuwa imetolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Kwa mantiki hii, inaonyesha kwamba hakuna kazi yoyote ya mendeleo iliyofanywa na wizara hii… mheshimiwa mwenyekiti kukosekana kabisa bajeti ya maendeleo inamaanisha kwamba wizara hii haina jipya katika kuendeleza nchi hii.
“Kamati inapenda kueleza wasiwasi wake juu ya kutokuwapo kwa nia ya dhati ya serikali kwa kutotenga fedha za kutosha au kuinyima fedha za miradi ya maendeleo na kuifanya isimame pale ilipo na kutosonga mbele hata kwa hatua moja,” alisema Dk. Maua.
Kamati hiyo pia ilikumbusha ahadi ya serikali kupitia hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mei 2015 kuhusu umuhimu wa wazee na mchango wao katika taifa.
Dk. Maua alisema mwaka jana kamati yake iliishauri serikali ikamilishe mchakato wa kuanzishwa pensheni ya wazee waweze kuboresha hali zao za maisha. Alisema utekelezaji wa suala hilo bado unasuasua na kuonekana kuwa mgumu.
Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya wazee nchini Tanzania kwa sasa imefikia milioni tano kati ya wastani wa watu milioni 49. Hii ni sawa na asilimia 11 ya idadi ya watu wote nchini.
Katika hotuba yake ya bajeti, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alizungumzia shughuli mbalimbali zilizotekelezwa na wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Alisema wizara yake ilihamasisha wafanyakazi na waajiri kujadiliana kwa pamoja kuhusu kuboresha maslahi ya wafanyakazi ambako katika kipindi hicho, mikataba ya hali bora 67 ilisainiwa na kusajiliwa na Kamishna wa Kazi.
Kabaka alizungumzia suala la ajira za wageni akisema wizara imeratibu utungaji wa sheria ya ajira za wageni kwa lengo la kuimarisha na kuongeza ufanisi katika kutoa vibali kwa kuzingatia ujuzi adimu nchini. Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh bilioni 38.8.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles