SOCHI, URUSI
SERIKALI ya Urusi imesema itafanya kila liwezekanalo ili kulinda masilahi ya kisheria ya seneta wake, Suleiman Kerimov, ambaye anashikiliwa nchini Ufaransa.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, aliwaambia wanahabari mjini hapa jana kuwa seneta huyo kama walivyo raia wengine wa nchi hii, Serikali ina dhamana ya kuhakikisha inamlinda kisheria.
“Kwa jinsi hali ilivyo na kiukweli, Kerimov ni raia wa Urusi kama walivyo raia wengine, hivyo tuna dhamana ya kufanya jitihada ili kulinda masilahi yake kisheria,” alisema Peskov.
Alisema miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Serikali ni kwamba tayari mjumbe ameshatumwa nchini Ufaransa ili kushughulikia suala hili.
“Ni muhimu kuona Suleiman Kerimov ndiye mmiliki wa pasipoti ya kidiplomasia, ambayo aliingia nayo Ufaransa. Ndiyo sababu tunafanya kazi kubwa ya kulinda masilahi yake,” aliongeza msemaji huyo.
Seneta Kerimov ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu la Seneta nchini hapa, alikamatwa mwanzoni mwa wiki akiwa uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Nice kisha akapelekwa kituo cha polisi.
Shirika la Habari la Reuters, liliripoti mapema juzi kuwa waendesha mashtaka wa Ufaransa wanamshikilia seneta huyo kwa kosa la kukwepa kulipa kodi.