21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘MTAALA WETU HAUTUWEZESHI KUWA NA TANZANIA YA VIWANDA’

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM


MFUMO wa elimu nchini kwa muda mrefu umekuwa ukilalamikiwa kwamba umeshindwa kusaidia kuzalisha wahitimu wenye ujuzi. Hii ni kutokana na mitaala ya kuwa ni ya kinadharia zaidi ya vitendo.

Mabadiliko kadhaa katika mitaala yamekuwa yakifanyika ili kuhakikisha inawezesha kutolewa kwa elimu bora, inayomjengea mwanafunzi ujuzi, lakini bado kumekuwa na ufundishaji na ujifunzaji usioendana na matakwa ya mtaala husika.

Wakati huu, ambapo Serikali inafanya jitihada za kukuza uchumi kuwa wa kati, unaotegemea maendeleo ya viwanda kumekuwapo mjadala mingi kuhusu upatikanaji wa wataalamu watakaosaidia kuendesha viwanda hivyo.

Kutokana na changamoto lukuki zinazoelezwa kuikabili sekta ya elimu na kuzingatia umuhimu wa elimu bora katika maendeleo ya shughuli za viwanda, Taasisi isiyo ya kiserikali ya Haki Elimu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwanzoni mwa wiki hii waliandaa mdahalo uliobebwa na jina la ‘Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda; kufikiria upya sera ya elimu ya kujitegemea.’

Akiwasilisha mada katika mdahalo huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, anasema miongoni mwa mambo yanayochangia kuzorota kwa elimu nchini ni usimamizi na uendeshaji wa elimu nchini.

Pamoja na Serikali kufanya ugatuzi wa majukumu katika sekta ya elimu na mafunzo kutoka Serikali kuu kwenda mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha ufanisi, bado kumekuwapo changamoto ya mwingiliano wa baadhi ya majukumu katika utekelezaji kwa upande wa utendaji na usimamizi wa elimu kati ya pande hizo mbili.

Kuhusu hali ya ufundishaji, anasema licha ya kuwapo kwa mabadiliko mbalimbali ya mitaala, kuna changamoto katika utekelezaji wa miongozo iliyopo kwenye mitaala hiyo ambazo zimekuwa zikiathiri ubora na usawa katika elimu inayotolewa kwa ngazi mbalimbali.

Anasema elimu itolewayo katika ngazi yoyote inaongozwa na mtaala. Katika muktadha huu, mtaala ni mwongozo mpana unaoweka viwango vya utoaji elimu kwa kuzingatia vipengele vya ujuzi watakaoujenga wanafunzi, maarifa, stadi, mwelekeo, njia za kufundishia na kujifunzia zitakazotumika katika utekelezaji wa mtaala.

“Vingine ni vifaa na kujifunzia upimaji, ufuatiliaji na tathmini ya mtaala husika, sifa za kitaaluma na kitaalamu za mwalimu atakayeuwezesha mtaala husika, miundombinu wezeshi kwa utekelezaji wa mtaala wenye ufanisi na muda utakaotumika kufundishia au utekelezaji mtaala.

“Mitaala mara nyingi hubadilishwa au kuboreshwa ili elimu inayotolewa iendane na mahitaji ya jamii husika kwa wakati huo. Mtaala unaotumika sasa wa mwaka 2005, unahitaji ufundishaji unaozingatia ujuzi kwa mwanafunzi kuwa mlengwa na mshiriki mkuu kwenye ufundishaji na ujifunzaji.

“Tafiti zinaonesha kuwa bado hali ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni katika ngazi zote unaendelea kwa kiasi kikubwa kuzingatia mwalimu anachukuliwa kuwa ndiye chanzo kikuu cha maarifa,” anasema Profesa Mukandala.

Katika mdahalo huo wasomi, wadau na viongozi mbalimbali wa Serikali nchini wanakubaliana kuwa ili Tanzania kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda, ni lazima kuhakikisha kunakuwapo utolewaji wa elimu inayowawezesha wahitimu kujitegemea.

Wanaamini kuwa Tanzania haiwezi kufikia azma yake hiyo kama haitawezesha wananchi kupata elimu itakayowawezesha kujitegemea na kuendana na mahitaji ya soko la ajira duniani.

Profesa Mukandala anasema licha ya mtaala huo kusisitiza ujuzi na kutoa fursa kulingana na uwezo, vipaji na vipawa bado umetawaliwa na muundo wa kuchuja wahitimu ili kupata wahitimu wachache wenye uwezo kitaaluma watakaoendelea ngazi za juu.

Anasema mchujo huo umekuwa ukitumika kama kipimo cha ubora wa elimu badala ya kutumia ujuzi na umahiri anaoupata baada ya kuhitimu.

Kwa maneno mengine, kipimo cha ubora wa elimu na mafanikio hutokana na ufaulu wa wanafunzi na si umahiri au ujuzi anaoupata mwanafunzi baada ya kuhitimu. Ndiyo maana watu wengi wanapozungumzia kushuka kwa ubora wa elimu nchini wanaanza kwa kutaja takwimu za ufaulu na si wahitimu wangapi wamekosa kupata ujuzi unaostahiki.

“Dhana hii inapingana na ile ya elimu ya kujitegemea, ambayo inashabihiana na mtaala huu wa sasa inayomuhitaji mhitimu kuwa mahiri katika ngazi yoyote anayomaliza hatimaye kujiajiri.

“Maarifa na ujuzi wa wanafunzi katika ngazi walizopo ni mdogo ikilinganishwa na ngazi ya elimu waliyofikia, ujuzi wa wahitimu wa mafunzo ya ufundi na elimu ya juu nchini, umebainika kutokidhi mahitaji wa ulimwengu wa kazi,” anasema Profesa huyo.

 

UTAFITI WA WB

Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) mwaka 2013 – 2014 katika kampuni 723 za sekta rasmi na isiyo rasmi nchini, ulibaini wafanyakazi wasio na ujuzi wa kutosha ni kikwazo kikubwa cha maendeleo na ufanisi wa kampuni.

Asilimia 40 ya kampuni zilizoshiriki utafiti huo zilibainisha kuwa idadi kubwa ya kampuni zinasumbuliwa na changamoto ya uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi, asilimia 63 ya kampuni ziliripoti kuwa uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi sahihi ni sababu kubwa ya kampuni hizo kushindwa.

Pia utafiti huo ulibainisha kuwapo kwa pengo la ujuzi ambalo ni kubwa kuliko wastani wan chi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

 

UALIMU KIMBILIO

Profesa Mkandala anasema pamoja ya kuwa ubora wa walimu ni chachu ya kuboresha namna ya kujifunza na kuleta mafanikio katika elimu, kumekuwapo changamoto kubwa hasa katika suala la sifa za kujiunga na ualimu, sifa ya wakufunzi wanaofundisha walimu wa vyuo vya walimu na ubora wa mafunzo ya ualimu.

Anasema wanafunzi wengi wanaojiunga na mafunzo ya ualimu nchini hukosa sifa stahiki za kielimu ikilinganishwa na matakwa ya kisera ya nchi.

Kikanunui kiwango cha chini cha kujiunga na programu ya Stashahada ya Ualimu ni angalau ufaulu wa msingi (Principle Passes) mbili ya kidato cha sita, lakini tafiti zinaonesha kuwa hata wenye msingi mmoja hujiunga na program hiyo.

“Fani ya ualimu imekuwa kimbilio au chaguo la mwisho kwa wanafunzi wengi wanaohitaji nafasi za kazi, wengi wa wanafunzi hawa hukimbilia ualimu baada ya kukosa nafasi katika fani nyingine wanazozipenda aidha kwa sababu ya mazingira mazuri ya kazi au mshahara mnono,” anasema Profesa Mukandala.

Sifa za wakufunzi wanaofundisha vyuo vya ualimu na ubora wa mafunzo ya ualimu ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika mdahalo huo, ambapo inaelezwa kuwa mafunzo ya ualimu yanayotolewa katika vyuo vingi nchini hayaendani na mahitaji ya mtaala uliopo na falsafa ya elimu ya kujitegemea kutokana na ufundishaji kutegemea nadharaia kuliko vitendo.

Profesa Mukandala anasisitiza ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi, ni lazima tuwe na Taifa la lenye watu walioelimika na watakaoweza kuchangia katika pato la Taifa kuleta maendeleo kama Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Mpango wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano dira na dhima ya elimu ya mafunzo ya nchi inavyoelekeza.

“Ualimu ni miongoni mwa taaluma kongwe na za kihistoria duniani. Pamoja na sifa hii, bado hadhi ya taaluma hii imeendelea kutopewa kipaumbele ikilinganishwa na taaluma nyingine kama uhasibu, uhandisi, udaktari na sheria,” anasema.

Mambo mengine yanayotajwa kutakiwa kuimarishwa ili kufikia Tanzania ya viwanda ni usimamizi wa mifumo ya uongozi wa uendeshaji elimu, kutoa ufadhili wa elimu, kuweka mkazo katika mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vikuu vya ufundi pamoja na kufanya tafiti katika maendeleo ya kiuchumi, kiteknolojia na elimu.

 

KUUNDA MAMLAKA YA KUSIMAMIA ELIMU

Katika mdahalo huo, wadau wa elimu walipendekeza kuundwa kwa mamlaka ya kusimamia sekta ya elimu ili kuwezesha elimu inayotolewa kuendana na uchumi wa viwanda.

Mkurugenzi wa Shirika la HakiElimu, John Kalage anasema mamlaka itakayosimamia elimu itawezesha kusaidia mabadiliko yanayofanywa na watunga sera.

Kalage anasema mamlaka itakayoundwa kusimamia elimu, itawezesha kusaidia mabadiliko yanayofanywa na watunga sera kufanyiwa upembuzi kabla ya kuingizwa katika mfumo rasmi wa utekelezaji.

“Kuna baadhi ya mambo tunajadili leo, lakini si mapya. Kuna wakati waziri anakuja na kubadili mfumo bila kufanya tafakuri na uchambuzi wa kina, hii huathiri mamilioni ya Watanzania. Kwa hiyo tukiwa na mamlaka ya kusimamia elimu, itatuwezesha kutoa elimu iliyo bora.

“Tutakapokuwa na chombo hicho, kitaweza kusaidia kufanya upembuzi kwa kina na kubaini tumefikaje hapa tulipo na tunatokaje,” anasema Kalage.

Kalage anaamini umefika wakati wa kuwa na sera inayowaandaa wahitimu kujitegemea na kama ipo, iangaliwe kama inaendana na matakwa ya sasa ya Taifa.

“Elimu ya kujitegemea lazima iendane na mfumo wa siasa na uchumi wa nchi, mfumo wetu bado una changamoto tunazopaswa kuzibadili ili uwe na tija, tunaweza kuwa na viwanda lakini tunaandaa rasilimali watu ili kuviendesha.

Jaji na Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mdahalo huo, anasema mapendekezo yaliyotolewa na wachangiaji ikiwamo kupitiwa mfumo wa elimu, yatakuwa na tija kwa kuwa yatawezesha kubaini changamoto zilizopo na jinsi ya kuzitatua.

“Tunapaswa kutoa elimu iliyo bora na kuwa na mwelekeo wa aina ya elimu tunayoitoa. Naamini, Serikali itatusaidia kuyatumia mapendekezo na kuyaingiza katika sera na kanuni na kuona itaboreshaje elimu,” anasema Jaji Warioba.

Jaji Warioba anasema mfumo wa elimu nchini umekuwa na matatizo makubwa kwani wanafunzi wanaomaliza darasa la saba hawafahamu kusoma na kuandika, ikilinganishwa na hapo awali ambapo mwanafunzi aliyehitimu darasa la nne aliweza kufanya hivyo.

Naye Dk. Joviter Katabaro anasema kama nchi inataka kutoa elimu, basi ianzishe vyuo vya ufundi katika kila wilaya ambavyo vitawafundisha vijana kwa vitendo na kuwapo shule ya mfano ya sayansi kwa kila wilaya ili kufanikisha sera ya uchumi wa viwanda.

“Tanzania ya viwanda inahitaji watu wenye ujuzi na mbinu kuanzia ngazi ya chini, na vyuo hivi vya ufundi ni muhimu,” anasema Dk. Katabaro.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage anaamini kuwa wanafunzi wa Kitanzania wamekuwa na uwezo mkubwa wa kushika vitu wanavyofundishwa, hivyo ikiwa itatolewa elimu inayowawezesha kujitegemea watasadia kufikia uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo anasema ili kujikomboa kiuchumi, kisiasa na kiitikadi ni lazima kuangalia aina ya maudhui na mifumo ya ufundishaji ambayo yataunda mfumo wa elimu utakaoweza kulifikisha Taifa katika azma ya uchumi wa viwanda.

“Tunahakikisha vipi kwamba mfumo wetu wa elimu unazaa watu wenye vipaji vya ubunifu wa hali ya juu, ujuzi wa kutosheleza na kuwa na watu waliokombolewa kifikra ili nchi iondokane na dhoruba ya utegemezi wa muda mrefu?” anahoji Jafo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles