25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

WASIOONA WATENGENEZEWA MACHO BANDIA YENYE UONI HALISI

Na MWANDISHI WETU


WAKATI zaidi ya watu milioni 40 duniani wakiathirika na maradhi ya macho yaliyosababisha kupata upofu na wengine milioni 124 wakiathiriwa na tatizo la uoni hafifu, wanasayansi wanaelekea kupata suluhisho la kudumu la matatizo haya.

Aina mpya ya jicho la bandia ambalo linaweza kumfanya binadamu asiyeona kuona tena linaloitwa kama bionic eye limegunduliwa.

Wanasayansi wanaotengeneza Bionic eye wanatumia teknolojia ya kisasa kutengeneza jicho bandia litakalowawezesha wasioona kuona tena kwa kupandikizwa jicho hilo. Teknolojia hii inafanana kwa mbali na ile inayoweza kuwafanya wasiosikia kusikia.

Majaribio kadhaa ya macho hayo ya bandia yanafanyika kwa sasa na moja ya jaribio lililofanyika nchini Marekani limeonesha mafanikio makubwa. Jicho hilo limeweza kuwekewa mtu na kuona lakini ni kwa wagonjwa wanaopata upofu kutokana na aina maalumu ya ugonjwa unaosababisha tatizo hilo.

Teknolojia ya bionic eye ambayo pia huitwa glass eye inafanya kazi baada ya jicho la kawaida lenye matatizo kuondolewa na kuwekwa la bandia. Jicho hili ni tofauti na yale ambayo huwekewa watu ili kuonekana kama wana macho lakini ki uhalisia ni kama urembo tu.

Kama ambavyo hakuna chanzo kimoja cha upofu, pia hakuna tiba moja ya upofu. Ili kujua kama bionic eye inaweza kukusaidia kuona tena, ni muhimu kujua tatizo lililokusababishia kutoona.

Nchini Marekani, Mamlaka ya Chakula na Dawa imepitisha na kuidhinisha aina moja biotic eye inayoitwa Argus II Retina Prosthesis System, ambayo imetengenezwa na Kampuni ya Second Sight ya nchini California.

Argus II imetumika kusaidia kutengeneza uoni kwa mamia ya watu ambao huathiriwa na ugonjwa wa retinitis pigmentosa inayokadiriwa kuathiri zaidi ya watu 5,000 nchini humo.

Argus II pia imesaidia watu wenye umri mkubwa wenye matatizo ya kuona.

Argus II ina sehemu mbili, ambayo ni pamoja na kamera inayomsaidia mtu kuona na kifaa kingine ambacho huwekwa kwa nyuma ya jicho.

Kile ambacho kamera inakiona, hubadilishwa kuwa taarifa ambayo husafirishwa pasipo kutumia waya kwenda kwenye sehemu ya jicho ya retina. Baada ya hapo, kitu kama laini huziamsha seli za retina ambazo hupokea taarifa na kuzipeleka katika mishipa inayoitwa optic nerve ili ziweze kutafsiriwa na ubongo.

Japokuwa Argus II inamwezesha anayeitumia kutofautisha mwanga, mwendo na maumbo, bado haijakuwa na uwezo wa kurudisha hali ya uoni kama ambavyo jicho la kawaida linaweza kuona.

Hii ni kwa sababu, ili kuweza kuona kikamilifu mtu anahitaji kuwa na mamilioni ya electrode wakati teknalojia hiyo inawezesha kurudisha  electrode 60 tu

Hata hivyo, watumiaji wa Argus II wanaweza kusoma maandishi makubwa na kukatiza katika mitaa mbalimbali bila shida na pasipo msaada wowote. Kampuni inayotengeneza Argus II imesema itaongeza idadi ya electrodes ili kuongeza ufanisi zaidi kwa ajili ya watumiaji wake katika matoleo yake yajayo.

Udhaifu mwingine wa Argus II haiwezi kumfanya mtumiaji kutambua rangi ya vitu, pia huuzwa kwa gharama kubwa ambayo ni zaidi ya Sh milioni 300 za Kitanzania. Kibaya zaidi, hakuna bima za afya zinazokubali kutoa huduma hiyo mteja wake anapopoteza uwezo wake wa kuona

Wataalamu wa teknolojia na tiba ya macho wanasema Argus II inaleta matumaini makubwa kwa wasioona na kuwa maboresho zaidi yatawezesha watumiaji wake kutofautisha rangi na kuweza kuona kwa ufasaha zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles