KULWA MZEE- DAR ES SALAAM
KESI ya kuchapisha video ya ngono inayomkabili msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu, imepanga kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka Machi 18, mwaka.
Uamuzi huo umetolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonda, baada ya upande wa mashtaka kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo.
Wakili wa Serikali, Glori Mwenda, alidai mahakamani hapo kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali na upande wa mashtaka wapo tayari kumsomea.
Wakili wa utetezi, Ruben Simwanza, alidai hana pingamizi mteja wake kusomewa maelezo ya awali.
Wakili Glory alidai kuwa Wema
anakabiliwa na shtaka moja la kuchapisha video ya ngono katika mtandao wa
kijamii.
Wema anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Oktoba 15, 2018 katika maeneo
mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo alisambaza video za ngono kupitia
akaunti yake ya Instagram, picha ambazo inadaiwa kuwa hazina maudhui.
Alidai Wema ambaye ni mkazi wa Mbezi Salasala, anamiliki mtandao wa kijamii wa Instagramu wenye jina la @Wemasepetu.
Alidai siku hiyo ya tukio, mshtakiwa alirekodi video ya ngono ambayo haina maudhui kupitia simu yake ya kiganjani, akitumia laini ya Vodacom yenye namba 0755 555 6 55.
“Baada ya kurekodi video hiyo, Oktoba 25, 2018, mshtakiwa aliisambaza katika akaunti yake ya Instagram, wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
“Video hiyo aliyorekodi Wema, ilikuwa inaonyesha kuwa Wema alikuwa ananyonyana ndimi (denda) na mwanamume, huku akijua kuwa kitendo hicho ni kinyume na maadili ya Tanzania,” alidai.
Inadaiwa Oktoba 25, 2018 maofisa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), waliiona video hiyo na kuripoti tukio hilo katika kituo cha Polisi Kijitonyama.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa baada ya maofisa wa TCRA kuripoti tukio hilo, Wema alikamatwa Oktoba 29, 2018 na kupelekwa katika kituo Kikuu cha Polisi (Central), ambapo alihojiwa na polisi.
Wema alikubali kuwa anamiliki akaunti ya Instagram yenye jina la Wemasepetu, alikiri kukamatwa Oktoba 29, 2018 na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa.
Pia alikubali kuwa alifikishwa Mahakama ya Kisutu, Novemba mosi, 2018, kujibu shtaka linalomkabili.
Upande wa mashtaka unatarajia kuwa na mashahidi watano katika kesi hiyo. Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18, mwaka huu ambapo upande wa mashtaka wataanza kusikiliza ushahidi.