UN, NEW YORK
UMOJA wa Mataifa (UN) umezionya nchi zenye nguvu zaidi duniani kutochochea mzozo wa madai ya matumizi ya silaha za sumu dhidi ya raia nchini Syria.
Kauli hiyo imekuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema makombora yanakuja nchini Syria.
Kufuatia hali ya taharuki kuhusiana na mzozo huo wa Syria, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilikutana kwa kikao cha dharura kujadili hali hiyo ya Syria.
Aidha Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ameitisha kikao cha dharura cha baraza lake la mawaziri kujadili uwezekano wa nchi hiyo kuhusika katika operesheni ya kijeshi dhidi ya utawala wa Syria.
Ni baada ya kuutuhumu utawala huo na washirika wake Urusi kutumia silaha za sumu dhidi ya raia katika mji wa Douma.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres, Baraza la Usalama la umoja huo mpaka sasa limeshindwa kufikia suluhisho la kidiplomasia kuhusu Syria.
Kwa sababu hiyo ametoa wito wa nchi wanachama wa kudumu wa baraza hilo Marekani, Urusi, China, Ufaransa na Uingereza kutakafakari kwa undani na kuchukua hatua madhubuti ambazo haitauchochea zaidi mzozo wa Syria.