32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

UMUHIMU WA KUMBEBA, KUMKUMBATIA MTOTO

Na CHRISTIAN BWAYA


mama-akiwa-amembeba-mtoto-mgongoniKWA muda mrefu utamaduni wa kubeba watoto mgongoni umekuwa sehemu ya malezi katika jamii nyingi za ki-Afrika. Tangu mtoto anapozaliwa, kwa mfano, wanafamilia hupokezana kumshika na kumbeba kama namna ya kuonesha furaha yao. Ni nadra mtoto mchanga kubaki mwenyewe kitandani isipokuwa katika nyakati fulani fulani.

Sambamba na kubebwa mgongoni, mtoto huyu hulala kitanda kimoja na wazazi wake mpaka hapo atakapofikia umri wa kuhamia chumba kingine aweze kulala na wenzake.

Jamii nyingine nje ya bara la Afrika zinapata shida kuelewa desturi hii. Kwao kwa mfano, ni rahisi kufikiri kuwa kumweka mtoto mgongoni ni aina fulani ya ukatili na kumkosea mtoto haki ya kuwa huru. Katika jamii hizo watoto huzoezwa maisha ya upekee tangu wanapokuwa wadogo.

Pamoja na tofauti hiyo ya kiutamaduni, mambo yameanza kubadilika kwa kasi hapa kwetu. Imeanza kuwa kawaida kwa mfano kwa wazazi kuwaandalia watoto vitanda vyao tangu wanapozaliwa. Watoto wameanza kulala peke yao. Ule utaratibu wa mtoto kubebwa kifuani au mgongoni mwa mzazi wake pia umeanza kupotea. Badala yake wazazi huwaweka watoto katika vifaa maalumu wanapokuwa katika matembezi sambamba na kuwalaza kwenye vitanda vya kujitegemea.

Zipo sababu nyingi zinazoweza kueleza kwa nini mambo yamebadilika. Kwa mfano kuna suala la mwingiliano wa utamaduni baina ya jamii mbalimbali. Hivi sasa ni rahisi kwa mzazi wa Simiyu kujua mtindo wa maisha ya wazazi wa barani Ulaya na hivyo kubadili kabisa namna anavyoishi.

Lakini pia mwingiliano huu unapokwenda sambamba na kuimarika kwa uwezo wa kiuchumi inakuwa rahisi kwa wazazi kubadili namna yao ya maisha. Wazazi wenye kipato cha kati kwa mfano, wanaweza kutengeneza kitanda maalumu kwa ajili ya mtoto mchanga kwa sababu wanao uwezo huo.

Pamoja na mabadiliko haya ni muhimu kuelewa kuwa utamaduni huu wa kubeba watoto ni suala la kimaumbile kuliko lilivyo kiutamaduni. Hata katika makundi ya wanyama wengine mbali na mwanadamu, kubeba watoto ni kawaida.

Kisayansi watoto huzaliwa na hitaji ndani yao la kuunganishwa kimahusiano na watu wengine. Wanazaliwa na njaa ya kutengeneza ukaribu na watu. Katika umri pungufu ya miaka mitatu, watafiti wanasema mtoto anahitaji ukaribu mkubwa wa kimwili na kihisia na wazazi wake. Mzazi anahitajika kufanya juhudi za kuwa karibu na mwanawe ili kujenga mahusiano hayo.

Kwa ushahidi huo mantiki ya desturi ya kubeba na kukumbatia watoto ambayo kwa Afrika ni sehemu ya maisha ya kila siku inapata nguvu. Tunahitaji kurekebisha makosa yanayoanza kufanyika katika jamii yetu. Tunahitaji kurudia desturi ya kubeba, kulala na kuwakumbatia watoto wachanga.

Watafiti wengi wa makuzi wamepata ushahidi wa kisayansi kuwa watoto wachanga wanaobebwa mara kwa mara hujenga ukaribu wa kihisia na wazazi na hivyo huwa na nafsi zilizotulia ukilinganisha na watoto wasiobebwa. Hivyo pamoja na mabadiliko ya kijamii yanayoendelea ni vyema kuendeleza desturi ya kubeba watoto kama ilivyokuwa zamani.

Tunahitaji kurudia desturi ya kulala na watoto wachanga, kwa kufanya hivyo tunajenga misingi imara ya kuwa karibu nao wangali wadogo. Madai kwamba kulala na watoto wachanga ni kuwaambukiza magonjwa hayana nguvu ya kuondoa mantiki ya desturi hii. Tujenge mazoea ya kumkumbatia mtoto kila  inapowezekana kwani kuwakumbatia kunawahakikishia kuwa wako salama.

0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles