24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

BODABODA ZISITUMIWE KUKATISHA MASOMO WANAFUNZI

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


 

wanafunzi-wa-kikeHABARI wasomaji wa safu ya bodaboda, leo tunakumbushana baadhi ya mambo yaliyopo ndani ya jamii.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, aliwahi kukemea tabia ya kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Pinda aliwahi kuagiza wale wote wanaowapa mimba wanafunzi wakamatwe na kufikishwa mahakamani ili liwe fundisho kwa wengine.

“Haiwezekani kabisa! Hivi akina baba kuamua kutembea na mtoto wa shule ya msingi ni lipi hasa unalolitaka kwake…unamwachisha shule mtoto kwa lipi hasa, hapana. Nimeshatoa agizo wahusika wakamatwe,” hayo yalikuwa maneno ya Pinda alipokuwa Chunya mkoani Mbeya.

Nimeguswa kumkumbuka Waziri Pinda baada ya kuona alichohitaji kifanyike hakifanyiki kwa kiwango kinachostahili ili kupunguza ama kumaliza tatizo la wanafunzi kupata mimba.

Biashara ya bodaboda ilianzishwa kwa nia nzuri lakini baadhi ya vijana wamekuwa waharibifu wakubwa kwa wanafunzi.

Nimeshuhudia mara kadhaa bodaboda akimkuta binti kasimama kituoni anamwita ampe lifti na kwa kuwa mabinti wenge wanapenda lifti hukimbilia kupanda wawahi shuleni.

Binti hawezi kujiuliza anapewa lifti kila siku ili kitokee nini, hajiulizi kwanini asiwape lifti watoto wadogo wa shule ya msingi ampe yeye wa sekondari, hajiulizi bodaboda huyo hana kazi zingine kwa muda huo anaotumia kumvizia yeye kituoni?

Hakuna anayejipa muda wa kujiuliza maswali matokeo yake ukiwa barabarani unashuhudia mabinti wengi wakiwa wamepakiwa katika bodaboda wawili wawili ama watatu mshikaki wanapelekwa na kurudishwa nyumbani.

Bodaboda kila kijiwe wanajuana yupi mtaalamu wa wanafunzi na wanajua wanachokifanya na hata hawajali.

Nani anachangaia matatizo haya? Siwezi kulaumu vijana wa bodaboda peke yao nikiwaacha wanafunzi wapenda lifti, katika hili pande zote mbili zina tatizo.

Siamini katika mazingira ninayoyaona katika vijiwe vya bodaboda pasiwepo binti ama mabinti waliokatisha shule kwa sababu ya kupewa mimba na vijana wa bodaboda.

Hapa wazazi wanachangia hali hiyo kuendelea kuwapo, haiwezekani binti akatishwe masomo kwa kupewa mimba usitoe taarifa Polisi akamatwe, wanakaa kimya binti anakatishwa masomo anaolewa.

Vijana tambueni mipaka ya kazi yenu, biashara ya bodaboda si kibali cha kupata wachumba wanafunzi, kuwapa lifti kusiwe kishawishi cha kuwaingiza katika mahusiano ya mapenzi katika umri mdogo.

Ni jambo la aibu unawakuta bodaboda wanataniana baada ya kuwaona wanafunzi kituoni, utasikia ‘teacher…teacher’ maana yake anaitwa bodaboda mtaalamu wa wanafunzi, utaona anachomoka alipo na pikipiki yake anapakia wanafunzi wawili mshikaki.

Mmoja wa waendesha bodaboda katika eneo la Mongola Ndege, Dar es Salaam, aliwahi kusema hawaishii kuwabeba tu bali wanawafundisha maisha.

Je, ni maisha gani bodaboda anamfundisha mwanafunzi wa kike, kwanini wasiweke utaratibu wa kuwabeba na wavulana?.

Bodabodaacheni uhuni, kama mnahitaji kuwa walimu nendeni chuo, ualimu wa kukatisha watoto wa watu masomo utawafikisha gerezani.

Wanafunzi pia mnatakiwa kuacha tamaa, acheni kupenda starehe, kama shuleni unaweza kufika kwa kutembea tembea, kama kwa kupanda daladala wahi kituoni panda. Tabia ya kupenda lifti itawaingiza katika mahusiano ya kimapenzi.

Lazima tukubali kwamba hakuna anayeweza kutoa msaada bila kutegemea kupata kitu kutoka kwa anayemsaidia, acheni kupenda lifti kama mlipelekwa shule kusoma someni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles