a makosa atafunguliwa mashtaka, na kwa hili nitachukua hatua, hawawezi kuendelea na upotoshaji wa aina hiyo.
“Watanzania wana haki ya kutoa maoni, lakini wasitumie haki hiyo kwa masilahi yao binafsi, iwe wanasiasa au raia, kama mtu anadiriki kusema kuna watu 13 wameuliwa na mmoja kuchomwa moto, ana lengo la kuitishia amani.
“Katiba ya nchi inakupatia uhuru wa kujieleza, lakini hakuna uhuru usio na mipaka, tusikimbilie haki za binadamu.
“Hatuwezi kutumia kigezo cha haki za binadamu kuvunja umoja na amani ya nchi kwa sababu una haki ya kusema chochote,” alisema Biswalo.
Alisema Lema ameorodhesha kesi nane na kudai Jumanne Nderema alichinjwa na Serikali haijafanya lolote, tukio la Feb 5, mwaka huu eneo la Sasajila, Manyoni
DPP akifafanua matukio ya vifo aliyoyataja Lema, alisema Hamis Chadem (25) amekamatwa na sababu ya kifo cha Jumanne ni mwili kukutwa na majeraha na sehemu ya shingo imekatwa.
Alisema marehemu na mshtakiwa ni mtu na kaka yake, ambapo alikuwa akimtuhumu kufanya mapenzi na shemeji yake, hivyo alimvizia alipolala na kumkata na kesi namba 4 ya mwaka huu imefunguliwa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni.
Pia alimtaja Issa Abdallah tukio lililotokea Januari 23 eneo la Sanjalanda, ambapo polisi wamefungua jalada kwa mshtakiwa Maria Robert (21).
Alisema marehemu hakuchinjwa na taarifa ya daktari inaonyesha ni mtoto wa kuzaliwa na mshtakiwa huyo, alikuwa na mgogoro na mumewe ambaye alikuwa hampatii matunzo hivyo alimnyonga mtoto wake mpaka kufa na akatoa taarifa za uongo Januari 27, amefunguliwa kesi ya mauaji namba 3 ya mwaka huu.
“Tukio la Novemba 21 mwaka jana, Mnyambelele Nyandu wa Itigi anadai amechinjwa, anarukia mambo ambayo hayawahusu, Myambelele Nyandu ni mshtakiwa kamuua mkewe Shoma Ngasa. Mshtakiwa ana wake wawili, mwengine ni Ana Makilrma, aliwapiga viboko wake zake na wakiwa ndani alimpiga mpaka kusababisha kifo chake, alifunguliwa kesi namba 22/2019.
“Tukio la Martin Motelewa, alichomwa moto. Washtakiwa Msem Hamidu (33) na Athanas Stephani maarufu Manyama walikamatwa, taarifa ya daktari na maelezo kwenye jalada ni kupigwa na kitu kizito usoni na kuchomwa moto, alikuwa amelala kwenye pagale, hakuna ushahidi wa kuwaunganisha watuhumiwa, hivyo walihojiwa na kuachiwa.
“Alex Jonas wa Manyoni mjini ni Katibu Mwenezi Wilaya Manyoni (Chadema), tukio la Februari 26 mwaka huu na sababu ya kifo ni kuvuja damu nyingi, alikuwa na majeraha upande wa uso na hadi sasa hakuna mshtakiwa aliyekamatwa na polisi wanaendelea na upelelezi. Aliuawa, lakini hakuchinjwa, alikatwa kwenye paji la uso,” alisema Biswalo.
Alisema Lema alidai pia Msechelela Leonard alichinjwa, lakini polisi wamefungua jalada na washtakiwa ni Rashidi Rashidi (34), Timothy Kindulu na Gervas maarufu Etoo.
Biswalo alisema marehemu alikuwa ni mtoto wa diwani wa CCM, alivuja damu kutokana na majeraha kichwani na michubuko tumboni, lakini hakuna maelezo kama alichinjwa.
“Kwanini watoe taarifa za uongo, kwamba Serikali na watu wake hawafanyi kitu chochote, tufanye siasa zenye ustaarabu, hakuna haki pasipo wajibu, kifungu 9 cha makosa ya jinai nawajibika kwenda kutoa taarifa polisi kueleza.
“Aje (Lema) aniambie ni lini alienda kutoa taarifa na kwamba hao watu anawafahamu, hatuwezi kuendelea kuwa na watu kueneza taarifa za uzushi na zenye kueneza chuki na kusababisha watu wakae kwa mihemuko kwamba hakuna amani.
“Baadhi ya watu wanasema wanachama wa upinzani wanaonewa wakati wanafanya mambo ya kipuuzi, usijifiche kwenye siasa, iwe CCM au chama chochote kwa kufanya watu waishi kwa hofu, haki za kikatiba zisije zikaathiri mambo ya watu wengine,” alisema Biswalo.
mwisho
Watu 357 wakiri makosa na
kulipa Sh bilioni 13.5 kwa DPP
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam
MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga amesema hadi kufikia jana jumla ya fedha zilizokusanywa kwa wale waliokiri makosa ya uhujumu uchumi ni Sh bilioni 13.5.
Biswalo alisema kiwango hicho cha fedha kinatokana na jumla ya watuhumiwa 357 waliomba msamaha kwa DPP.
Alisema mwaka jana Oktoba walianza mchakato watu kukiri makosa na kulipa fedha, lakini baadhi wamefanya fursa na kuharibu sifa za Watanzania wanaofanya kazi serikalini.
Biswalo alisema kuna watu hadi sasa hawajakamilisha makubaliano na mikataba waliosaini itarejeshwa mahakamani.
“Unapoingia mahakamani na mkataba ukasajiliwa na mahakama ikatoa amri, ile ni amri ya mahakama na usipotekeleza kuna njia za kutekeleza.
“Waache wakae, lakini wajue wasipotimiza kwa mujibu wa mkataba hatua zitachukuliwa, amri ya mahakama lazima itekelezwe, hivyo tutakazia hukumu.
“Mikataba waliyoijaza inasema kama utashindwa au kuvunja masharti yaliyomo kwenye mkataba, DPP anaweza kuchukua hatua nyingine yoyote, hivyo kama wanafanya utani, mimi sitanii, wasitufikishe sehemu ambako hatukutaka kwenda,” alisema Biswalo.
MASHTAKA YA KINA LUGOLA
Katika hatua nyingine, Biswalo alisema aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na wenzake, majalada yao yanafanyia kazi kwa mujibu wa taratibu na yanapokamilika atatoa taarifa.
Hivi karibuni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ilisema imemaliza uchunguzi dhidi ya Lugola na wenzake wanaodaiwa kuingia mkataba tata wa zaidi ya Sh trilioni 1 na wamewakuta na makosa ya uhujumu uchumi.
Ilisema tayari imepekeka jalada kwa DPP, ili aweze kuendelea na hatua nyingie shauri hilo.
Jana DPP alisema; “muda ukifika kama kuna sababu nitawaambia, kwa sasa sina cha kuwaambia, sipendi kufanya kazi nusu nusu, muda ukifika tutaweka wazi kwa sababu mna haki ya kufahamu,” alisema Biswalo.
Mwisho
Biteko: Tunataka wafanyabiashara wa madini wawe mamilionea
Na Mwandishi wetu
-Dodoma
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko, amesema Serikali kupitia wizara yake na Tume ya Madini, inaendelea kuhakikisha inawawezesha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili waweze kuwa mamilionea na Serikali ipate mapato yake kutokana na kodi na kuinua sekta ya madini.
Biteko aliyasema hayo jana akiwa kwenye ziara ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanyika katika machimbo ya mawe ya nakshi Ntyuka, Soko la Madini Dodoma na Chuo cha Madini Dodoma (MRI), yenye lengo la kufahamu utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Madini na Tume ya Madini.
Alisema ili kuhakikisha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini wanaendesha shughuli zao kwa faida, Serikali imeweka mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini na kupunguza kodi mbalimbali.
Akielezea mikakati ya kuboresha masoko ya madini yaliyoanzishwa tangu Machi mwaka jana, Biteko alisema Wizara ya Madini inaendelea kuboresha miundombinu katika masoko hayo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mashine za kupima madini, mizani na kusomesha wataalamu katika fani ya upimaji wa madini.
Katika hatua nyingine, Biteko alipongeza mgodi wa kuchimba mawe wa Ntyuka uliopo jijini Dodoma kwa kukiwezesha kikundi cha kina mama 120 kwa kuwapatia mabaki ya mawe ambayo huyatumia kuzalisha kokoto ambazo huziuza na kujipatia kipato.
Akizungumza kwa niaba ya kikundi cha kina mama wanaozalisha kokoto katika eneo la Ntyuka jijini Dodoma, Blandina Daudi, mbali na kushukuru mgodi kwa kuwapatia mabaki ya mawe kuzalisha kokoto, alieleza kuwa kupitia kazi husika wameweza kufanya maendeleo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba na kusomesha watoto.
mwisho
Ummy ataka wadau washirikiane kuhakikisha corona haiingii nchini
Na Mwandishi wetu
-Dar es Salaam
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa sekta ya afya lengo likiwa ni kujadili kwa pamoja tishio la mlipuko wa virusi vya corona.
Ummy alisema kikao hicho waliwaeleza wadau kama taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza hali ya maambukizi ya ugonjwa huo duniani, hivyo kama Serikali ni vyema kuwapatia taarifa wadau hao.
“Tumewapa taarifa wadau wetu na kuwahakikishia kwamba Tanzania hakuna mtu mwenye maambukizi ya virusi wa corona na tumewaeleza hatua gani kama Serikali tumezichukua katika kujiandaa kukabiliana na tishio hili,” alisema Ummy.
Katika kikao hicho Ummy alieleza kwamba wizara yake imeweza kuchukua hatua ya kukabiliana na tishio hilo kwa kuimarisha ufuatiliaji katika maeneo mbalimbali, ikiwemo viwanja vya ndege na viingilio vingine ikiwemo bandarini.
Hata hivyo, Ummy alisema wameweza kutoa mafunzo kwa baadhi ya wataalamu wa afya waliopo mikoani na kuandaa dawa, vifaa na vifaa tiba endapo nchi itapata mshukiwa wa virusi vya corona.
“Tumewaomba washirikiane nasi katika kuhakikisha kwamba sasa tunakuwa tayari kukabiliana na tishio hilo hata kama hatuna mgonjwa, hii tulikubaliana kwenye mkutano wa nchi wanachama wa SADC, kwamba nchi zote tunaingia kwenye hatua ya kukabiliana,” alisema Ummy.
Katika kikao hicho alisema wamewaomba wadau waunge mkono katika kutoa mafunzo zaidi, hususan kwa wataalamu wote wa afya ili kuwakinga na maambukizi pamoja na kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi.
Wadau hao wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuwashirikisha na wameridhika kwa hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huo.
Kikao hicho kiliwashirikisha WHO, mabalozi na wakuu wa taasisi za kimataifa hapa nchini.