27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa watumia Bunge kunadi ahadi za uchaguzi

CECILIA PARESONa Khamis Mkotya, Dodoma
KAMBI ya Upinzani bungeni imekuja na mbinu mpya baada ya kuamua kulitumia Bunge kutangaza ahadi mbalimbali iwapo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) utashinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Miaka iliyopita wakati wa Bunge la Bajeti, kambi hiyo imekuwa ikiishauri Serikali kuhusu jinsi ya kuongeza mapato, lakini safari hii hotuba za upinzani zimejikita katika kutoa ahadi.
Hali hiyo ilijidhihirisha jana wakati Msemaji wa Kambi ya Upinzani bungeni, Secilia Pareso, akiwasilisha maoni ya kambi hiyo, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Pareso alisema kada ya utumishi nchini ina changamoto nyingi kubwa ikiwa ni ile ya watumishi kufanya kazi kwa mazoea (business as usual), jambo ambalo limerudisha nyuma maendeleo ya taifa.
Mishahara
Katika hotuba hiyo Pareso alisema kambi ya upinzani kwa muda mrefu imepiga kelele kuitaka Serikali ipandishe kima cha chini cha mshahara kufikia Sh 315, 000 kwa mwezi lakini serikali imeamua kuziba masikio.
“Iwapo upinzani utashika dola kupitia Ukawa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, kima cha chini kitapandishwa na ngazi nyingine za mishahara zitaboreshwa, hivyo watumishi wa umma wakae mkao wa kula,” alisema.
Mafao
Kuhusu mafao ya watumishi wa umma wanapostaafu, Pareso alisema kambi yake imepokea malalamiko mengi ya watumishi wastaafu wanaosumbuliwa katika kupata mafao yao.
“Kambi ya upinzani inalaani kitendo cha Serikali kuwatumikisha watumishi na wanapostaafu inawanyanyapaa. Suala la kustaafu si jambo la ghafla au la dharura.
“Kambi rasmi ya upinzani bungeni inawaahidi watumishi wote wa umma kwamba ikiwa upinzani utatwaa madaraka katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, serikali ya Ukawa itaweka skimu ya mafao ya wastaafu,” alisema.

Kuwatambua madiwani

Pareso alisema iwapo Ukawa utaingia madarakani utahakikisha madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa wanatambuliwa kwa sheria kama watumishi wa umma, tofauti na ilivyo sasa waweze kupata stahili zao kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma.
“Madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa ni viongozi wanaochaguliwa na wananchi na wanatumia muda wao kuwatumikia wananchi. Kwa maana halisi hawa ni watumishi wa umma kwa kuwa wanatumikia wananchi.
“Licha ya uhalisia huu viongozi hawa hawatambuliwi katika sheria kama watumishi wa umma na hivyo hawajaingizwa katika mfumo wa utumishi wa umma,” alisema.
Madai ya walimu
Kuhusu madai ya walimu, Pareso alisema kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikitoa ahadi hewa za kulipa madai ya walimu, jambo ambalo alisema linashusha moyo wa utendaji kazi.
“Walimu ni sehemu ya watumishi wa umma, Serikali imekuwa ikiwatumia walimu ikiwa ni pamoja na kusimamia sense na uandikishaji wapiga kura lakini baada ya kazi zote Serikali huwasahau walimu.
“Kwa miaka yote mitano ya uhai wa Bunge hili, kambi rasmi ya upinzani bungeni imekuwa ikitetea maslahi ya walimu hasa madai ya malimbikizo ya mishahara, posho za uhamisho na posho za mazingira,” alisema.

Mikataba kuwekwa wazi

Naye msemaji wa kambi hiyo kwa Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Profesa Kulikoyela Kahigi, alisema miongoni mwa msingi wa utawala bora ambao haujazingatiwa ni suala la uwazi.
“Mpaka sasa Serikali haijakubali kuleta mikataba ya uwekezaji bungeni, jambo linaloonyesha kwamba haina mpango wa kuzuia ufisadi unaofanyika kupitia mikataba ya uwekezaji.
“Kambi rasmi ya upinzani inawaahidi Watanzania wote kwamba endapo vyama vinavyounda Ukawa vitashinda uchaguzi mkuu Oktoba na kuunda serikali, mikataba yote ya uwekezaji itawekwa wazi na kujadiliwa bungeni,” alisema.
Akizungumza nje ya ukumbi jana mchana, mbunge mmoja wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema kunadi ahadi ni mkakati wao katika Bunge hili la Bajeti.
“Sisi tumeamua kuja vingine, miaka yote katika Bunge la Bajeti huwa tunashauri lakini ushauri wetu umekuwa ukipuuzwa na Serikali.
“Kwa kuwa hili ni Bunge la mwisho, hatukuona sababu ya kuleta hotuba za kushauri na kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi na Ukawa tumetia nia ya kuchukua Serikali, tumeona bora tuwaeleze wananchi ahadi zetu nini tutafanya, badala ya kushauri,” alisema mbunge huyo kutoka kanda ya kaskazini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles