26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ujumbe mzito mwaka mpya

Na WAANDISHI WETU-DAR/MIKOANI

RAIS Dk. John Magufuli amewatakia Watanzania heri ya Mwaka Mpya wa 2020 na kuwaomba waendelee kudumisha amani na upendo ili uwe mwaka wa maendeleo na ustawi kwa taifa.

Salamu hizo alizitoa mkesha wa Mwaka Mpya, usiku wa kuamkia jana, wakati akiagana na maofisa na askari wanyamapori na Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita, ambako ametembelea na kujionea vivutio vya utalii.

Pamoja na salamu hizo, alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Chato, kufuatilia ukusanyaji wa mapato katika soko la Kasenda ili kuchukua hatua za kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato itakayobainika.

Alisema hatua hiyo itasaidia Halmashauri ya Wilaya ya Chato iweze kupata fedha zitakazosaidia kutatua kero za wananchi, ikiwamo kuboresha mazingira ya soko hilo na ujenzi wa Shule ya Sekondari Nyabugera ambao amechangia Sh milioni 5.

Rais Magufuli pia alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Eliud Mwaiteleke kutangaza zabuni ya ujenzi wa Barabara ya Kasenda – Muganza yenye urefu wa kilometa 2.2 ili ijengwe kwa kiwango cha lami kama alivyoahidi na kwamba Serikali itatoa fedha za ujenzi.

“Nchi hii ilikuwa inaliwa sana na majizi na mpaka sasa bado wapo, namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kunipa uhai ili katika mwaka 2020 niendelee kuwatumbua majizi wote na fedha tutakazopata tuzipeleke kwenye miradi ya maendeleo kama ambavyo tumenunua ndege 11, tunajenga reli (standard gauge), tunatoa elimu bure na mengine mengi,” alisema Rais Magufuli.

Pia amemuonya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, kwa matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa na halmashauri hiyo na ametaka dosari hizo zirekebishwe mara moja. 

“Nataka ujirekebishe, wananchi hawa wanateseka sana,” alisisitiza.

SALAMU ZA PONGEZI

Rais Magufuli pia alipokea salamu za heri ya Mwaka Mpya wa 2020 kutoka kwa wananchi, viongozi mbalimbali wakiwamo marais wastaafu, maaskofu na masheikh ambao wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuongoza nchi kwa mafanikio makubwa na wamemwelezea matarajio yao ya kufanikiwa zaidi katika mwaka ujao.

“Mheshimiwa Rais wangu, Dk. Magufuli, Bwana Yesu Asifiwe. Ninakupa hongera sana kwa wajibu mzito ulionao. Kwa neema ya Mungu tumejaaliwa kufikia siku ya mwisho kwa mwaka huu wa 2019.

“Mimi nakupongeza kwa jitihada zako nyingi za kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Ninakuombea na kukutakia Mwaka Mpya 2020 wa heri na mafanikio makubwa. Uso wa Bwana uende nawe popote utakapokuwa,” alisema Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo alipompigia simu Rais Magufuli.

ASKOFU AISHANGAA CHADEMA 

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Solomon Massangwa, alisema kuwa siasa ni vita visivyomwaga damu – ni maneno.

Alisema mwaka 2020 unapaswa kuwa mwaka wa taifa kupanga mkakati wenye dira ambayo inaonyesha nini kimefanyika, kilichokwama na kinachotakiwa kufanyika ili kusogeza mbele gurudumu la maendeleo.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini Arusha, wakati akihubiri katika ibada ya kusherehekea Mwaka Mpya, Kanisa la KKKT Usharika wa Mjini Kati.

Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka jana, Askofu Massangwa, alionyesha kushangazwa na kitendo cha baadhi ya vyama vya upinzani kujiondoa katika uchaguzi huo.

“Tukikutana na changamoto za aina mbalimbali, sio sababu ya kurudi nyuma, kukata tamaa, kuacha hiyo biashara, kuacha hiyo siasa au chama cha siasa siyo sawa. Ndugu zangu wa Chadema na wengine mniwie radhi, Serikali pia iniwie radhi.

“Waliposema (Chadema), hatutaki tena kuingia kwenye uchaguzi, mnaogopa ulingo wa mapambano ya kisiasa, si  mlishakubali, mmevua nguo unayaoga maji, hata kama ni ngumu kwa sababu ulishakubali.

“Ndiyo maana napenda usemi kuhusu siasa unaosema ‘siasa ni vita visivyomwaga damu, ni maneno’. Lakini upande wa pili wanasema ‘siasa ni vita inayomwaga damu’, ila kwa Tanzania hatuko upande wa pili wa vita ambayo inasababisha umwagaji damu.

“Nakumbuka nilipokuwa kijana, ukiwa unamchumbia msishana wakitaka kukunyang’anya kwa maneno wanamwambia yule msichana unakojoa kitandani, watakunyang’anya kwa maneno na anakuacha,” alisema Askofu Massangwa.

Alisema kuwa wao kama wachungaji hawapaswi kujiunga na vyama vyovyote vya siasa ili kuepuka kuegemea upande mmoja na kuwa badala yake wanawakumbatia wote bila kujali itikadi za vyama vyao.

“Unajua wanasiasa ndio wanaongoza nchi, hatuwezi kujitoa tuseme ni mchezo mchafu, kama ni mchafu unausafisha unakuwa mzuri na huwezi kusema ni mchezo mchafu, kwa hiyo wakristo hatuendi huko, hapana.

“Sisi wachungaji wenu kwa sababu vyama ni vingi, nakumbuka kipindi cha nyuma hata mimi nilikuwa mwanachama wa CCM, miaka hiyo kabla sijaenda kusoma theolojia, ila kwa sababu vyama ni vingi, sisi wachungaji wenu hatupaswi kujiunga na chama chochote kwa sababu lazima utaegemea mahali fulani, hivyo tunawakumbatia wote, lakini wewe Mkristo umesimama wapi kwenye siasa,” alisema Askofu Massangwa.

HALI YA MWAKA 2020

Akizungumzia Mwaka Mpya wa 2020, alisema ni vema Wakristo na Tanzania kwa ujumla kuwa watii kwa Mungu huku wakiwa mahodari na mashujaa katika kufanya mambo mema.

“Tukisema tunampenda Mungu na sisi Wakristo tunachukiana, huo ni uongo, kumpenda Mungu kuonekane kuanzia sisi kwa sisi, hivyo Wakristo na Tanzania tuanze mwaka 2020 tukiwa hodari na mashujaa katika mambo mema na watii mbele za Mungu na hata mambo yakiwa magumu tusiache kumwambia Mungu bila woga ili tusonge mbele,” alisema Askofu Massangwa.

UCHUMI

Akizungumzia masuala ya uchumi, Dk. Massangwa alisema ni muhimu kila mmoja katika kipindi hiki kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na uaminifu ikizingatiwa taifa lina sera ya Tanzania ya viwanda kuelekea uchumi wa kati.

“Ukifanya kazi kwa uaminifu tutafikia mafanikio kwani Mungu hutimiza ahadi zake. Akisema ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtaona, bisheni nanyi mtafunguliwa, atatimiza hayo, kama mmoja wetu ameanzisha kiwanda, tunaofanya kazi hapo tusiwe wezi.

“Tusiwe na uvivu, tufanye kazi kwa bidii na maarifa. Nakumbuka Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema mtu akizoea kula nyama ya mtu atakula tu, ukianza kuzoea kuiba kwa mwenzako ukianza kwako utajiibia na kutapanya mali hovyo,” aliongeza.

MIRADI

Kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo, alisema umefika wakati wa kuangalia namna wawekezaji wa ndani wanavyoweza kuitekeleza kwani mingi mikubwa inatekelezwa na watu kutoka nje ya nchi.

“Miradi mikubwa katika nchi hii inatekelezwa na makampuni na mashirika makubwa ya nje ya nchi hii, Wachina wanafanya miradi mikubwa katika nchi hii  kwanini? Sikatai ushirikiano ni sawa na wala hatukatai kuwakaribisha wageni.

“Lakini maziwa ya kwanza ananyonya mtoto awe mwanadamu au mnyama na mnajua maziwa ya kwanza yalivyo na thamani kubwa kwa maisha ya mtoto, kwanini mpaka leo miradi mikubwa inatekelezwa na watu wengine?

 “Tukiangalia rasilimali nyingi ikiwemo madini, kwanini tuendelee kuwa soko la watu wengine, badala ya kutengeneza bidhaa zetu na kuziuza na wao wawe soko letu huko waliko?

“Nini cha kufanya kwa mwanzo huu? Mwaka 2020 ni vizuri kutayarisha mpango mkakati, dira ya mwelekeo kuanzia ngazi za chini hadi taifa,” alisema.

MWAKA 2020 NI UCHAGUZI

Kutokana na mwaka 2020 kuwa ni mwaka wa uchaguzi wanasiasa wametakiwa kukubali matokeo ya aina yoyote yatakayotokea mara baada ya kutangaziwa matokeo.

Hayo yalielezwa jana na Mchungaji  Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches (TFC), mkoani Dodoma, Rose Amani wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya uliombatana na dua maalumu katika kanisa lililopo eneo la Kisasa jijini Dodoma.

Mchungaji huyo alisema kwa kuwa mwaka 2020 ni mwaka wa uchaguzi, wanasiasa ambao watashiriki uchaguzi wanatakiwa kukubaliana na matokeo yoyote ambayo yatatangazwa.

Alisema kama watapinga huo ndio mwanzo wa kwenda katika machafuko, hivyo wana wajibu wa kukubali ili nchi isifike katika machafuko.

Mchungaji huyo alivitaka vyama vya siasa nchini kukaa meza moja na kuondoa tofauti zao ili kuepukana na machafuko ambayo yanaweza kujitokeza.

Alisema kuwa mwaka 2020 ni mwaka wa kuwa tofauti na kujitakasa na kuondokana na tabia ya kujengeana chuki na badala yake tunatakiwa kupendana na kusikilizana.

Mchungaji Rose alisema hakuna sababu ya wanasiasa kusigana au kutofautiana kati ya chama na chama bali wanatakiwa kukaa meza moja ili kufikia mwafaka.

Alisema kuwa wanasiasa wanatakiwa kuwa na roho ya kusameheana, kupatana baina ya vyama vya siasa, kuvunja roho za visasi pamoja na kukubaliana na matokeo kwa chochote ambacho kitatokea.

Katika mkesha huo kulikuwa na vipengele nane vya maombi, vikihusisha maombi ya kujitakasa, toba kwa maovu ya taiga, maombi ya kuvunja nguvu za giza kwa mkuu wa anga, kuwaombea Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na viongozi wote wa Serikali na kisiasa.

Maombi mengine yalikuwa kuombea Uchaguzi Mkuu wa 2020, maombi ya kuombea maridhiano ya kitaifa, kuomba kwa ajili ya kuimarika na kukua kwa uchumi wa taifa, kuombea Jumuiya ya Afrika Mashariki na mabalozi wote sambamba na mihimili mingine ya dola.

MWAKA WA NEEMA

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Blastoni Gavile, alisema kuwa mwaka 2020 ni mwaka wa neema kubwa ya fedha kwa kila Mtanzania na utakuwa mgumu kwa wavivu.

Pamoja na hali hiyo, aliwataka Wakristo nchini kuombea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu ili kuweza kupata viongozi wazuri na wenye hofu ya Mungu.

Alisema ili kuweza kupata viongozi hao ni lazima uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu huku akiwataka wananchi wa wenye sifa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi badala ya kuwaachia watu wengine huku wao wakibaki walalamikaji.

Ushauri huo aliutoa jana katika ibada ya mkesha wa Mwaka Mpya 2020 iliyofanyika Kanisa Kuu la Iringa.

Alisema ni lazima kila mmoja kuendelea kuombea amani ya nchi na kuweza kupata viongozi wenye sifa na hofu ya Mungu.

HABARI HII IMEANDALIWA NA  JANETH MUSHI (ARUSHA), FRANCIS  GODWIN (IRINGA) NA RAMADHAN HASSAN (DODOMA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles