23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ujenzi Reli ya Kati wayeyuka

Philip-MpangoNa Elias Msuya, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amefuta ndoto ya wabunge waliopigia debe ujenzi wa Reli ya Kati akisema haiwezekani kwa bajeti ya Serikali.

Ujenzi wa reli hiyo ulikuwa ni ahadi ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete ya mwaka 2010 alipokuwa akiwania awamu ya pili ya urais wake lakini haikutekelezeka.

Pia ahadi hiyo imetolewa na Rais John Magufuli katika kampeni zake za mwaka jana akisema lazima itajengwa katika utawala wake.

Wakijadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano na mwaka mmoja bungeni Dodoma hivi karibuni, wabunge wengi hasa wa mikoa ya Kanda ya Kati na Magharibi walipigia kelele ujenzi wa reli hiyo katika kiwango cha ‘standard gauge’.

Hata hivyo, katika majumuisho ya mjadala wa mwongozo wa bajeti ya mwaka 2016/2017, Dk. Mpango, alisema kwa sasa uwezekano wa kujenga reli hiyo kwa fedha za ndani haupo.

Alisema utafiti uliofanyika ili kubaini kama ujenzi huo utakuwa wa manufaa kibiashara (commercially viable), umeonyesha kuwa itahitajika reli yote na matawi yake kwenda nchi jirani za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yajumuishwe.

“Gharama ya kujenga reli ya kati inakadiriwa kuwa kati ya dola bilioni 7,000 hadi bilioni 9,500 za Marekani kwenye tuta jipya na kama itajengwa kwenye tuta lililopo itagharimu nusu ya fedha hizo,” alisema Dk. Mpango na kuongeza:

“Sasa kwa uchumi wetu ambao tuna GDP (pato la ndani) ya dola bilioni 53 au shilingi trilioni 100 na ushee hivi uchumi wetu bado ni mdogo kubeba mzigo huu.”

Dk. Mpango alisema kama Tanzania itajenga reli hiyo kwa mapato yake itatumia zaidi ya miaka 300 kwa kuwa ni madogo.

Alisema kama Tanzania ikijenga reli hiyo kwa miaka minne kwa kujinyima huko, zitatumika Sh trilioni nne kwa kila mwaka mmoja.

Alikosoa ushauri uliotolewa na wabunge wa kushughulikia reli yake peke yake bila kuzihusisha nchi za jirani akisema hautawezekana na utaikosesha fursa ya biashara.

Alishauri kufuata mpango wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Jukwaa la Uchumi la Dunia (WEF) ambao wameshaanza mpango wa ujenzi wa reli hiyo kwa kuzihusisha nchi za Burundi, Rwanda na DRC.

Akifafanua zaidi nje ya ukumbi wa Bunge, Dk. Mpango, alisema lazima ujenzi huo wa reli uwe wa ubia na nchi na mashirika ya kimataifa.

“Ni vizuri tuambizane ukweli maana namba hazidanganyi, tusije tukawaambia wananchi kuwa tutajenga reli kwa fedha zetu wakati hatuna uwezo,” alisema na kuongeza: “Kuna utaratibu unaofanywa chini ya WEF na iko timu ambayo mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown, inayotusaidia kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga reli ya kati lakini kwa maana kwamba mradi huu unakuwa wa kikanda na sio wa nchi moja.”

Alisema katika mchakato huo, Kanda za Afrika zilishindanishwa na Kanda ya Kati (Central Corridor) inayohusisha Tanzania, Burundi na DRC ilishinda ikifuatiwa na Kanda ya Beira.

Hata hivyo, alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa bandari za Dar es Salaam, Kalema na Kigoma.

Kuhusu Reli ya Mwanza, alisema nayo itajengwa na kutakuwa na treni zinazotembea juu ya maji kwa ajili ya kwenda Uganda.

“Kwa hiyo sio Tanzania kukaa pembeni na kusema tunaliweza wenyewe, tutumie sasa hizi taratibu ambazo wenzetu wanatusaidia. Tutumie PPP (ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi).

Alisema hadi sasa kuna kampuni ambazo zimejitokeza kuwekeza kwenye ujenzi huo kutoka Marekani na China.

“Kuna kampuni moja ya Kimarekani ilishaonyesha interest, kuna kampuni ya China na walishaanza kujenga kipande Soga Station kama kilomita mbili. Lakini sasa mchakato wa ununuzi uliparaganyika ila bado wana interests ya kujenga reli,” alisema.

Hata hivyo, alisema mchakato wa kujenga reli hiyo ni mrefu kutokana na gharama kubwa na ugumu wa kupata wafadhili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles