28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

Ukawa wabebeshana misalaba bungeni

MBWENA KHAMIS MKOTYA

KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, jana alitangaza baraza la mawaziri kivuli huku akiwabebesha misalaba mizito baadhi ya aliowateua.

Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na pia mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo ni NCCR- Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), amewapangia baadhi ya mawaziri wake kivuli kusimamia wizara tofauti na ujumbe wao ndani ya Kamati za Kudumu za Bunge.

Mawaziri kivuli waliopangwa kusimamia wizara tofauti na ujumbe wao ndani ya Kamati za Bunge hawatakuwa na sifa ya kupiga kura ya maamuzi ndani ya kamati hizo na wataruhusiwa kuingia kama waalikwa ambao pia hawatalipwa posho za vikao.

Aidha, katika uteuzi wa baraza hilo la mawaziri kivuli 39, Mbowe amewaacha pembeni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) na Saed Kubenea wa Ubungo (Chadema) ambao walikuwa wakitajwa tajwa kuwemo kwenye baraza hilo.

Akitangaza baraza hilo bungeni jana kwa kuzingatia vyama vinavyounda Ukawa, Mbowe alisema Chadema kinawakilishwa na wabunge 27, CUF wabunge 11 na NCCR-Mageuzi mbunge mmoja.

Alisema uteuzi wake umezingatia kanuni ya 15 inayompa mamlaka ya kuteua baraza kivuli.

Awali, Mbowe alinukuliwa na vyombo vya habari akisema vigezo atakavyotumia katika uteuzi wa baraza lake ni elimu, uzoefu, jinsia na vipaumbele vyao.

Mawaziri vivuli ambao kamati zao zinatofautiana na majukumu ya wizara zao ni Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini na mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ambaye ni Naibu Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Ukimwi.

Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Molles ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria.

Lissu

Akizungumza na MTANZANIA katika viwanja vya Bunge, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema uteuzi wa baraza hilo ni mzuri kwa kuwa umezingatia uwezo, uzoefu na taaluma za wabunge.

Hata hivyo, alisema mawaziri hao kwa sasa inabidi kuchagua aidha kushiriki kamati zao au kuingia katika kamati ambazo wizara zao zinawajibika.

“Kwanza kanuni hazikatazi mbunge akiwa kamati moja akateuliwa kusimamia wizara inayowajibika kamati nyingine.

“Hapa ni suala la kuchagua, lakini yapo madhara kama matatu, kwanza wataingia kama wageni kwenye kamati ambazo zinahusika na wizara wanazosimamia na itakuwa ni busara ya mwenyekiti kumruhusu kuchangia kwa kuwa si mjumbe wa kamati.

“Pili wakati wa uamuzi hawatapiga kura, tatu hawatapata posho. Kama wanataka posho itawabidi waende kwenye kamati zao ingawa kwetu sisi ni kazi tu posho hazina umuhimu,” alisema Lissu.

Alipoulizwa kuhusu Zitto kutupwa nje, Lissu alisema hilo liko wazi kwa sababu siyo mwenzao ndani ya Ukawa.

Hata alipoulizwa pamoja na sababu hizo, kwanini hawakufumba macho kama hatua ya kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano na kujenga afya ya demokrasia, alisema kufumba macho ni hatari na haiwezekani kwa sababu wanaweza kujikuta wanaingia shimoni.

Mnyika

Kwa upande wake Mnyika alisema ni wakati mwafaka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kufanya marekebisho ya muundo wa kamati za Bunge kwa kuwahamisha mawaziri kivuli kwenda kwenye kamati ambazo wizara zao zinawajibika ili kuondoa mkorogano.

“Ni kweli tutapata wakati mgumu lakini tutafanya kazi hivyo hivyo ingawa changamoto zipo. Huu ni muda mwafaka Spika kufanya mabadiliko ili kudhihirisha Kamati za Bunge hazikupangwa Ikulu,” alisema Mnyika.

Lijualikali

Naye Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali, alisema uteuzi huo utaleta matatizo kwa sababu hautamuwezesha  kushirika vizuri kwenye kamati yake.

“Sasa kule sipo na huku ninapoingia nitachangia kwa busara ya mwenyekiti asipokuwa na hiyo busara ndiyo imetoka sasa hapo ni kama vile sina kamati, ili kuondoa haya inabidi tuhamishwe kamati,” alisema.

Joel

Alipoulizwa Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema Kanuni za Bunge zinaruhusu mbunge yeyote kuingia katika kamati yoyote.

“Anaruhusiwa kuingia kamati yoyote isipokuwa hatapiga kura. Na hili la kuhamishwa kwenye kamati zao za sasa linamhusu Spika, kama ataona inafaa anaweza kufanya hivyo vinginevyo hakuna namna,” alisema Joel.

Baraza kivuli

Akitangaza baraza hilo, Mbowe alisema yeye mwenyewe atasimamia Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais, Tamisemi ni Mbunge wa Moshi Mjini, Jafar Michael (Chadema) na naibu wake ni Joseph Mkundi (Chadema).

Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ni Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema), Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) ni Mbunge wa Malindi, Ally Saleh Abdallah (CUF) na naibu wake ni Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema).

Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) ni Esther Bulaya (Chadema) na naibu wake ni Yusuph Kaiza Makame (CUF) na Maftah Abdallah Nachuma (CUF).

Wizara ya Fedha na Mipango, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema).

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ni Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na naibu wake ni Mbunge wa Karatu, Willy Quambalo (Chadema).

Wizara ya Nishati na Madini, ni Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema).

Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kanda na Kimataifa, ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Shahali Mngwali (CUF).

Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) na naibu wake ni Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Immaculate Sware Semesi (Chadema).

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ni Juma Hamad Omar (CUF) na naibu wake ni Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF).

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Viti Maalumu, Salma Mwassa (CUF).

Wizara ya Maliasili na Utalii, ni Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko akisaidiwa Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso wote kutoka Chadema.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ni Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema).

Wazari ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi ni Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lymo (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Mgogoni, Dk. Ali Suleiman Yusuf (CUF).

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ni Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel (Chadema) na naibu wake ni Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Sakuru (Chadema).

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na naibu wake ni Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja wote kutoka Chadema.

Wizara ya Maji na Umwagiliaji, ni Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) na naibu wake ni Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema).

Wizara ya Katiba na Sheria, ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) akisaidiana na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles