LONDON, UINGEREZA
POLISI wa Uingereza wamesitisha kubadilishana taarifa za siri na Marekani zinazohusu shambulio la bomu la kujitoa mhanga mjini Manchester.
Hatua hiyo imeripotiwa kuwa inatokana na hofu ya kuvuja kwa taarifa hizo katika vyombo vya habari nchini Marekani, hali inayoweza kuvuruga msako wa mtu anayeaminika kuhusika katika utengenezaji wa bomu lililoua watu 22, Jumatatu wiki hii.
Iwapo itathibitishwa, hatua hiyo ya kuzuia kupeana taarifa na mshirika wake muhimu kabisa katika ulinzi na usalama, itaonyesha kiwango cha hasira ya Uingereza kuhusu vitendo vya uvujishaji siri kwa vyombo vya habari vinavyoshuhudiwa nchini Marekani sasa.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, alitarajia kuzungumzia hilo wakati wa mkutano wake na Rais Donald Trump wa Marekani mjini Brussels, Ubelgiji jana.
Hilo linakuja baada ya gazeti la New York Times kuchapisha picha za eneo lililotokea mashambulizi mjini humo, nyaraka ambazo walibadilishana na wenzao wa Marekani.
Shambulio hilo lilitokea Jumatatu wiki hii katika ukumbi wa tamasha la muziki uliojaa watu kaskazini mwa mji huo.
Picha hizo ni pamoja na mabaki ya bomu linaloshukiwa kutumiwa katika shambulio hilo, mfuko wa kubeba mgongoni uliokuwa umebebwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga na kuonyesha damu katika mabaki ya magari yaliyoharibiwa.
Katika siku za hivi karibuni, Rais Trump mwenyewe na maofisa wake wamekuwa wakishutumiwa kuvujisha kwa vyombo vya habari na Urusi taarifa za kijasusi inazopewa na washirika wake.
Baada ya shambulio baya kabisa kuwahi kutokea Uingereza tangu mashambulizi ya kigaidi ya mwaka 2005, polisi iko katika msako kumtafuta mshirika inayemshuku alimsaidia Salman Abeid kutengeneza bomu hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za kijasusi za Ujerumani, raia huyo wa Uingereza mwenye asili ya Libya, alizuru mji wa Dusseldorf, Ujerumani siku nne kabla ya kuendesha shambulio hilo la kujitoa mhanga.
Mji huo ulio kilometa 300 magharibi mwa mji mkuu wa Berlin, unaelezwa kuwa na wahamiaji wengi kutoka mataifa ya Kiarabu hasa wenye itikadi kali za kidini.
Wachunguzi wanaonyesha Abedi alikuwa sehemu ya mtandao mpana wa wanamgambo wanaoendesha harakati za kigaidi.
Kinachowapa hofu majirani wa Abedi hivi sasa ni uhusiano ambao haujulikani kati yake na ndugu zake ambao ni washukiwa na kati ya shambulio hilo na imani yake.
Wakati baba yake Abedi na ndugu zake wanashikiliwa kwa uchunguzi nchini Libya, wanahabari wamezuru msikiti mkubwa mjini Manchester kutaka kujua ushahidi wa kuhusika katika shambulio hilo.