27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MSHAURI WA RAIS AWAPONDA UHURU, RAILA

NAIROBI, KENYA


MSHAURI wa Rais Uhuru Kenyatta na waziri wa zamani wa vyama vya ushirika, Joseph Nyagah, amejitosa rasmi katika kinyang’anyiro cha urais, huku akiwataka Wakenya kuwakataa Rais Kenyatta wa Jubilee na mgombea urais wa upinzani wa NASA, Raila Odinga katika uchaguzi wa Agosti 8.

Nyagah, ambaye amejiuzulu ushauri wake kwa rais na ambaye atawania kama mgombea binafsi asiyekuwa na chama, alisema Rais Kenyatta na Odinga hawana lolote la kuwafanyia Wakenya.

“Nikichaguliwa kama mgombea binafsi asiyekuwa na chama, nitakuwa na fursa ya kutangamana na vyama vyote vya kisiasa bila kizuizi. Nitahakikisha kuwa Wakenya wanaohudumu katika Serikali yangu wanatoka katika kila jamii bila kuzingatia kabila wala dini,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Gachoka (sasa Mbeere Kusini).

Nyagah alipuuzilia mbali dhana kwamba kinyang’anyiro cha urais kitakuwa baina ya mafahari wawili; Rais Kenyatta na Odinga.

“Ni dhana potovu kusema kwamba uchaguzi ujao wa urais utakuwa baina ya farasi wawili. Mimi naitwa Nyagah ambayo inamaanisha mbuni. Je, kati ya farasi na mbuni ni yupi ana mbio zaidi?” aliuliza waziri huyo wa zamani wa vyama vya Ushirika.

Nyagah aliahidi kukabiliana na umasikini, uhaba wa chakula, ukabila, kuboresha kiwango cha elimu, kushughulikia masilahi ya vijana na wanawake, kukabili ufisadi, kusitisha ukopaji wa fedha kutoka mataifa ya kigeni kwa kutaja ahadi chache.

“Uhaba wa chakula unaoendelea kushuhudiwa nchini na ongezeko la deni ambalo Wakenya wanadaiwa na mataifa ya kigeni, ni ishara kuwa kuna haja ya kufanyia mabadiliko Serikali.

“Wakati Jubilee ikiingia madarakani mwaka 2013, deni la Kenya lilikuwa Sh trilioni 1.6 na sasa limefikia Sh trilioni 4. Hiyo inamaanisha kuwa kila Mkenya aliye hai anadaiwa Sh 100,000,” alisema Nyagah.

Nyagah aliteuliwa uwaziri na Odinga aliyekuwa Waziri Mkuu wakati wa Serikali ya ‘nusu mkate’ chini ya Rais Mwai Kibaki.

Kwa mujibu wa takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), jumla ya wagombea 18 wamewasilisha maombi yao ya kutaka kuwania urais.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles