23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Ugaidi tena Kenya

NAIROBI, KENYA

  • Polisi wasema ni shambulio la kigaidi,Alshabaab wadai kuhusika

WATU ambao idadi yao haijafahamika wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha wanaodaiwa kuwa magaidi kushambulia hoteli ya kifahari jijini hapa jana.

Wakati milipuko mikubwa ya mabomu na milio ya risasi ilipotetemesha jiji, watu walikimbia huku na kule kwa kihoro.

Kundi la wanamgambo wa Al-Shabab la Somalia lililoendesha shambulio baya la kigaidi mwaka 2013 katika kituo cha biashara cha maduka ya kisasa cha Westgate jijini hapa na kuua watu 67, limedai kuhusika na shambulio hilo, likiahidi kutoa maelezo zaidi baada ya operesheni waliyowatuma wapiganaji wao kukamilika.

Shambulio hilo lilitokea katika majengo yenye hoteli kubwa maarufu ya DusitD2, benki kadhaa na ofisi za kampuni mbalimbali, hasa za kimataifa, Barabara ya 14 Riverside, Kitongoji cha Westlands.

Moto, miale ya moto na wingu jeusi la moshi lilishuhudiwa likielekea angani kutokea eneo la kuegeshea magari.

Magari kadhaa yalikuwa yakiteketea moto huku watu wengi wakikimbia kujinusuru, wengine wakionekana kujeruhiwa.

Waliojeruhiwa walikimbizwa hospitali zikiwamo AgaKhan na Nairobi zilizoelezwa kuelemewa na majeruhi pamoja na upungufu wa damu.

Mtu mmoja alionekana akibebwa kwa machela na baadhi wamejificha nyuma ya magari wakilia.

“Hali inatisha. Nilichoona kinatisha sana. Nimeona nyama za binadamu zimetapakaa kila mahali,” alisema Charles Njenga aliyekimbia kutoka eneo la tukio.

“Nilikuwa nimejificha. Wafanyakazi wenzangu walikuwa wkaikimbia huko na kule,” alisema huku akihema kwa nguvu.

Shuhuda mwingine, Robert Murire, alisema aliona miili miwili eneo la tukio pamoja na washambuliaji wakiwa wamevalia nguo za kijani wakiwa na mkanda wa risasi.

Shuhuda mwingine, Simon Crump, ambaye anafanya kazi katika moja ya ofisi, alisema wafanyakazi walijichimbia katika ofisi zao baada ya milipuko kadhaa kusikika.

“Hatukuwa tukijua nini kilikuwa kikitokea. Milio ya risasi inatokea kutoka pande mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa watu walishikwa na hofu kubwa.

Milio ya risasi ya polisi ilisikika katika jiji zima na helikopta za polisi zilionekana angani.

Kwa mujibu wa waandishi wa habari waliokuwa eneo la tukio, watu wenye silaha na vikosi vya usalama walikuwa wakishambuliana kwa risasi.

“Kulikuwa na mabomu, kuna milio mingi ya risasi,” alinong’oneza mtu mwingine anayefanya kazi eneo hilo akiomba kutotajwa.

NAMNA WASHAMBULIAJI WALIVYOINGIA HOTELINI

Mashuhuda walieleza kuwaona watu sita au zaidi wenye silaha wakiingia eneo hilo.

Washambuliaji hao waliwasili wakitumia magari mawili madogo, likiwamo lenye namba KCN 340E, huku jingine likifuatia baada ya kulazimisha kuingia Barabara ya 14 Riverside Drive, hali iliyowalazimisha walinzi kufungua geti baada ya kuwatupia risasi.

Kisha washambuliaji wakafanikiwa kuingia ndani ya uzio na kurusha mabomu kuelekea eneo la kuegeshea magari kabla ya kuzama ndani ya hoteli ya Dusit D2.

Gari lililotumiwa na washambuliaji hao lilizingirwa na kikosi cha kutegua mabomu kilichokuwa kikihaha kulichunguza iwapo lina mabomu zaidi.

Vikosi vingine vya Recce, Flying Squad na kile cha kupambana na ugaidi vikiongozwa na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai, George Kinoti vilikuwa vikiitikia mapambano.

Hadi wakati gazeti hili likienda mitamboni, polisi walikuwa wakijaribu kubaini mahali walipo washambuliaji, wakitumia ramani ya jengo ili waweze kuingia ndani ya Dusit D2 kuwakabili pamoja na kuendelea na operersheni ya uokoaji.

Wakati operesheni ikiendelea, mshukiwa mmoja alikamatwa na watu wengi kuokolewa wakati polisi wakiendelea kuizingira DusitD2.

Mahali walipojichimbia washambuliahi bado palikuwa hapajulikani wala idadi yao kufahamika.

POLISI WAZINGIRA MAJENGO KARIBU NA HOTELI

Polisi wamesema hali si nzuri na wamewashauri watu kutopita eneo hilo, ambalo lilishuhudiwa magari mawili yakiwaka moto.

Watu kadhaa walikuwa wamejeruhiwa na kuhudumiwa na maofisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakisaidiwa na watu wengine wa kujitolea.

Baadhi ya watu waliokwama kwenye vyumba vya jumba hilo wamekuwa wakiandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii wakieleza kwamba wamekwama au kujificha.

 “Polisi inathibitisha kuwa kumetokea shambulio katika Barabara ya Riverside 14. Eneo limezingirwa na hivyo watu na waendesha pikipiki watumie njia nyingine ili kuwezesha polisi kuendesha operesheni ya uokozi na dhidi ya wahalifu kwa ufanisi,” iliandika Tume ya Taifa ya Huduma za Polisi katika mtandao wa tweeter.

“Timu zote za polisi ziko eneo la tukio. Kwa sasa tunalichukulia kama kitu chochote ikiwamo shambulio kubwa,” alisema kwa njia ya simu msemaji wa polisi, Charles Owino.

“Timu zote za polisi ikiwamo maofisa wa kupambana na ugaidi wako eneo la tukio,” alisema.

Wakati Mkuu wa Jeshi la Polisi Kenya, Joseph Boinnet akikataa kuthibitisha taarifa za idadi ya vifo wala majeruhi, kama ilivyothibitishwa na mashuhuda wafanyao kazi eneo hilo, baadhi ya polisi walio katika operesheni ya kuwakabili wavamizi eneo hilo, walikiri kuona miili ya waliokufa, lakini walidai hawakuwa na muda wa kuihesabu.

AL-SHABAAB WADAI KUHUSIKA

Msemaji wa wanamgambo wa al-Shabab alipiga simu kwenye Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), akidai kundi lao limehusika katika operesheni ambayo bado inaendelea Nairobi.

Msemaji huyo hakutoa maelezo zaidi, lakini alisema watatoa zaidi punde operesheni yao ikikamilika katika hoteli hiyo.

Alitoa maelezo zaidi akisema; “watu wetu waliingia ndani na bado wako ndani ya majengo muhimu Mtaa wa Westlands, Nairobi wakiendelea na kazi tuliyowatuma.”

MASHAMBULIZI MENGINE YA KIGAIDI

Tukio la jana linawakumbushia wakazi wa Nairobi shambulio baya la kigaidi lililoua watu 67 wakati wanamgambo wa al-Shabaab walipovamia maduka ya kisasa ya Westgate mwaka 2013.

Kenya ilikabiliwa na mlolongo wa mashamblizi ya kigaidi baada ya kutuma jeshi nchini Somalia Oktoba 2011 kukabiliana na al- Shabaab waliokuwa wakiendesha matukio ya utekaji, hasa watalii.

Aprili 2, 2015 kundi hilo lenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda likaendesha shambulio jingine lililoua watu 148 katika Chuo Kikuu cha Garissa, mashariki mwa Kenya.

Aidha shambulio la jana limekuja miaka mitatu baada ya shambulio la al-Shabab katika kambi yao huko el-Adde nchini Somalia.

Kundi hilo liliteka na kudhibiti kambi ya majeshi ya Muungano wa Afrika mjini el-Adde na kuua wanajeshi 63 wa Kenya.

Lakini taarifa nyingi huru zinadai waliouawa ni zaidi ya hao.

Rais wa Somalia wakati huo, Hassan Sheikh Mohamoud baadaye pia alieleza kuwa wanajeshi kati ya 180 na 200 waliuawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles