29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Magufuli apiga marufuku kuondoa vijiji katika hifadhi

Mwandishi wetu -Dar es Salaam


RAIS John Magufuli ameagiza kusitishwa hatua ya kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa kuwamo katika maeneo ya hifadhi.


Amewataka viongozi wa wizara zinazohusika kukutana ili kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji hivyo.


Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli aliagiza viongozi wa wizara husika kubainisha maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu ambayo hayana wanyamapori ama misitu ili yagawiwe kwa wafugaji na wakulima.


Pia Rais ameeleza kutofurahishwa kwake na mazao kufekwa kwa kisingizo cha kupandwa ndani ya mita 60 za mito.


Alitoa maagizo hayo jana alipokutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangallah, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, (Tamisemi), Joseph Nyamhanga na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Dorothy Mwanyika.


Kwa mujibu wa taarifa hoiyo, Rais Magufuli pia ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia upya hatua ya kuweka mipaka ya hifadhi na makazi, na kutumia busara katika uwekaji wa mawe ya mipaka hiyo ili kutowaondoa wananchi katika maeneo ambayo hayana ulazima wa kuwaondoa.


“Mimi sifurahii kuona wafugaji kila mahali wanafukuzwa, kama kuna eneo ambalo tunafikiri lilikuwa hifadhi ya wanyama lakini halitumiki, tutabadilisha sheria, tunalimega na tunaligawa kwa wafugaji.


“Vivyo hivyo hata kwa wakulima kama kuna eneo tunaona ni hifadhi lakini halina msitu wala wanyamapori, na lina rutuba na wakulima wanataka kulima, nalo tunalimega tunawapa wakulima.


“Baadaye tutajua kabisa eneo hili ni la hifadhi, hili ni la mifugo, hili ni la wakulima, hili ni la makazi. Kwa hiyo nyinyi mawaziri na makatibu wakuu mkakae mkatangulize maslahi ya hawa tunaowaongoza ambao ni wakulima, wafugaji, wavuvi na kadhalika.


“Pia tunahitaji wanyamapori, sijasema sasa hifadhi zote za wanyama tunazimaliza, hapana, hifadhi za wanyama lazima tuzihifadhi,” alisema Rais Magufuli.
Taarifa hiyo pia ilisema Rais Magufuli ameagiza vijiji 366 vilivyoainishwa kuwamo ndani ya maeneo ya hifadhi nchini, visiondolewe katika maeneo hayo.
Badala yake ametoa mwezi mmoja kwa viongozi wa wizara zote zinazohusika kubainisha maeneo ya vijiji hivyo na kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya sheria iyawasilishwe katika kikao kijacho cha Bunge.


Alisema ni lazima Serikali ifanye uamuzi huo kwa kuwa idadi ya Watanzania imeongezeka na kufikia milioni 55, mifugo imefikia milioni 35.


Alisema kutokana na hali hiyo, kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya maeneo ya ardhi ikilinganishwa na wakati nchi ilipokuwa inapata uhuru ambako Watanzania walikuwa milioni tisa na mifugo ilikuwa milioni 10.


Taarifa hiyo pia ilisema Rais Magufuli ameagiza sheria ya vyanzo vya maji pia iangaliwe upya ili kutowazuia Watanzania wanaozalisha mazao kandokando mwa mito na ameelezea kutofurahishwa kwake na vitendo vya kufyeka mazao ya wakulima kwa madai kuwa wamelima ndani ya mita 60.


Taarifa hiyo ilisema pia Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwasilisha mapendekezo ya kufutwa mashamba ambayo hayajaendelezwa,
Ameagiza wizara hiyo iendelee kumpelekea mapendekezo ya mashamba yote yaliyotelekezwa ili ayafute na wananchi wagawiwe kwa ajili ya kuyatumia kwa uzalishaji wa mazao na mifugo.


Alisema maagizo hayo hayana maana kuwa sasa wananchi waruhusiwe kuvamia maeneo ya hifadhi, na ametaka uwekaji wa mipaka ufanyike haraka na kwa uwazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles