27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ufuta waingiza bil 37/- kwa wakulima

Ramadhan Hassan -Dodoma

 UFUTA umeingiza Sh bilioni 37.3 katika soko la mauzo kwa msimu wa 2020 kutokana na mfumo wa stakabadhi ghalani na kati ya fedha hizo wakulima wamelipwa Sh bilioni 32.

 Takwimu hizo zilitolewa jana jijini hapa na Ofisa Mtendaji wa Soko la Bidhaa Tanzania, Nicholaus Kaswela wakati akiwasilisha mada katika warsha ya wadau wa mazao.

 Warsha hiyo ya kitaifa ilihusu utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala na soko la bidhaa Tanzania (TMX) kuhusu mazao ya ufuta na korosho ambapo wadau walikutanishwa kujadili mifumo hiyo na changamoto zake.

 Kaswela alisema licha ya changamoto ambazo zimejitokeza kutoka maeneo mbalimbali, lakini mfumo wa stakabadhi ghalani umekuwa mkombozi wa wakulima na umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza thamani ya mazao.

Alisema mauzo ya ufuta kwa maeneo yaliyofuata mfumo huo yalikuwa mazuri kwa kilo moja kufikia bei ya Sh 2,420 wakati kwa maeneo ambayo hawakufuata mfumo soko lilishuka hadi Sh 900 kwa kilo ya ufuta.

Katika msimu huu, mikoa iliyotajwa kuwa na uzalishaji wa kiwango cha juu ni Mtwara, Dodoma, Pwani na Singida ambayo hata katika mauzo imekuwa na kiasi kikubwa kwenye masoko hayo.

 “Kumekuwa na mabadiliko makubwa baada ya kuboresha mfumo wa stakabadhi ghalani licha ya ukweli kuwa bado kuna changamoto kwa baadhi ya maeneo na kuwepo malalamiko kutokana na mambo madogo madogo, lakini ukiacha hayo, mfumo umekuwa mkombozi kwa wakulima wetu,” alisema Kaswela.

Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Dk. Charles Mwamaja, alisema bado kuna tatizo katika mfumo wa masoko ikiwemo ukosefu wa masoko yenye uwazi na ushindani kwa wakulima.

 Dk. Mwamaja alisema pato la mkulima limekua kwa asilimia 17 katika kipindi cha miaka mitano fedha zilizopatikana kutoka sekta ya kilimo ziliongezeka kutoka Sh trilioni 15.2 kwa mwaka 2015 hadi Sh trilioni 29.5 kwa mwaka 2019.

 Aliitaja sekta ya kilimo kwa ujumla wake imekua kwa wastani wa asilimia 5.8 kutoka asilimia 5.2, hivyo kusaidia katika ongezeko la uchumi wa taifa na pato la mtu mmoja mmoja, lakini zao la ufuta likaelezwa kuwa mfano kwa mazao mengine.

 Mtendaji Mkuu wa Masoko ya Kilimo, Godfrey Malekano alisema bado kuna kazi ya kufanya katika sekta hiyo kutokana na wanunuzi wa mazao ya biashara, ikiwemo ufuta kuwa ni wachache.

Alisema wanaendelea kufanya juhudi za kushirikisha wadau wengine katika kutafuta masoko ikiwemo ubalozi wa China ambao wamekubali kushirikiana ili kuboresha soko la nje ambalo litasogeza ushindani kwenye masoko ya ndani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles