25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

UCHUNGUZI ESCROW WATIMIZA MIAKA MIWILI

JONAS MUSHI Na MAULI MUYENJWA, DAR ES SALAAM


 

frank-kanyusiUCHUNGUZI wa kuchotwa zaidi ya Sh bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow na kuuzwa mitambo ya kufua umeme ya Independent Power Solution Tanzania Limited (IPTL) kwa Kampuni ya Pan Africa Power (Tanzania) Limited (PAP), umefikisha miaka miwili sasa.

Vilevile, ukimya umeendelea kutawala   tangu Bunge litoe maazimio manane kuhusu suala hilo, miaka miwili iliyopita.

Tangu litolewe azimio hilo, hakuna chombo chochote cha uchunguzi na usalama kilichotoa taarifa ya utekelezaji wake na watuhumiwa kufikishwa mahakamani.

Taarifa ambazo MTANZANIA imezipata kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya taasisi za dola, jalada la usajili wa Kampuni ya PAP mpaka sasa linaendelea kushikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa uchunguzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili na Leseni za Biashara (BRELA), Frank Kanyusi, alithibitisha kuwa jalada hilo  linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya uchunguzi.

“Bado jalada lao (PAP) lipo kwenye vyombo vya uchunguzi linaendelea kuchunguzwa,” alisema Kanyusi.

Takukuru nayo imelithibitishia MTANZANIA kwamba bado inaendelea na uchunguzi wa suala la Escrow.

Msemaji wa taasisi hiyo, Musa Misalaba, alisema  taasisi hiyo inaendelea na uchunguzi huku akisisitiza kuwa suala hilo si kitu cha siku moja.

“Uchunguzi ni ‘process’ (mchakato), si kitu cha siku moja na sitaki kuzungumza mambo mengi kwa sababu ni suala la uchunguzi,  bado linaendelea,” alisema Misalaba.

Alisema taasisi hiyo ipo makini katika kusimamia kazi zake hivyo kila kitu kitafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Maazimio ya Bunge

Tarehe kama ya leo,  Novemba 28 mwaka 2014, Bunge lilipitisha maazimio manane likiwamo la kuvitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kwa watu wote waliotajwa kuhusika na suala  hilo na kuwachukulia hatua za sheria.

Pamoja na watu wengine, Kampuni ya PAP ilikuwa muhusika wa kwanza wa suala hilo kwa vile ilidaiwa kuchota fedha kwenye Akaunti ya Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akaunti hiyo ilifunguliwa na pande mbili zilizokuwa zinabishana juu ya uhalali wa fedha ambazo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilipaswa kuilipa IPTL.

Katika Bunge hilo, tuhuma mbalimbali zilitolewa kwa PAP na mtoa hoja aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (akiwa Chadema kwa wakati huo), ambaye hivi sasa ni Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

Akizungumzia kuhusu uhalali wa PAP kumiliki IPTL bungeni, Zitto alisema haina uhalali huo kutokana na kukiuka taratibu mbalimbali na kuvunja sheria za nchi.

“Uhalali wa PAP kumiliki IPTL umejibiwa na taarifa ya uchunguzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ipo kwenye nyaraka zenu (wabunge ), lakini naiweka tena mezani.

“TRA wamegundua ‘fraud’ (udanganyifu) kwamba kuna nyaraka za kughushi, mkataba kutokuwa na majina, kodi haikulipwa na kwa barua yake TRA imethibitisha imeandika barua kuwaarifu (PAP) kuwa inaondoa ‘certificate’.

“Hata Waziri Mwigulu Nchemba (aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango) amezungumza  vizuri hapa na nampongeza sana kwa sababu ameonyesha barua hiyo hapa kwamba imemnyang’anya PAP certificate si mmiliki tena wa IPTL,” alisema Zitto.

Alisema pia kwamba hakukuwa na uhamishaji wa hisa kwa mujibu wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hivyo PAP si mmiliki wa IPTL.

 “Inakuwaje awe mmiliki wakati hakukuwa na ‘transfer’ ya hisa na ndiyo maana CAG alienda Hon Kong kuangalia kama kweli PAP alikuwa na hisa hizo, lakini hakuzikuta.

“Badala yake, alikuta za Standard Chartered.Tunakubali vipi PAP awe mmiliki? ” alihoji Zitto.

Kutokana na tuhuma hizo, azimio namba moja la Bunge lilisema Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria dhidi ya watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya kamati.

Watu hao ni wanaodaiwa kuhusika na vitendo vyote vya jinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi unaoendelea kuhusika katika vitendo vya jinai.

PAP KUINUNUA IPTL

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mmiliki wa Kampuni ya PAP, aliinunua IPTL mbayo ilikuwa na mgogoro na Tanesco.

Inadaiwa kwamba kabla PAP hajainunua IPTL, kulikuwa na mgogoro kati ya IPTL na Tanesco,  mgogoro ambao ulizidi baada ya PAP kudai imeinunua IPTL.

PAP iliinunua IPTL kutoka kwa Mechmar iliyokuwa ikimiliki asilimia 70 ya hisa na VIP iliyokuwa na umiliki wa asilimia 30.

Ushahidi mwingine kuhusu suala hilo ulitolewa bungeni  na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi kwa wakati huo) bungeni.

Kafulila  alidai   ushahidi wa cheti ulionyesha kuwa PAP ilinunua asilimia 30 ya hisa za VIP, lakini haikuwa na ushahidi wa ununuzi wa hisa asilimia 70 za Mechmar.

Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Wawekezaji (ISCID), lilitoa hukumu ya awali Februari 2014 na kutoa siku 90, kwamba Tanesco ikae na IPTL wapige upya hesabu za bei ya umeme kwa vile ilikuwa  inatoza zaidi.

Kafulila alisisitiza kuwa suala hilo lilikuwa  wazi kwa vile lilithibitishwa na Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu, alipoitwa kwenye Kamati ya Bunge na akasema alipewa maelekezo ya kutoa fedha hizo.

PAP iliinunua IPTL siku chache baada ya kulipwa mabilioni yaliyokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Ushahidi wa nyaraka ambao ulipatikana na kuchapishwa kwenye vyombo mbalimbali, ulionyesha tayari mmoja wa wabia wa IPTL, alikuwa amelalamika na kuomba PAP wasilipwe fedha za Escrow kwa vile walikuwa hawajamlipa fedha zake, lakini alilipwa baada ya BoT kuilipa fedha   PAP.

Taarifa hizo ziliibua uwezekano kwamba huenda PAP ilitumia fedha za IPTL kuinunua, jambo ambalo liliibua mapya zaidi katika suala  hilo.

Mwisho….

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles