26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MZEE WA UPAKO: NIMETIKISA NCHI

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM


 

mzee-wa-upako3MCHUNGAJI Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’, ameibuka na kusema  amesimamisha nchi kwa tukio lake la  kutuhumiwa kufanya fujo na kuwatukana majirani zake wiki iliyopita.

Mzee wa Upako alitoa kauli hiyo jana mbele ya waumini wake kwenye mahubiri ya Jumapili katika Kanisa lake, Ubungo Kibangu  Dar es Salaam, alipokuwa akiwaelezea kuhusu tukio lake hilo.

Kiongozi huyo ambaye alianza kutoa mahubiri yake saa 5:55 asubuhi, alisema binafsi anafurahi kwa kuisimamisha nchi kwa tukio hilo kwa kupamba vichwa vya habari vya magazeti Alhamisi Novemba 25.

Katika mahubiri hayo alisisitiza kuwa tukio hilo halijamkatisha tamaa.

“Kila baraka ina gharama yake, siwezi kujisemea… watasema wao wakimaliza mimi ndiyo nitaanza kusema, pamoja na uzoefu wote wa vita hamtaniweza.

“Nimesikia wengine mko hapa lakini hamniwezi najua baada ya mwezi mtakuwa mmechoka na mimi nitaanza kusema’

“Kuna mama alikuwa hajapata mtoto zaidi ya miaka sita nikamtabiria kuwa mwaka huu atapata mtoto na leo ana mtoto mbona hamjaandika front page?( kurasa za mbele).

“Lakini imekuwa Mzee wa Upako matatani, mzee wa upako… babu yako?,” alihoji  kiongozi huyo huku akipigiwa makofi na waumini wake.

Alisema kwa sasa hakuna jipya kwa sababu hata Yesu Kristo alisema katika mafundisho yake kwamba ‘siku za mwisho mtasingiziwa’.

“Lakini nataka niwaambie kuwa sijavunjwa moyo, hizo zote nahesabu kama chapa za utumishi wangu bado naendelea.

“Nimefurahi kuona kuwa nchi nzima imesimama, kila kona ni Mzee wa Upako…nimekamata vichwa vyote vya magazeti makubwa kama MTANZANIA na mengine.

“Kila gazeti unakuta Mzee wa upako kaka juu pale na mustachi wake, ilihali kulikuwa na habari sijui Rais anakabidhi nini lakini mimi ndo nikawa nimekaa mbele pale,” alisema.

Alisema umaarufu wake hakuupata kupitia vyombo vya habari kwa hiyo haviwezi kumshusha kwa vyovyote vile.

“Kama magazeti yangekuwa yamenipandisha basi yangeweza pia kunishusha lakini kadri ambavyo yananichafua ndivyo Mungu anavyozidi kunitakasa.

“Gazeti kubwa kama MTANZANIA ambalo linauza nakala zaidi ya milioni 20 kwa siku limeacha kuandika habari za uchumi na biashara na mambo mengine likaniandika mimi.

“Siyo mbaya kusikiliza tuhuma zako lakini unatakiwa uwe na roho saba, najua wengi mlitaka niseme neno lakini siwezi kusema hilo sababu siwezi kuyumbishwa na matukio…tuwaachie wenyewe waendelee na mambo yao,” alisema Mzee wa Upako ambaye alikuwa amevaa suruali nyeusi na shati nyeupe la mikono mirefu.

Aelezea tukio

Mchungaji Lusekelo pia alitumia muda huo kuelezea kisa kizima cha tukio lake lililosababisha akamatwe na kuhojiwa na polisi.

Akinukuu baadhi ya vifungu vya   Biblia, Mchungaji Lusekelo alisema, “Mtu akisema akiwa na hasira mwache aseme mpaka hasira zake ziishe, kwani kwenye umoja malaika wema watakuwa na wewe.

“Hakuna jambo baya kama kumsingizia mtu, utapata shida katika maisha yako utakufa lakini matendo yako yatabaki milele.

“Hivyo usimtungie mtu maneno ambayo hayapo, wajibika kwa makosa yako na siyo ya mwingine.

“Nakumbuka siku ya tukio saa 10:30 alfajiri niliona watu wawili, Masai na binti mmoja hivi nikawauliza mmetoka wapi huku na hii ni barabara yangu nimejenga mwenyewe?

“Badala yake wakaanza kunitukana, nikasema mnanitukania kwangu kumbe walikuwa walinzi wametoka sehemu wakakimbilia kwenye nyumba moja ya mzungu. Lakini kesho yake watu wanasema Mzee wa Upako amemtukana jirani yake.

“Kujizuia ni ishara ya ukomavu hakuna mtu anayekwazwa na jirani yake iwapo mna maelewano.

Mtu yeyote anapokuwa jirani yako akiona yupo salama kwako usimzushie.  Hata hivyo nimeona wameandika Mzee wa Upako amtukana jirani yake.

“Maeneo yale mimi sina jirani ni kama wanaishi majitu tu hivyo ngoja waseme wakimaliza ndipo na mimi nitasema, kwani Yesu alisema  hakuna jipya mtasingiziwa, mtaonewa,” alisema.

Alisema anashangaa kuona vijana wa Sirro (Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro) wanataka kumkamata kwa nia ya kuzidi kumuumiza bila kumpa nafasi ya kumsikiliza.

“Hata Yesu alikamatwa hivyo siogopi, siyo mnaungaunga tu maneno mimi simuogopi mtu wala selo, au gereza la  Keko… siyo mnaunga tu maneno kuwadanganya watu, unakuja kunikamata sawa ila sema ni kwa kosa gani.

“…mimi siogopi polisi bali naogopa kuvunja sheria za nchi mimi nimekula kiapo, kwangu kufa ni Kristo kuishi ni Kristo wala matendo yangu yasiwafadhaishe,” alisema kiongozi huyo nakufanya waumini wake kumshangilia.

Taarifa za mchungaji huyo kufanya vurugu, zilisambaa katika mitandao mbalimbali ya jamii, huku video aliyorekodiwa eneo la tukio ikimuonyesha akizungumza huku akionekana kama mtu aliyekunywa pombe.

Wakati wa tukio hilo, Mchungaji Lusekelo alikuwa ameegesha gari lake barabarani kiasi cha kusababisha usumbufu na foleni ya magari mengine.

Chanzo cha tukio hilo kinadaiwa ni kulipiza kisasi kwa jirani zake hao wanaoishi katika nyumba namba KAW/MZN/1348, ambao alidai wamekuwa wakimkebehi kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ya ulevi.

Baada ya purukushani hizo, polisi kutoka katika Kituo cha Kawe walifika eneo hilo saa 3.00 asubuhi, wakamchukua   na kumpeleka kituoni.

Inadaiwa baada ya kufikishwa kituoni hapo, mchungaji huyo alipimwa kiwango cha ulevi na kukutwa 131, ambacho kinaelezwa kuwa ni kikubwa (ulevi wa kupindukia).

Ilipofika saa 5.00 asubuhi, mchungaji huyo alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) ambako huko nako inadaiwa alipimwa kilevi na kuonekana kushuka hadi kufikia 121.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles