28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Lini CCM wamewahi kuwa wakweli?

Mtz template • Sunday ikuuuu copy.indd

NA RATIFA BARANYIKWA,

KABLA sijaenda moja kwa moja kuchambua kile nilichokusudia leo, niwarudishe kidogo nyuma juu ya habari ambayo iliwahi kuripotiwa Februari 8, 2015 na gazeti hili iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Wakubwa wamtaka Magufuli urais’.

Ni habari ambayo binafsi nilishiriki kukusanya baadhi ya taarifa.

Wakati habari hiyo ilipotoka mwanzoni kabisa kabla CCM haijaanza mchakato wa kumtafuta mrithi wa Rais Jakaya Kikwete ilikuwa si rahisi kwa walio wengi wakiwamo wana-CCM wenyewe kuamini kile tulichokiandika.

Baadhi ya watu wakiwamo wana-CCM walituita wazushi, waongo na maneno ya kashfa ya kila aina.

Wengine walitucheka kwa dharau, wapo walituambia kwa kejeli kwamba hatujui siasa za nchi hii, walisahau wajibu wetu kama waandishi wa habari wa kuhabarisha, kuelimisha, kufichua nk.

Walituona kituko kwa sababu upepo ulikuwa unavuma vyema kuelekea upande wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ambaye inasemekana alikuwa akipigiwa chapuo na familia namba moja.

Hata miongoni mwa wale ambao leo hii wanajifanya kuwa mstari wa mbele kwa Magufuli, walituambia tunatumika, hakuna aliyekuwa tayari kuamini kile tulichokiandika, walituona wababaishaji.

Leo hii ninapotizama nyuma, huwa ninacheka kicheko cha furaha, nafurahi kwa sababu moja tu tulitimiza wajibu wetu kama waandishi wa habari.

Kama tulivyodharauliwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, wiki hii gazeti lile lile ninaloliongoza kwa namna ile ile tumeitwa wazushi, waongo.

Wengine wamekwenda mbali wakidhani tuna nia ovu baada ya kuripoti habari ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kuachwa na ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mwishoni mwa wiki baada ya baadhi ya watu waliokuwa katika ujumbe wake kuonekana kuwa na shida katika nyaraka zao za kusafiria.

Miongoni mwa waliotuita waongo ni CCM kupitia mtandao wao wa twitter.

Chama hicho kilikwenda mbali na kupindisha kile tulichokiripoti siku ya Jumapili eti kikionyesha mshangao wa tukio hilo hasa baada ya JK kuwa amekwishafika Abu Dhabi alikokuwa ameelekea.

CCM ikijua kwamba katika habari hiyo tuliyoiripoti siku ya Jumapili ilieleza bayana kwamba endapo ujumbe huo wa Kikwete utakamilisha taratibu zote utaondoka siku hiyo, lakini bado walituita waongo na ikataka jamii iamini hivyo.

Ukweli ni kwamba Kikwete ambaye alikuwa ameongozana na mke wake, Salma pamoja na ujumbe wa watu wapatao wanne alilazimika kuondoka Jumapili saa 6:20 usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Oman (Oman Air).

Kwa misingi hiyo, ninaweza kusema pasipo shaka kwamba kwa kauli yake hiyo, CCM imedhihirisha kwa mara nyingine kwamba, ni nadra kwake kusema ukweli.

Mtu mmoja aliwahi kuandika na pengine hili CCM ilichukue kama changamoto kwamba; katika yote inayozungumza asilimia 15 tu ndio ukweli, mengine yote uongo.

Hili linaweza kuthibitishwa na mambo kadhaa ambayo imeyafanya huko nyuma na mfano mmojawapo ni kashfa ya zaidi ya sh bilioni 40 kutoka  Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Watu wenye kumbukumbu zao watakuwa wanakumbuka jinsi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Willibroad Slaa alivyoitwa mzushi na baadhi wa wana-CCM wakati alipoweka hadharani nyaraka zilizoonyesha jinsi fedha hizo zilivyokwapuliwa.

Aliyekuwa Spika wa Bunge la 10, Samuel Sitta (Mungu amrehemu ) alimwambia Dk. Slaa kwamba Bunge haliwezi kufanyia kazi ‘vipeperushi’ vyake.

Lakini baada ya Dk. Slaa kushtaki kwa wananchi na upepo kuwa mbaya dhidi ya serikali ya Kikwete, vipeperushi vikafanyiwa kazi tukasikia baadhi wamefikishwa Mahakamani huku wengine wakiombwa na utawala huo wa serikali ya nne wazirudishe fedha hizo kimya kimya bila majina yao kutangazwa.

Si hilo tu Mtanzania yeyote makini ambaye anakumbuka kauli mbiu ya CCM iliyobebwa na Kikwete wakati huo akitafuta nafasi ya urais ya ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’ leo hii anaweza kukubaliana na mimi juu ya kile ninachokiita uongo wa CCM.

Ipo mifano mingi ya uwongo wa CCM ikiwamo katika sakata zima la Escrow, ahadi hewa na mambo kadha wa kadha.

Ukitaka kujua kwamba CCM hawaogopi kusema uwongo ni pale walipoamua kuwalaghai waislamu ili hali wakifahamu fika kwamba hata vitabu vitakatifu vinakataza kusema uwongo.

CCM waliahidi mahakama ya Kadhi  tangu mwaka 2005 na waislamu wakajua wakichagua CCM basi mahakama imepatikana.

Waislamu walipigwa dana dana kwa zaidi ya miaka 10.

Walipoona uchaguzi wa 2015 unakaribia na bado wameshindwa kutekeleza ahadi hiyo, lilipokuja dudu la Katiba kwenye Bunge Maalum la Katiba, waislamu walidanganywa tena.

Ili Katiba ya ‘Chenge’ ipite walianza kuambiwa eti wapigie kura ya ndio ili ikipita tu basi serikali itapeleka muswada wa sheria kuhusu mahakama ya kadhi.

Kilichotokea baada ya hapo majibu wanayo Waislamu wenyewe.

Rais John Magufuli mwenyewe pamoja na machache mazuri aliyoyafanya ndani ya kipindi kifupi, alipoingia madarakani miezi michache tu serikali yake ikashusha bei ya umeme.

Kumbe ilikuwa ni hadaa leo hii miezi saba baadae inatangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.19 kutoka bei ya sasa.

Wakati fulani mwanasiasa mmoja simkumbuki vizuri aliwahi kusema ni aibu kuwa na taifa na wanasiasa wanaoongoza dola ambao kwao, uongo “is the order of the day”.

Kwamba hata mambo ambayo yanahitaji msimamo na kielimu wanaingiza uongo.

Na mimi nasema kwa wenzetu wanaojali maadili, uongo ni sababu tosha ya kumweka pembeni kiongozi au chama.

Tukatae kujenga mfumo wa kusema uongo, vinginevyo tunajiandalia janga la taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles