23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Benki zetu zinaogopa hata kuuza chenji !

page-3

Na Markus Mpangala,

BIASHARA ya benki tangu ilipoanza karne nyingi zilizopita, wapo watu walionufaika kupindukia, kwa mfano familia ya Mayer Amschel Rothschild(1743-1812).

Mayer Amschel Rothschild ni mzaliwa wa Jiji la Frankfurt, nchini Ujerumani. Rothschild ni miongoni mwa wanadamu waliofanya biashara kubwa ya fedha hadi kuwa wakala wa Serikali ya Uingereza.

Sera za uchumi za Bara la Ulaya zilihusishwa na nguvu ya familia ya Rothschild kutokana na kujihusisha nayo kwa kipindi kirefu, kufahamiana na wachumi, wanasiasa na watu muhimu katika utungwaji wa sheria.

Umahiri wa Rothschild katika biashara ya fedha, alichukuliwa kuwa mshauri wa kifedha kwa tajiri Hessen-Kassel, William IX. Baada ya kuona faida na uwezo mkubwa wa kuendesha biashara hiyo, aliwarithisha watoto wake, Amschel Mayer Rothschild (1773-1855), ambaye alibaki jijini Frankfurt.

Mwingine ni Salomon Rothschild (1774-1855) naye alibaki jijini Frankfurt hadi mwishoni mwa vita ya Napoleonic, kisha alikwenda kuanzisha tawi la benki la familia hiyo jijini Vienna.

Halafu kulikuwa na Nathan Mayer Rothschild (1777-1836), ambaye alianzisha tawi la familia hiyo jijini London, nchini Uingereza ambako walikuwa wakala wa serikali katika masuala ya fedha.

Baadaye Nathan Rothschild alimzaa Lionel Nathan Rothschild (1808-1879), ambaye alichukua cheo cha umeneja wa benki yao iliyokuwa Uingereza. Baadaye Lionel Rothschild alichaguliwa kuwa mbunge nchini humo.

Angalau kwa ufupi, maana kuna mlolongo mrefu wa kizazi cha Rothschild.

Si nia yangu kuelezea historia ya familia hiyo, lakini unapozungumzia masuala ya benki na biashara ya fedha, si rahisi kutotaja familia hii, sababu kuanguka kwake katika miaka ya 1980 kulisababisha nchi nyingi kuporomoka kiuchumi.

Ni sababu hii Ufaransa ikataifisha biashara za benki na kuwa mali ya taifa. Hivyo basi, suala la biashara ya fedha maana yake ni benki, maana yake kuuza na kununua chenji. Kuuza na kununu chenji ni suala ambalo linahusisha uwepo wa benki.

Hapa nchini tunazo benki nyingi zinazoongozwa na mawazo ya kipuuzi kabisa. Bahati mbaya sana, benki hizo zimeendelea kutoelewa maana ya kununua na uuzaji chenji.

Matokeo yake kuna biashara isiyo rasmi ya kuuza chenji ambayo imezagaa kutokana na kutokuwapo kwa utaratibu mzuri wa usimamizi. Benki zetu zimekuwa katika ushindani wa kuanzisha huduma za wachezaji kamari na kunyang’anyana wateja tu.

Uuzwaji wa chenji katika benki zetu haufanyiki. Hakuna sababu za msingi za kutofanyika kwa biashara hiyo kwa utaratibu rasmi,  hali ilivyo mitaani imezidi kuwapa nafasi vijana kujiingiza katika biashara hiyo.

Ni vipi nchi yetu itapiga hatua katika maendeleo kwa kuuza chenji? Sina elimu ya uchumi, hata hivyo, siamini kwa hatua hii ya kuachia uuzwaji holela wa chenji ni nyenzo ya maendeleo. Sidhani kama tunaweza kusonga mbele kimaendelo kwa kuuza chenji.

Sijawahi kuona vijana wauza chenji kwa makondakta kama wamepiga hatua zaidi ya kufanya biashara hiyo kwa kwenda na kurudi nyuma wakidhani wanasonga mbele.

Ninawazungumzia wanaoshinda kutwa wakiuza chenji kwenye magari ya daladala.

Mathalani kondakta akitoa noti ya Sh1,000, anapewa sarafu za Sh 900, kwa hiyo muuzaji anapata faida Sh100. Muuzaji anakusudia kupata faida kubwa, lakini hauwezi kuwa mchango wa maendeleo ya taifa letu kwa mtindo wa kubangaiza kama huu. Maendeleo yanakuja kwa kuzalisha hata kama ni viwanda vidogovidogo, vikiwa vingi vina mchango mkubwa sana kimaendelo, leo hii hata bahasha tunanunua za nje ya nchi, vijana wetu wanauza chenji tu.

Tuna huduma nyingi za kutuma na kuchukua fedha kwenye kampuni za simu, ambazo hakuna shaka hilo ni kama kuuza chenji.

Kazi ambayo ilitakiwa kufanywa na beki zetu zilizopo. Pamoja na faida ndogo inayopatikana kwa wauzaji chenji hawa, lakini ni kielelezo kwamba, benki zetu zinafanya kazi zikiwa nyuma kimaendeleo miaka 40.

Wakuu wa benki zetu hawana haja ya kutuacha tununue chenji mitaani. Hawana sababu yoyote kuacha biashara hii ikiingia katika maeneo ambayo si rasmi, hali ambayo inaangamiza maisha ya vijana wengi.

Kwa msingi huo, benki zetu haziwezi kukwepa lawama kwamba zimeshindwa kabisa kufanya kazi zao kwa ufasaha. Ni rahisi sana benki zetu kutupiwa lawama, kwani zinaongozwa na taratibu mbovu zenye kujaa imani ya miaka 40 iliyopita kwamba suala la ubadilishwaji wa fedha (chenji) ni aina ya ushirikina.

Wakurugenzi wetu wa benki hizo wameshindwa kuelewa kuwa ni chenji hizo ziliwapa uwakala akina Mayer Amschel Rothschild. Hawajui kuwa kuuza na kununua chenji ni sehemu ya biashara ya benki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles