25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF: POLISI WANAMBEBA LIPUMBA

Na  Kulwa Mzee-Dar es Salaam


 

maalim-seif-sharif-hamadKATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amelituhumu Jeshi la Polisi kwa kubariki hujuma zinazofanywa na Profesa Ibrahimu Lipumba kwa kushirikiana na wafuasi wake kuvuruga chama.

Maalim Seif amemuandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, akimuomba achukue hatua dhidi ya watendaji wake  wanaobariki hujuma hizo.

Alisema hayo jana alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu changamoto zinazokipitia chama hicho.

“Chama kinakabiliwa na changamoto nyingi katika kutekeleza majukumu yake kutokana na vitendo vya hujuma vinavyofanywa na Profesa Ibrahimu Lipumba (Bwana yule) na wafuasi wake kwa msaada wa Jeshi la Polisi.

“Jeshi la Polisi limekua likivamia na kuvuruga mikutano halali ya chama cha CUF.

“Matukio yako mengi lakini nayataja haya baadhi, Lipumba na kundi lake alivamia  mkutano mkuu maalum wa chama  na kuuvuruga Agosti 21 mwaka huu katika Hoteli ya Blue Pearl, uliogharimu Sh milioni 600.

“Utekaji wa wanachama na viongozi unaofanywa na makundi ya Profesa Lipumba pamoja na kuripotiwa bado hakuna kilichofanywa,” alisema.

Alitaja matukio ya uvamizi wa ofisi za chama Bagamoyo ambazo zilivunjwa na kuweka kufuli mpya kuzuia kazi za chama zisiendelee.

“Wabunge wetu walizuiliwa kufanya mikutano ya ndani lakini Bwana yule (Profesa Lipumba) anapewa kibali na Jaji Mutungi alimuandikia barua na nakala kwa IGP ili Jeshi la Polisi litoe ulinzi  katika mikutano yake maeneo mbalimbali,”alisema.

Alisema pamoja na kutolewa taarifa za matukio yote ya utekaji na uharibifu unaofanywa na wafuasi wa Lipumba bado jeshi hilo limekaa kimya.

Alisema CUF iliamua kuchukua hatua kwa kumtafuta Waziri Nchemba lakini hakupatikana kutokana na majukumu yake lakini wamemuandikia barua.

“Nimemuandikia Mwigulu barua Novemba 24 mwaka  huu yenye kumbukumbu CUF/HQ/AKM/2016/vol/000 kuelezea matendo yanayofanywa na watendaji wake ili achukue hatua zinazostahili.

“Inashangaza kuona Jeshi la Polisi linashirikiana na wahalifu, linalinda wahalifu wasifikishwe mbele ya sheria.

“Jeshi la Polisi limeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa weledi, linaingilia shughuli za siasa.

Lipumba alijiuzulu kwa matashi yake mchana kweupe, pamoja na kushauriwa sana na viongozi wa chama na dini alikataa kata kata,”alisema Maalim.

Alisema hujuma zote zinazofanywa zinahusiana na harakati za kudai haki Zanzibar na kuna ushahidi wa mazingira kwamba dola imo ndani yake.

“Wanataka niendelee na mgogoro niache kudai haki, mimi na Lipumba hatuna ugomvi, ugomvi uliopo ni kati ya Lipumba na chama, hata tukikutanishwa leo siwezi kubatilisha uamuzi wa Baraza Kuu.

“Lipumba bado hajasema sababu za kujiuzulu, awaambie Watanzania asiruke ruke,”alisema na kuongea kwamba yuko tayari kufanya mdahalo na Profesa Lipumba.

Maalim Seif alisema  kutokana na kuonyesha msimamo dhidi ya dhuluma inayofanywa na Profesa Lipumba na Serikali dhidi ya CUF, Msajili amezuia ruzuku.

“Kuanzia Agosti 2016 Msajili hajatoa ruzuku ya CUF kwa maelezo kuwa chama kina mgogoro wakati alitaka kumpa Lipumba,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles