25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI WA UDIWANI: CCM, CHADEMA NANI MBABE?

Na Waandishi Wetu – Dar es Salaam/Mikoani

KAMPENI za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43, unaotarajiwa kufanyika leo, zimekuwa na visa na mikasa ya kila aina na kusababisha mchuano mkali kwa vyama vya CCM na Chadema katika majukwaa ya kuomba kura, huku kila kimoja kikiponda hoja, sera na ahadi zinazotolewa na mwenzake.

Jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya majigambo, tambo na kunadi sera na leo washindi katika kata hizo watajulikana baada ya wananchi kupiga kura kuchagua madiwani watakaowaongoza hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Matokeo ya uchaguzi huu unaotarajiwa kuwa huru na haki yanatarajiwa kuonyesha nguvu, taswira au mwelekeo wa vyama hivyo baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka juzi kwa kuwa katika kampeni za mwaka huu kila kimoja kilitumia nguvu kubwa kuhakikisha kinashinda.

Baadhi ya mikutano ya kampeni ya vyama hivyo pamoja na ACT-Wazalendo ambacho pia kimesimamisha wagombea, ilitawaliwa na vurugu za kupopoana kwa mawe baina ya wanachama wa vyama hivyo na wafuasi wao kujeruhiwa vibaya na kusababisha wengine kupelekwa hospitali kutibiwa.

Miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na vurugu hizo, ni Kata ya Mbweni iliyopo Jimbo la Kawe, Dar es Salaam ambako wafuasi wa CCM na Chadema walipigana mawe kiasi cha kuharibu magari na baadhi ya watu kujeruhiwa vibaya.

Usiku wa kuamkia jana, Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Saranga iliyopo Dar es Salaam, iliungua kwa moto uliowashwa na watu wasiojulikana na kusababisha vifaa vya uchaguzi yakiwamo masanduku ya kupigia kura kuteketea.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, John Kayombo, alisisitiza uchaguzi wa madiwani katika kata hiyo uko palepale na tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliahidi kupeleka vifaa vingine.

Pia vyama hivyo licha ya kunadi wagombea wao, lakini pia vilijikita katika kuzungumzia masuala mbalimbali yanayoendelea katika jamii na siasa na kugeuza mikotano hiyo ya kampeni kuwa ya kisiasa.

WAFUASI WAPYA

Katika baadhi ya maeneo, vyama hivyo viliwatumia wafuasi wao waliohamia kutoka vyama vingine ili kuongeza nguvu na hamasa katika mikutano hiyo.

Katika kampeni za lala salama, CCM iliwatumia Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, aliyejiunga tena na chama hicho hivi karibuni akitokea Chadema na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.

Kwa upande wa Chadema kupitia kampeni zao za Mwanza, ilimsimamisha aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, ambaye alizungumzia uamuzi wake wa kuondoka CCM.

Mbali na hilo, Chadema ililalamikia uvunjifu wa sheria mkoani Arusha ikiwamo maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, unaofanywa na CCM.

Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, alisema watalinda kura zao katika marudio ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika katika kata nane zilizopo mkoani humo.

Wakati Lazaro akitoa madai hayo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alisema kuna mkakati umepangwa na CCM kwa kushirikiana na kundi la wahuni kuvamia ngome za Chadema jana baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni uliofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

VITA YA MANENO

Kampeni hizo zilizotawaliwa na vita ya maneno, ziliwaibua baadhi ya makada wa vyama hivyo, akiwamo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.

Akizungumza hivi karibuni katika eneo la FFU Sokoni kwenye mkutano wa kampeni, Lowassa, aliwaambia wakazi wa eneo hilo kuwa kujitokeza kwao kwa wingi katika mkutano huo ni ishara ya kukubalika kwa mgombea wa Chadema.

“Hii ni ishara Chadema inakubalika na itashinda katika uchaguzi, mpigieni kura Moses Mollel akafanye kazi na Meya wa Jiji ambaye anatoka chama chetu, achaneni na wale wanaopita na kuwadanganya huko mitaani,” alisema Lowassa.

Pia aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, aliibukia katika kampeni za uchaguzi wa udiwani Kata ya Mhandu, wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, ambako alidai kitendo cha Nyalandu kuhamia Chadema ni sawa na mzimu unaokataa kwao.

JESHI LA POLISI LAJIPANGA

Kutokana na mwenendo wa mikutano hiyo, Jeshi la Polisi lilisema limejipanga vyema kuimarisha ulinzi katika vituo vyote vya kupigia kura katika uchaguzi wa leo. 

TAMKO LA NEC

Kwa upande wake, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilivitaka vyama vya siasa na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa amani na utulivu na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Akizungumza jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, alisema wapigakura wapatao 333,309 wanatarajiwa kupiga kura kuwachagua madiwani katika kata 43 za Tanzania Bara na kuongeza kuwa uchaguzi huo utafanyika katika vituo 884 vya uchaguzi ambako ndipo wapigakura walijiandikishia kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Jaji Kaijage alisema masharti ya mpigakura kuruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala yatazingatia sharti la kwamba majina lazima yafanane kwa herufi na majina yaliyoko katika kitambulisho mbadala ambayo yako katika Daftari la Kudumu la Wapigakura

Kuhusu mawakala wa vyama vya siasa katika vituo vya kupigia kura, aliwasihi kufuata na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza uchaguzi katika kipindi chote cha kupiga, kuhesabu na kujumlisha kura vituoni. 

ACT YAFUNGA KAMPENI DAR

Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliwaomba wananchi kujitokeza kuwapigia kura wagombea wao na kuwataka kupigia vyama vya upinzani katika maeneo wasiyosimamisha mgombea.

Zitto alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi huo uliofanyika Mtoni Kijichi, Dar es Salaam.

“Tunawaomba kesho (leo) wale wote waliojiandikisha katika kata zenye uchaguzi wajitokeze kutupigia kura, na kule ambako chama chetu hakina wagombea, nawasihi mpigie kura chama chochote cha upinzani  kilichoweka mgombea,” alisema Zitto.

Alisema katika kipindi cha mwezi mmoja wa kampeni, chama hicho kimezunguka maeneo mbalimbali kuwaeleza wananchi hali ya kisiasa na kiuchumi nchini.

“Tumeweza kufikisha ujumbe wetu wa kampeni za mwaka huu zilizojikita kwenye masuala ya haki na uchumi, tumewaeleza wananchi namna haki za raia zinavyominywa na namna uendeshaji mbovu wa uchumi unavyowaweka kwenye dimbwi la umasikini,” alisema.

Alisema chama hicho pia kilipata nafasi ya kuwaeleza wananchi namna uhuru wa mawazo unavyominywa, vyama kuzuiwa kufanya mikutano kueneza sera zao, Bunge kuzuiwa kuonyeshwa moja kwa moja (‘Live’) ili wananchi kufuatilia namna wanavyowakilishwa na ufungwaji wa magazeti ili kudhibiti uhuru wa habari. 

KINANA AUNGURUMA ARUSHA

Kinana alivunja ukimya juu ya wimbi la wanasiasa nchini kuhama vyama vyao akisema si dhambi kufanya hivyo.

Kauli hiyo aliitoa Viwanja vya Sokoni Kwamorombo katika mkutano wa kufunga kampeni za mgombea udiwani wa CCM katika Kata ya Murrieta, Francis Mbisse.

Akitolea mfano wa nchi zinazoongoza kwa demokrasia ya wanasiasa wake kuhama vyama, alizitaja kuwa ni pamoja na Marekani, India na Uingereza.

“Kenya jirani zenu, hakuna mwanasiasa ambaye hajahama chama, viongozi waliopo wote wamehama. Ni mwanasiasa Gidioni Moi ndio yupo kwenye chama chake cha Kanu kwa miaka yote, Marekani yenye miaka 300 ya demokrasia, ina wabunge zaidi ya 600 waliohama vyama vyao,” alisema na kuongeza.

“Uingereza demokrasia yao inakaribia miaka 1,000 wabunge wake zaidi ya 1,000 walihamia kwenye vyama vingine. Sasa kwetu hapa mtu akihama anakuwa amenunuliwa.”

Akifafanua sababu za kuhama, alisema tofauti na kushindwa kuelewana ndani ya vyama ndiyo inayowafanya wanasiasa kuhama.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kupishana katika sera na utekelezaji wa mambo kwa wananchi, huku mwingine akiona kuhama kunaweza kuwa fursa ya kuonyesha uwezo wake.

“Msipoteze muda mrefu kwa watu kuhama vyama, kitu gani cha ajabu mtu kuhama kutoka upinzani kwenda chama kinachotawala?

“Isituumize kichwa, watu wanahama kuangalia fursa, watu wanahama kazi kuangalia fursa na si dhambi. Jambo la vyama tuwaachie wanaohama na kwa sababu zao,” alisema Kinana.

Katika mkutano huo, pia Kinana alipokea wanachama wapya akiwamo Godluck ole Medeye, ambaye miezi michache iliyopita alitangaza kuachia nafasi yake ya ukatibu mkuu katika Chama cha UDP kinachoongozwa na John Cheyo baada ya kutoka Chadema.

NAPE

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Mtamba, Nape Nnauye, aliwataka wananchi hao kuchagua kiongozi anayejua matatizo ya wananchi.

“Tunataka mtu mwenye uwezo wa kwenda kuchukua majibu ya matatizo yenu, na hilo lipo kwa mgombea anayetokana na Serikali ya CCM,” alisema Nape.

RC GAMBO

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema amekwenda katika mkutano huo kama Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa.

Alisema kwa miezi sita iliyopita Kata ya Murrieta haikuwa na umeme, lakini kwa sasa tayari wananchi waishio maeneo hayo wamefungiwa umeme.

“Katika kipindi kifupi tumefanikiwa kusambaza nguzo za umeme kwenye kata hii. Lakini pia tunaendelea kukamilisha ujenzi wa zanahati ya Murrieti,” alisema Gambo. 

MALALAMIKO IRINGA

Saa nne asubuhi ya jana, Chadema  walisambaza taarifa katika mitandao ya   kijamii wakilalamika kuvamiwa kwa  ngome yao na watu wasiojulikana wakiwa na bastola na kuondoka na kada wake  mmoja aliyetajwa kwa jina la Linus.

Hata hivyo, taarifa hizo zilikanushwa na  Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kwa madai  kuwa kada huyo wa Chadema alikamatwa kwa mahojiano baada ya simu yake  kutumika kusambaza ujumbe wenye lengo la kuvuruga uchaguzi katika Kata ya Kitwiru.

Kamanda wa jeshi hilo mkoani Iringa, Julius Mjengi, alisema walipata taarifa za  siri kutoka kwa wasiri wake kuhusu mtandao wa vijana kutoka nje na ndani ya Iringa wanataka kuvuruga uchaguzi huo na hata kusambaza ujumbe wa vitisho kwa wananchi.

Pia alisema bado jeshi lake linaendelea  kumhoji Linus ambaye alikutwa na ushahidi wa ujumbe huo.

“Watu wanaendelea kupotosha katika  mitandao ya kijamii kuwa amekamatwa na  watu wasiojulikana, huu ni upotoshaji. Huyu amekamatwa na polisi na tunamshikilia wakati tukiendelea kuwasaka wenzake wanaotaka kuvuruga uchaguzi huu,” alisema.

 CHADEMA WATOA NENO

Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi wa chama hicho, Benson Kigaila, aliwataka wafuasi wa chama hicho kujitokeza kupiga kura, kuzilinda na wasikubali matokeo yao yachezewe.

Kigaila aliyasema hayo jana wakati akizungumzia mwenendo wa kampeni za uchaguzi huo katika mkutano wake wa na waandishi wa habari uliofanyika Kinondoni, Dar es Salaam.

“Tunasema kesho (leo) wakapige kura wasiogope kitisho, wakipiga kura wasiogope kitisho, warudi nyuma hatua 100 na waongeze moja na walinde ushindi wao,” alisema.

Kigaila alitoa madai kuwa kuna uwepo wa  taarifa kuwa wakurugenzi wameelekezwa kumtangaza mshindi wa CCM hata kama aliyeshinda ni wa Chadema.

Kutokana na hilo, aliwataka wananchi kukataa matokeo yenye mwelekeo wa kuchezewa.

“Wananchi msikubali matokeo kuchezewa, Watanzania wawe tayari kujilinda ili wahakikishe wanakuwa salama na yule anayekwenda kufanya vurugu kwenye mkutano wa wenzake apigwe sawasawa,” alisema.

Kigaila alisema chama hicho kitashinda katika uchaguzi huo kwa nguvu ya umma.

Pia alisema kuna baadhi ya maeneo ambako wafuasi wao walikamatwa na wengine kujeruhiwa na wale aliowaita wafuasi wa CCM.

Alisisitiza kauli zilizowahi kutolewa na chama hicho kuhusu kumkataa Kayombo ambaye anasimamia uchaguzi wa Kata ya Saranga kwa kuwa ni kada wa CCM.

Alisema Rais Dk. John Magufuli amevunja Katiba ibara ya 74, ibara ndogo ya 4 na 5 kwa kuteua watu ambao ni makada.

Kuhusu vurugu zilizotokea juzi huko Mbweni, alisema kuwa zilisababishwa na CCM ambao pia waliwajeruhi wafuasi wa Chadema.

Alisema iwapo Jeshi la Polisi halitachukua hatua, upo uwezekano wa wanasiasa hapa nchini kusababisha machafuko kama ilivyotokea nchini Rwanda.

Imeandikwa na Abraham Gwandu na Eliya Mbonea (ARUSHA), Francis Godwin (Iringa) na Agatha Charles (Dar es Salaam)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles