30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

BAADA YA MUGABE SASA ZAMU YA HAWA

NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

SIKU chache baada ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kutangaza kujiuzulu kwa shinikizo la jeshi la nchi hiyo, ambalo lilidai kuwa amezungukwa na wahalifu, gumzo limetanda kuhusu hatma ya viongozi wengine katika nchi kadhaa barani Afrika ambao wametawala muda mrefu zaidi.

Mugabe alitangaza kujiuzulu mapema wiki hii katika kipindi ambacho Spika Jacob Mudenda alikuwa akijiandaa kuliongoza Bunge kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye, msingi ukiwa ni baada ya Jeshi kuonekana kupenyeza ajenda yake hadi ndani ya chama chake cha ZANU-PF.

Kiongozi huyo hakujiuzulu urais pekee, bali pia alifutwa madaraka ya kiongozi mkuu wa chama chake cha ZANU-PF na mkewe Grace kuvuliwa uanachama na kuondolewa katika nafasi ya mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa chama hicho.

Wakati jeshi likifanikiwa kupenyeza ushawishi wake na kuhitimisha utawala wa miaka 37 ya Mugabe, swali kubwa na ambalo limezua mjadala katika baadhi ya vyombo vya habari vikubwa duniani, mitandao ya kijamii na katika nchi ambazo zimeishi tawala za aina hiyo, ni kuhusu hatma ya viongozi takribani 12 barani Afrika, ambao wapo madarakani kwa muda mrefu.

Viongozi hao ni pamoja na Rais wa Guinea ya Ikweta, Teodoro Obiang Nguema,  Omar al Bashir (Sudan),  Idriss Deby (Chad), Issayas Afewerki (Eritrea), Paul Biya (Cameroon) na Yoweri Museveni (Uganda).

Wengine ni Rais wa Congo Brazaville Denis Sassou Nguesso, Abdelaziz Bouteflika (Algeria), Paul Kagame (Rwanda), Joseph Kabila (DR Congo), Faure Gnassingbe  (Togo) na Pierre Nkurunziza (Burundi).

Wakati Mugabe akiwa ameondoka na kuacha taswira ya kiongozi aliyekuwa akiongoza kwa kukaa madarakani muda mrefu zaidi, pengine  hilo likichochewa zaidi na mgogoro wake na nchi za Magharibi, lakini ukweli ni kwamba alikuwa akishika nafasi ya pili nyuma ya Rais Nguema wa Guinea ya Ikweta.

Nguema ndiye anayeshika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kutawala nchi hiyo kwa miaka 38, akiingia madarakani  mwaka 1979.

Tofauti yao ni kwamba wakati Mugabe akishika rekodi ya kuwa kiongozi mkongwe zaidi duniani akiwa na miaka 93, Nguema yeye licha ya kutawala muda mrefu zaidi, ana umri wa miaka 75 kama ilivyo kwa mrithi wa Mugabe, Emmerson Mnangagwa.

Watu wanaofuatilia siasa za Afrika watakuwa wanakumbuka jinsi ambavyo Nguema aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi yaliyofanyika Agosti 3, 1979 yakimtoa kwenye utawala mjomba wake, Francisco Macias Nguema, ambaye alipigwa risasi na kikosi cha rais huyo.

Wakati mijadala mikubwa iliyotawala katika taarifa za vyombo vya habari ikishauri viongozi hao kusoma alama za nyakati kama alivyofanya Jose Eduardo Dos Santos wa Angola ambaye mwaka huu aling’atuka kwa hiari baada ya kutawala kwa miaka 38, Cameroon nayo imenyooshewa kidole.

Rais Biya ambaye hadi sasa ametawala miaka 35 tangu aingie madarakani mwaka 1982 na kabla ya hapo Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka saba, tayari wapinzani wake wamesema walikuwa wakifuatilia kwa ukaribu matukio ya Zimbabwe.

Franck Essi, ambaye ni Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha Cameroon Peoples, mapema wiki hii alikaririwa na Shirika la Habari la Reuters akisema viongozi wanatakiwa kusoma alama za nyakati.

“Viongozi lazima waweke kwenye mstari mabadiliko ya kidemokrasia na ya uongozi wa mpito kwa njia ya amani, ambayo itawezesha uongozi mpya. Ikiwa si sasa au baadae, watu walioishiwa pumzi wataamka,” alisema.

Mbali na Biya, Rais wa Uganda, Museveni  ambaye hadi sasa ametawala nchi hiyo kwa miaka 31 tangu alipoingia madarakani Januari mwaka 1986 baada ya kumpindua Idd Amin Dada kwa msaada mkubwa wa Serikali ya Tanzania, naye huenda ametikiswa na tukio la Zimbabwe.

Museveni ambaye Februari mwaka 2016 alichaguliwa kuongoza muhula wa tano licha ya kutuhumiwa kufanya udanganyifu katika uchaguzi ili kujipatia ushindi, saa chache baada ya Mugabe kulazimishwa kuondoka madarakani, Reuters iliripoti kuwa aliandika katika akaunti yake ya tweeter akisema kuwa ameongeza mishahara kwa watumishi wa umma, sambamba na kuliimarisha jeshi.

“Sasa uchumi Uganda umeimarika, Serikali imeweza kuangalia uwezekano wa kuongeza mishahara kwa wanajeshi, watumishi wa umma, afya na walimu na kushughulikia suala la makazi,” aliandika Museveni jambo ambalo Reuters katika uchambuzi wake, imesema alifanya hivyo kwa kuogopa kivuli cha Zimbabwe.

Reuters ilikwenda mbali na kuponda kauli yake na kuhoji uchumi ambao alisema unakua wakati ukuaji wake ni mdogo mno, huku idadi ya watu milioni 37, wengi wao matumizi yao kwa siku ni chini ya dola moja.

Waliojadili mjadala huu, wamekumbusha jinsi ambavyo nyakati zilivyobadilika hasa ikizingatiwa kuwa mwaka huu si tu haukuwa mzuri kwa Mugabe, bali hata kabla ya hapo kwa Yahya Jammeh wa Gambia ambaye utawala wake wa miaka 22 ulihitimishwa na matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mpinzani wake, Adama Barrow wa chama cha United Democratic Party (UDP).

Kwa sababu kama hizo, ukimwacha Museveni, mwingine anayeangaliwa kwa jicho tofauti la uchambuzi wa utawala bora kutokana na kukaa madarakani muda mrefu ni Nguesso wa Congo Brazaville, ambaye ametawala kwa miaka 33 sasa.

Nguesso alitwaa madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 1979 hadi 1992, na kurudi baadaye mwaka 1997 katika kipindi cha mwisho cha vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Machi 2016 alichaguliwa tena kuongoza nchi hiyo  na wachambuzi wa mambo wanasema kuna uwezekano akagombea kwa mara nyingine baada ya kipindi cha sasa kumalizika.

Mjadala wa sasa haujamwacha Rais al Bashir wa Sudan, ambaye naye anatajwa kuliongoza taifa  hilo kwa mwaka wa 28 sasa tangu alipoingia madarakani Juni 1989.

Al Bashir aliingia madarakani alipokuwa Brigedia wa Jeshi na kuongoza kikosi kilichompindua waziri mkuu wake, Sadiq al-Mahdi.

Anayemkaribia Al Bashir ni Rais wa Chad, Deby, ambaye alichukua madaraka Desemba 1990  na hivyo kufanya miaka aliyokaa madarakani kufikia 27 hadi sasa.

Katika orodha hiyo, wamo pia Afewerki wa Eritrea, ambaye amekaa madarakani kwa miaka 24 sasa pasipo kuonyesha dalili za kuachia ngazi.

Wengine ni Bouteflika ambaye ametawala Algeria kwa miaka 18 sasa, sawa na Ismail Omar Guelleh wa Djibouti.

Kagame,  ambaye ametawala Rwanda kwa miaka 17 hadi sasa ingawa amekwishatangaza kuwa anaondoka kipindi cha mwisho hadi mwaka 2024, lakini wachambuzi wanasema lolote linaweza kutokea, kwamba itategemea na upepo utakavyokuwa.

Rais Kabila naye anaingia katika orodha hiyo akiwa ametawala DR Congo kwa kipindi cha miaka 16 na kuna kila dalili za upepo wa Zimbabwe kuivuruga Serikali yake.

Baada ya vuguvugu la kumwondoa Mugabe kuanza, Jean-Pierre Kambila, ambaye ni msaidizi wa  Kabila, aliandika katika ukurasa wake wa tweeter  kuwa maandamano ya Zimbabwe yaligubikwa na ukoloni.

“Maandamano yaliyotengenezwa yalichochewa na wale wote ambao hawakubali uhuru wa Afrika. Akina Mugabe wengine watazaliwa. Hakuna kitu cha kuhangaika,” aliandika.

Itakumbukwa Kabila aliahirisha uchaguzi kwa mara nyingine baada ya kukataa kuachia madaraka jambo ambalo lilizusha maandamano.

Mbali na Kabila, Rais Gnassingbe naye anaingia katika orodha hii akitajwa kuongozwa na kiburi ambacho kimemfanya agome kuondoka madarakani ambako amekaa kwa miaka 12 awali akiwa waziri katika uongozi wa baba yake, ambaye baada ya kufariki akarithishwa nafasi hiyo akisaidwa na Jeshi.

Kama Gnassingbe, Rais Nkurunziza naye amedumu madarakani kwa miaka 12 hadi sasa ingawa mwaka  2015 alinusurika katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi baada ya kushuhudiwa utata mkubwa katika uteuzi wake kugombea urais kwa muhula wa tatu.

Baadhi ya wachambuzi wanasema pamoja na kwamba anguko la Mugabe limeleta mtikisiko barani Afrika, hasa ikizingatiwa kuwa upande wa kaskazini ulikwishashuhudia vuguvugu katika nchi za kiarabu ‘Arab Spring’, licha viongozi wengi wapya kuonekana kupwaya ukilinganisha na wale wa zamani,  bado hakutawafanya wananchi warudi nyuma kudai uongozi unaoheshimu katiba na kuacha kuzifinyanga kwa masilahi binafsi.

WALIOACHA REKODI KUBWA

Ukimwacha Mugabe, viongozi wengine ambao hawako madarakani sasa, lakini wameacha rekodi ya kutawala muda mrefu ni pamoja na Mfalme Haile Selassie ambaye ameongoza Ethiopia kwa miaka 44 kabla ya kutimuliwa madarakani mwaka 1974.

Mwingine ni Rais wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi ambaye alitawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 42 kabla ya kung’olewa mwaka 2011 kwa ushirikiano kati ya majeshi ya Kujihami ya Umoja wa Nchi za Magharibi (NATO) na kikosi cha waasi kutoka Benghazi.

Rais wa zamani wa Gabon, Omar Bongo Ondimba aliongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 41 kabla ya kufariki dunia Juni mwaka 2009.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles