24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Uchaguzi Serikali za Mitaa kuondoka na wakuu wa mikoa

Mwandishi wetu-Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amesema wakuu wa mikoa na wilaya ambao watashindwa kuhamasisha wananchi kujiandikisha, wasimlaumu kwa uamuzi atakaochukua.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu, Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa, Selemani Jafo, atoe orodha ya mikoa na wilaya zilizofanya vizuri kwa siku mbili za kwanza.

Jafo alimwomba Rais kwa mikoa itakayofanya vibaya hadi uandikishaji utakapoisha Oktoba 14, amruhusu ampelekee dokezo juu ya viongozi wa maeneo hayo.

Akizungumza jana mjini Mpanda wakati akihitimisha ziara yake ya siku tisa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Rais Magufuli alisema viongozi wa mikoa na wilaya watakaoshindwa kuhamasisha wananchi kujiandikisha, wasije wakamlaumu.

“Kwa wale ambao hawajajiandikisha, wakajiandikishe kwenye hizi siku chache zilizobaki, jana Waziri wa Tamisemi alitoa takwimu za baadhi ya mikoa ambayo imefanya vizuri sana na wilaya zilizofanya vizuri sana, ninafuatilia.

“Lakini pia alitoa takwimu za mikoa ambayo inazidi kufanya vibaya, ninasubiri mpaka zoezi la uandikishaji litakapokamilika. Nitamuomba tena waziri aniletee taarifa za mikoa iliyofanya vizuri na ile iliyofanya vibaya.

 “Nataka niseme hapa hadharani, ile mikoa na wilaya zitakazokuwa zimezembea kuhamasisha watu wao kujiandikisha kupiga kura, nitawashangaa hao viongozi.

“Na ninaamini Watanzania hawatanilaumu kwa hatua nitakazochukua dhidi yao, mimi nataka watu wajiandikishe wakafanye demokrasia yao, wakachague viongozi wanaowataka kwa ajili ya maendeleo ya kesho,” alisema Rais Magufuli.

Juzi  Jafo alisema kwa tathimini ya Oktoba 8 na 9, Mkoa wa Iringa umefanikisha kuandikisha asilimia 53, Mbeya 34 na  Songwe 33.

Akizungumzia mikoa iliyofanya vibaya, Jafo alisema Dar es Salaam kwa siku mbili hizo iliandikisha wapigakura kwa asilimia nane, Kilimanjaro 12 na Arusha 13.

“Mheshimiwa Rais, wewe unafahamu kwamba ajenda kubwa hivi sasa ni ya uchaguzi, naomba uridhie kwamba endapo siku saba zitakuwa zimekamilika halafu kuna mikoa bado itakuwa haijafika hata asilimia 50, nitaomba nipeleke dokezo maalumu kwako.

“Haiwezekani hata kidogo, katika maeneo haya tuna wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, tuna makatibu tawala, wakurugenzi, maofisa tarafa, watendaji wa kata hadi wa vijiji, ajenda ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndio unatoa mchakato wa maendeleo.

“Naomba uridhie iwapo kuna watu walizembea nitaleta mapendekezo maalumu kwako,” alisema Jafo.

  Awali, akizungumza na waandishi wa habari kutoa tathimini ya uandikishaji, Jafo alisema anatarajia kumwomba Rais Magufuli kuwachukulia hatua wakuu wa mikoa na makatibu tawala, endapo mikoa yao itashindwa kufikisha asilimia 50 ya uandikishaji wapigakura.

Alisema uandikishaji wapigakura ulioanza Oktoba 8, umeonyesha kuna baadhi ya mikoa ambayo hadi sasa imefanya vibaya wakati muda wa kuandikisha unaisha Oktoba 14. 

Jafo alisema hadi sasa jumla ya watu milioni 5.8 wameshajiandikisha ambao ni asilimia 20 huku wanaume wakiwa ni asilimia 51 na wanawake   asilimia 49.

AZINDUA SAFARI ZA ATCL KATAVI

Rais Magufuli katika kuhitimisha ziara yake hiyo ya mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi alizindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) za Dar es Salaam – Mpanda .

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi, alisema shirika hilo litaanza kwa kufanya safari moja kwa wiki na baadaye litaongeza hadi safari tatu kwa wiki kutokana na mahitaji ya usafiri wa ndege kwa wakazi wa Katavi, mikoa jirani na nchi jirani.

Kwa upande wake, Rais Magufuli aliipongeza ATCL kwa kuitikia wito alioutoa siku nne zilizopita, alipoagiza shirika hilo kuanza safari za kwenda Mpanda ndani ya wiki moja baada ya kupokea maombi ya wananchi.

Rais Magufuli alielezea dhamira ya Serikali kuendelea kuimarisha usafiri wa anga kwa wananchi na kukuza uchumi kupitia utalii, biashara, uwekezaji na kwamba ndege nyingine mpya itawasili nchini baadaye mwaka huu.

Alisema Serikali imenunua ndege nyingine tatu kwa lengo la kuimarisha zaidi usafiri wa anga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles