23.4 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI KENYA 2017: Kenyatta kumwangusha tena Raila Odinga?  

president-uhuru-kenyattaNa Dorine Otinga, Nairobi

JE, hatima ya Kenya katika uchaguzi wa 2017 ni ipi? Hili ni swali sugu ambalo kila Mkenya anasubiri jibu lake kwa hamu. Uchaguzi wa urais ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yoyote. Ni ndoto ya kila mmoja kuishi katika maeneo yenye haki, usawa na amani. Kenya inapitia hatua muhimu inapojiandaa katika uchaguzi wa urais wa 2017.

 

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)

 

Hii ni tume ambayo hujihusisha na shughuli za kuhesabu kura katika uchaguzi nchini Kenya. Mnamo Mei mwaka huu, kulikuwa na ghasia zilizotokana na maandamano katika mji mkuu wa Nairobi na kusababisha vifo vya watu watatu.

Maandamano haya yalisababishwa na wafuasi wa chama cha CORD ambacho kinara wake ni Raila Odinga. Sababu kuu ya maandamano hayo, ni kwamba walitaka serikali ifanye mabadiliko katika tume hii ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

IEBC ilidaiwa kuunga mkono chama tawala na kupanga kukisaidia kwa kutumia ulaghai kwenye uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika mwaka ujao. Kufuatia hayo, IEBC ilitakiwa kujiuzulu na viongozi wa upinzani wa CORD. Upinzani ulihisi kwamba, makamishna wa IEBC walihusika na udanganyifu wa kura za urais mwaka 2013.

Hatimaye, makamishna wa Tume huru ya Uchaguzi Kenya, walisema wako tayari kujiuzulu. Makamishna hao tisa, wakiongozwa na mwenyekiti wao, Isaac Hassan, waliafiki uamuzi huo mbele ya kamati ya pamoja katika Bunge la Taifa na Seneti, iliyobuniwa kupokea shutuma dhidi yao na pia mapendekezo ya jinsi ya kuimarisha shughuli za uchaguzi nchini Kenya.

 

Kamati yasaka makamishna wapya wa IEBC

Huenda Kenya ikapata makamishna wapya wa IEBC wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi Desemba mwaka huu, iwapo jopo maalumu la kutafuta makamishna hawa litafikia malengo yake.

Oktoba 21, mwaka huu Mwenyekiti aliyechaguliwa kusimamia zoezi la kuwapata Makamishna wa IEBC, Bernadette Musundi,  alisema kwamba jopo hilo litachapisha taarifa kwa wanaotaka nafasi hiyo.

Jopo hilo linatarajia kukamilisha zoezi hilo Novemba mwaka huu, na siku hiyo pia watamkabidhi Rais Uhuru Kenyatta orodha ya watakaohitimu kuwa makamishna wa IEBC.

Shughuli ya kutafuta makamishna wapya wa kusimamia uchaguzi imeanza kushika kasi baada ya nafasi hizo kutangazwa wazi mnamo Oktoba 25, 2016. Taarifa zinasema wananchi wana siku 14 za kuwasilisha maombi ya nafasi hizo na siku ya mwisho ya kuwasilisha ilikuwa Novemba 7, mwaka huu.

 

Maandalizi ya Jubilee

 Rais Uhuru ana mpango upi ili apate ushindi katika uchaguzi wa urais wa 2017? Chama cha Jubilee ni mojawapo ya vyama vinavyovuma nchini Kenya kisiasa. Kinara wa Jubilee ni Rais Kenyatta.

Mojawapo ya mipango yao katika uchaguzi wa Urais wa 2017, ni kufungua ofisi  zao katika kaunti 47. Rais Kenyatta ana kibarua kikubwa katika kukipigia debe chama chake katika kaunti hizi.

Kuna mpango tayari wa kuhakikisha kwamba vyama vidogo vinavyounda Jubilee vinakubaliana kuhusu maofisa wa chama hicho kote nchini.

Mnamo Septemba 10, mwaka huu, Rais  Kenyatta pamoja na Naibu wake, William Rutto, walizuru uwanja wa Kasarani mjini Nairobi na kukutana na wafuasi wao.

Katika eneo la Magharibi mwa Kenya, litakuwa jukumu la vyama kama vile New Ford Kenya (NFK) na United Democratic Front (UDF), kuafikiana kuhusu watakaoteuliwa kuwa maofisa wa chama cha Jubilee.

Kando na hayo, wenyeviti kutoka matawi 47, watatengeneza baraza kuu la Jubilee Party, ambalo litaendesha shughuli za kila siku za chama. Wanasiasa wawili kutoka maeneo yote nane watafanya kazi pamoja na Rais Kenyatta na Naibu wake Rutto, ili kutengeneza kamati kuu tekelezi ya chama.

Kulingana na ripoti iliyochapishwa katika mtandao wa habari wa Star, Rais Kenyatta na Naibu wake watazuru kaunti 47 ili kukutana na viongozi wa vyama na kukiuza chama hicho kabla ya uchaguzi wa 2017. Ziara hizo za kaunti zitaanza mwishoni mwa mwaka huu.

 

Raila Odinga amejiandaa vipi?

Kinara wa chama cha CORD, Odinga, kwa muda mrefu amekuwa akitoa upinzani kwa chama tawala. Ilikuwa bahati mbaya sana kwake, kwani kila mara amekuwa akishindwa kutimiza ndoto yake ya kuingia Ikulu.

Inapendeza sana jinsi bingwa huyu wa siasa hafi moyo kisiasa, kwani anaonekana kila mara akiinyooshea serikali mkono wa lawama iwapo kumetokea sakata lolote la wizi au utenda kazi hafifu.

Katika chama hiki cha CORD, kulikuwa na mvutano kuhusu nani anastahili kupeperusha bendera ya muungano huo, dhidi ya muungano wa Jubilee.

Hata hivyo, katika mahojiano nyumbani kwake kule Karen Nairobi, Raila alisema kwamba yuko tayari kumuunga mkono yeyote atakayesimamia kiti cha ugombea urais katika chama cha CORD ili kumshinda Kenyatta.

Raila Odinga alikuwa katika ziara eneo la pwani katika mpango wa kuuza chama cha ODM ili kuimarisha uungwaji mkono wa chama hicho katika uchaguzi wa mwaka 2017.

Kiujumla Rais Kenyatta amejaribu kila awezavyo kuwa kiongozi bora. Hata hivyo, serikali yake imekumbwa na changamoto nyingi sana, mojawapo ikiwa ni ufisadi, ugaidi na mengine mengi. Wakenya wengi wanamtizama kwa jicho la karibu sana kulingana na namna anavyojaribu kukabiliana na changamoto hizo.

Viongozi wa fedha wa mataifa mbalimbali ulimwenguni wamempongeza Rais Kenyatta kwa mtazamo na uongozi bora ambao wanasema ni muhimu katika ukuaji wa bara la Afrika.

Kiongozi wa Benki ya Dunia na African Development Bank (AFDB) alisema sera za Kenya zilizoanzishwa na Rais Kenyatta zimeweka mazingira mazuri ambayo yamechangia uwekezaji na biashara kati ya mataifa ya Afrika.

Maoni: +254 716 955356

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles