31.1 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Ubunge viti maalumu CCM usipime

Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza mchakato wake wa ndani wa uchaguzi kuwapata wagombea ubunge wa majimbo, viti maalumu na udiwani.

Mchakato huo umeanza huku Bunge la 11 likiwa limebakiza vikao viwili vya uhai wake na hatimaye kuvunjwa, huku kila mmoja akielekea kutupa karata yake ili kutafuta ridhaa kwenye chama.

UBUNGE VITI MAALUMU

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi wa ndani ambayo imeshushwa kwa viongozi wa CCM wa mikoa na wilaya, wanaotaka kugombea ubunge kupitia viti maalumu, wametakiwa kuzingatia mambo matano muhimu, ikiwamo kila mgombea ni lazima awe na wadhamini 250 katika mikoa isiyopungua mitatu na kati ya hiyo angalau mmoja uwe kutoka upande wa Unguja au Pemba.

Sharti hilo la kutakiwa kutafuta wadhamini katika mikoa mitatu ikiwamo mmoja wa upande wa Zanzibar, inaonekana ni wazi kwamba linakwenda kuamsha vita ya kusaka kuungwa mkono kwa wagombea hao, ambao tayari kila mmoja ameanza kupiga hesabu za uchaguzi huo.

Sehemu ya masharti hayo kwa wagombea ubunge pamoja na wadhamini wao, ni kupigwa marufuku kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutomdhamini mgombea urais wa Zanzibar.

“Wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya Taifa hawaruhusiwi kumdhamini mgombea urais wa Zanzibar. Mwanachama haruhusiwi kumdhamini zaidi ya mgombea mmoja.

“Fomu ya udhamini ya wanachama ithibitishwe na Katibu wa CC wa wilaya kwa kupigwa muhuri wa chama wa wilaya husika. Na wanachama watakaomdhamini mgombea, unachama wao uthibitishwe na Katibu wa CCM wilaya husika,”  ilieleza sehemu ya maelekezo hayo kwa wana CCM.

Hata hivyo, ratiba hiyo pia inawataka wagombea ubunge kutambua kwamba wana wajibu wa kuzingatia maelezo na miiko ya chama, huku wale ambao watakiuka wapo hatarini kuenguliwa.

Kwa upande wa ubunge viti maalumu fomu zitaanza kutolewa kuanzia Julai 16 hadi 20, na Julai 23 vikao vya kamati za siasa vitakaa na kuanza kuwajadili wagombea kwa kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mikoa.

“Julai 25, vikao vya kamati za siasa za mkoa kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar kutoa mapendekezo kwa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar.

“Julai 27, 2020 Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu na Julai 30, kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuwajadili wagombea na kufanya uteuzi wa mwisho.

“Agosti 2 hadi 4, 2020 kupiga kura za maoni Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya/Jimbo kwa upande wa ubunge. Agosti 5, 2020 vikao vya kamati za siasa za wilaya kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mikoa huku Agosti 6 ikiwa ni vikao vya kamati za siasa za mkoa kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar kutoa mapendekezo kwa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar.

“Agosti 7, Halmashauri Kuu za mikoa kufanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea udiwani. Na Agosti 9, 2020 Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya CCM Taifa,” ilieleza taarifa hiyo ya CCM.

Pamoja na hayo, imeeleza Agosti 12 hadi 13 Kamati Kuu ya Taifa itawajadili wagombea ubunge na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu.

“Agosti 8, 2020 Halmashauri Kuu itawajadili na kufanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea ubunge,” ilieleza taarifa hiyo.

KATIBU MKUU UWT

MTANZANIA ilipomtafuta Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho, Mwalimu Queen Mulozi, ili kupata ufafanuzi wa ratiba hiyo kwa wagombea ubunge wa viti maalumu, alisema kwa sasa hawezi kusema chochote, anasubiri maelekezo ya chama.

“Kwa sasa siwezi kusema lolote katika hilo ila ninasubiri maelekezo ya chama taifa,” alisema Mulozi.

VITA YA UDIWANI

Wakati ratiba hiyo ambayo gazeti hili linayo nakala yake ikisambazwa kwa viongozi mbalimbali wa mikoa na wilaya wa CCM, viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya wameanza vikao vya wanachama na kuwahamisha uchukuaji wa fomu wakati ukifika na kukemea utoaji rushwa kwa baadhi ya makada wake.

 Halmashauri mbalimbali nchini kwa sasa zinafanya vikao vyake vya lala salama ikiwamo kupitisha bajeti zake za mwaka wa fedha 2020/21, huku madiwani waliopo wakitarajiwa kukabiliana na upinzani mkali katika kuwania kuteuliwa tena kugombea nafasi hiyo.

Ratiba hiyo inaonesha kwamba kuanzia Julai 16 hadi 20, mwaka huu uchukuaji wa fomu kwa wanaotakuwa kuwania udiwani utaanza na mwisho wa kurejesha itakuwa Julai 20, saa 10 jioni.

Baada ya hatua hiyo, hatua inayofuata ni vikao vya kamati za siasa za ngazi za kata na wadi kwa upande wa Zanzibar Julai 21, ambavyo vitatoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za wilaya na majimbo kwa upande wa Zanzibar.

“Julai 22, mwaka huu vikao vya kamati za siasa za jimbo kwa upande wa Zanzibar vitapendekeza wagombea udiwani. Na Julai 23 vikao vya kamati za siasa wilaya vitajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mikoa.

“Julai 24 Mkutano Mkuu wa UWT kuchagua madiwani wa viti maalumu wanawake. Na Julai 25, mwaka huu vikao vya kamati za siasa za mikoa kupendekeza wagombea kwa ajili ya kupigia kura za maoni.

“Agosti 1, 2020 kura za maoni za udiwani kupigwa. Na Agosti 3 vikao vya kamati za siasa za kata/wadi na jimbo kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za Siasa za Wilaya.

“Agosti5, 2020 vikao vya kamati za siasa za wilaya kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mikoa. Agosti 6, vikao vya kamati za siasa za mikoa kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa halmashauri kuu za mikoa.

“Huku Agosti 7, 2020 vikao vya halmashauri za mikoa kuwajadili wagombea na kufanya uteuzi wa mwisho,” ilieleza ratiba hiyo.

Hata hivyo, wagombea wote wametakiwa kuzingatia kwamba watalazimika kuzingatia maadili ya Chama Cha Mapinduzi na miiko ya uchaguzi ndani ya chama.

KAULI YA DK. BASHIRU

Kutokana na kile kinachoonekana kuwiva kwa mchakato wa kuwapata wagombea ndani ya CCM, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally, amewaonya wanachama waliogeuza uchaguzi ni sawa na soko la kununua au kuuza kura huku akisema sasa hawana nafasi.

Kauli hiyo amekuwa akitoa mara kwa mara ambapo hivi karibuni katika ziara yake katika mikoa ya Tanga na Kigoma, alivitaka vikao vya uteuzi kutenda haki kwa wagombea wote ikiwamo viongozi kuacha chuki.

Pamoja na hilo, alisema chama hicho hakitamwacha yeyote atakayehusika katika rushwa, wakati kikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Alisema matokeo ya rushwa katika kutafuta nafasi za uongozi yamekuwa na maumivu kwa wagombea na kusababisha kupata viongozi wasiostahili, ambao mwisho wake hawawezi kuwa watumishi wa wananchi.

“Rushwa inayotumika kwenye soko la kununua kura imewaumiza wengi. Imeumiza wote, walioshinda na walioshindwa kwa sababu wote wanajikuta katika madeni.  Walioshindwa hawana raha wanaendelea kuugulia wakiwa hawajui ni kwa namna gani watarejesha kile walichopoteza.

“Kwa upande wa walioshinda, pia wanakuwa hawana raha, muda wote wanawaza kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa madeni. Hawawezi kuwa na muda wa kuwasikiliza na kuwatumikia waliowachagua kwa kuwa wanaona kuwa wamenunua nafasi hizo,” alisema Dk. Bashiru.

Alisema kwa sasa chini ya uenyekiti wa Rais Dk. John Magufuli chama hicho kinahakikisha kuwa utaratibu wa soko la kura unakwisha ili kutoa nafasi kwa wanachama wenye uwezo na nia wajitokeze na kuomba kuchaguliwa kupitia mifumo halali isiyoruhusu rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles