23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

NIMR kusimika mitambo ya kuzalisha dawa ya tezi dume

Aveline Kitomary -Dar es Salaam

TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), inatarajia kusimika mitambo yenye uwezo wa kuzalisha dawa za mitishamba kuongeza uwezo wa kukabiliana na magonjwa mbalimbali yakiwamo selimundu (sickle cell) na tezi dume. 

Akizungumza wakati wa kampeni ya ‘Tumeboresha sekta ya afya’ iliyoandaliwa na maofisa habari wa taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya, alisema mitambo hiyo itakuwa bora zaidi na itagharimu Sh milioni 600.

Alisema hadi sasa wameshatengeneza fomula ya dawa ya mitishamba kuzalisha dawa za tezi dume na selimundu.

 “Mashine hizo zikifika kazi yake ni kuzalisha dawa zinazotokana na fomula hizo na nyingine zikiendelea kutengenezwa.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya walitupa Sh milioni 800, lakini tulipata fedha nyingine kutoka Costech (Tume ya Sayansi) ambao wametupa Sh milioni 400 kwa ajili ya kukarabati maabara zetu.

“Watafiti wameshatuambia ni maeneo gani yanatakiwa kufanyiwa utafiti. Tuna tafiti ambazo zinaangalia dawa zinazotengenezwa maabara za kemikali, namna ya kukinga au uwezekano wa kutumia mitishamba ili kutibu magonjwa,” alisema Profesa Mgaya. 

Alisema lengo la uzalishaji wa dawa hizo ni kuongeza kiwango cha matumizi ya dawa za mitishamba zenye uwezo mkubwa nchini.

“Zipo nchi duniani zinatumia dawa za mitishamba tu, nchi kama China, India, Korea na hata Amerika ya Kusini, lakini hata hapa kwetu watu wengi wanatumia dawa hizo, tunataka sasa ziboreshwe na ziwe na vipimo sahihi ili ziwasaidie wananchi, hivyo tutaendelea kushirikiana na waganga wa dawa asili ili kuziboresha,” alifafanua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NIMR Muhimbili, Profesa Sayoki Mfinanga, alisema hadi sasa wamefanikiwa kufanya tafiti zenye mafanikio makubwa kwenye ugonjwa wa kifua kikuu, vimelea vya Ukimwi na magonjwa yasiyoambukiza.

“Uwezo wa kituo kufanya utafiti umeongezeka kutoka wastani wa tafiti kubwa 10 kwa miaka ya 2010 mpaka wastani wa tafiti kubwa 20 kwenye miaka ya kuanzia 2017. Pia tumeboresha ubora wa vipimo vya maabara ya kitaifa ya kifua kikuu. 

“Tumefanya utafiti wa VVU, hasa kwa upande wa tiba ya homa ya uti wa mgongo inayosababisha fangasi kwa wagonjwa wa VVU kwani huchangia vifo kwa asilimia 25 kwa wagonjwa walioathirika.

“Utafiti huo ulihusisha wagonjwa 721 kutoka nchi tofauti barani Afrika. Mpango huo umefanikiwa kupunguza vifo kwa wastani wa robo tatu ya kila wagonjwa 100 waliotibiwa.

“Utafiti huo ulifanywa WHO kuunga sera mpya ya kutumia michanganyiko ya dawa hizi kutibu homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na fangasi,” alieleza Profesa Mfinanga.

Alisema utafiti uliofanyika pia umesaidia kushauri na kudhibiti usugu wa vimelea kwa dawa zinazotumika kutibu kifua kikuu.

“Tafiti iliyofanyika mwaka 2017 mpaka 2018 kwa kuhusishwa wagonjwa wapya na wanaorudia  1,557 inaonyesha viwango vidogo vya usugu wa dawa kwa vimelea vya kifua kikuu.

“Usugu wa dawa madhubuti maarufu kwa jina la MDR  TB ni asilimia 1.2 ambapo wagonjwa wapya ni asilimia 0.8 na wanaorudia matibabu ni asilimia 4.6.

“Matokeo hayo tofauti na tafiti tulizofanya mwaka 2007, zilionyesha kuwa usugu kwa dawa madhubuti kati ya mchanganyiko wa dawa za kutibu kifua kikuu (MDR) ni asilimia 1.1 kwa wagonjwa wapya na wanaorudia matibabu ni asilimia 4.6,” alifafanua Profesa Mfinanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,712FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles