Na Nora Damian, Dar es Salaam
Wanawake wajasirimali 100 kutoka katika Wilaya ya Ilala wamepatiwa mafunzo ili waweze kuachana na mikopo umiza ambayo imekuwa ikiwafanya kuwa watumwa katika biashara zao.
Mafunzo hayo yametolewa na Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha kuwainua wanawake nchini (Tuwodo) yakilenga kukuza uelewa wao katika masuala ya biashara, masoko na fedha.
Akizungumza jana wakati wa kongamano hilo Mkurugenzi wa Tuwodo, Awena Omary, alisema wanawahamasisha wajasiriamali wanawake kujiunga kwenye vikundi na kuvisajili ili waweze kutambulika kisheria na kukopesheka kwenye taasisi zenye riba nafuu kuepuka mikopo inayowaumiza.
“Kuna mikopo ya kausha damu ambayo imekuwa tatizo kubwa kwa wajasiriamali wadogo wadogo, wanaathirika kwa kutozwa riba kubwa na kufanywa kuwa watumwa katika biashara zao. Tunawapa elimu ili waweze kuachana nayo,” alisema Awena.
Alisema pia wamekuwa wakiwapa mafunzo ya kuweka akiba, kukuza mitaji, elimu ya biashara ya masoko, umuhimu wa kutumia nishati safi katika kujiletea maendeleo na kuacha kutumia kuni na mkaa ambao unachangia uharibifu wa mazingira.
Mkurugenzi huyo alisema wana mikakati ya kuendesha makongamano mengine katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ili kuendelea kuwainua wanawake kiuchumi na wafanyabiashara wadogo wadogo.
Naye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Ilala, Neema Kihusa, alisema Serikali inafanya jitihada kubwa kuwakomboa wanawake kiuchumi na kwamba kwa Dar es Salaam zimetengwa Sh bilioni 14 kwa ajili ya wanawake wajasiriamali.
“Kelele nyingi tunazokutana nazo ni mikopo ya asilimia 10, hili halikwepeki lakini kwa jinsi Rais Samia anavyowapenda wanawake wa Tanzania mikopo hii imerudi na itaanza kutolewa,” alisema Kihusa.
Katika kongamano hilo mada mbalimbali zilitolewa na wataalam waliobobea katika masuala ya ujasiriamali na uchumi huku wajasiriamali hao wakisisitizwa kuwa na nidhamu ya muda kuepuka kukimbiwa na wateja na kuwa na nidhamu ya fedha.