26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAWATAKIA WATANZANIA HERI YA MWAKA MPYA

2017

KESHO Watanzania wote wanaungana pamoja kila kona ya nchi hii kusherehekea sikukuu ya kuanza mwaka mpya wa 2017.

Kama ilivyokuwa siku ya Krismasi  Jumapili iliyopita, viongozi wa familia watawaongoza na kuwahimiza wanafamilia nchini kote kwenda kuhudhuria ibada makanisani na misikitini kumshukuru Mungu kuwapitisha salama katika mwaka huu 2016 uliokuwa na matatizo mengi, yakiwamo mafanikio waliyopata wakati wa kuhangaika na maisha yao.

Kwa vyovyote vile ibada hizo zitakwenda sambamba na mahubiri mbalimbali kutoka kwa viongozi wa kidini ambao watazungumzia kuheshimu na kuendelea kumshukuru Mungu kuwawezesha kuuona mwaka mpya na kuendelea kushiriki katika masuala mbalimbali yanayoisibu nchi yetu kwa sasa.

Tunaomba sana Mungu awawezeshe Watanzania wote wa nchi hii na watu wote ulimwenguni kwa ujumla wao kuweza kuuona mwaka mpya.

Aidha, Watanzania wote tunawasihi waonyeshe ushirikiano katika kila hatua ya sherehe hizo kwa upendo mkubwa unaoashiria undugu.

Kama inavyofahamika, sikukuu ya mwaka mpya ni siku ya kukumbuka yale yote yaliyotokea mwaka uliopita na kujiandaa kupambana na yatakayojili mwaka mpya.

Kwa Mtanzania atakayebahatika kuiona siku ya kesho, kwake hii itakuwa siku ya furaha kubwa, siku ya kufanya ibada na kushukuru kwa kuiona akiwa mzima au kwa namna yoyote aliyo nayo. Pia itakuwa siku ya kula na kunywa kwa kadiri mtu awezavyo na kwa kadiri atakavyojaliwa na Mungu.

Hii ina maana kuwa ni kula vyakula na kunywa vinywaji kwa kiwango kinachokubalika bila kupitiliza ili kutoleta usumbufu.

Siku ya mwaka mpya ni fursa ya toba na ya kusherehekea kwa kauli njema na kukumbushana kuendeleza mema siku zote katika jamii.

Haitarajiwi kwa namna yoyote kusikia mahali na eneo lolote la nchi hii, na dunia kwa ujumla wake, taarifa yoyote mbaya inayomchukiza Mungu kufanywa na Mkristo, Mwislamu au mtu mwingine yeyote kwa kisingizio cha furaha iliyopitiliza au ulaji na unywaji uliokithiri.

Tunawakumbusha Watanzania wote kuwa sherehe hizi ziendane na kutoa misaada kwa yatima, wajane, wagonjwa, masikini na wengine wote wenye kuhitaji.

Vilevile siku ya kesho iwe siku ya kudhihirisha mshikamano wa kitaifa kwa kuonyesha ushirikiano na madhehebu mengine kwa sababu binadamu wote ni wana wa Mungu mmoja.

Kwa hiyo wakati wakisherehekea mwaka mpya, ni muhimu kwa Watanzania wote nchini kuyakumbuka yote haya ili sherehe za kusindikiza siku hii ziwe chagizo ya upendo, mshikamano, undugu na umoja wa kitaifa.

Pia iwe siku ya kila mmoja kuangalia alichokifanya mwaka uliopita, alivyofanikiwa na matatazo aliyokumbana nayo ili ajiwekee mkakati wa kufanikiwa zaidi bila matatizo kama hayo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Mhariri Mtendaji Mkuu, wahariri wote na wafanyakazi wa New Habari (2006) Ltd katika ujumla wao wanachukua fursa hii kuwatakia Watanzania wote heri ya mwaka mpya wa 2017 na baraka tele.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles